Sambaza....

Yeah! , natamani sana aje leo hii. Natamani sana arudi kwenye mbuga ya msimbàzi. Mbuga yenye mnyama mmoja tu, Simba.

Tena Simba mwenye rangi mbili, rangi nyeupe na rangi nyekundu. Mbuga ambayo Pierre Lenchantre aliwahi kuwa mhifadhi mkuu kwa muda wa miezi 6.

Muda ambao kuna jambo moja kuu alinifundisha ambalo kwa sasa halipo ndani ya kikosi cha Simba na ninatamani kwa sasa kiwepo.

Kwanini natamani sana kiwepo kwa muda huu ?, jibu ni moja tu muda huu Simba wanakihitaji zaidi kuliko muda wowote ule.

Hakuna kipindi ambacho walikihitaji hiki kitu lakini kipindi hiki ndicho wanakijitaji hiki kitu tena kwa nguvu zote.

Unakumbuka mechi ya kimataifa ya msimu jana ya kombe la shirikisho barani Afrika kati ya Simba na Al Masry katika uwanja wa nyumbani na ugenini ?

Unaikumbuka vizuri?, unaikumbuka mvua kubwa iliyonyesha siku ile kwenye uwanja wa taifa na unakumbuka tukio la umeme kukatika kwenye uwanja wa Taifa ?

Bila shaka unakumbuka vizuri sana, na matokeo yalikuwa ni 2-2. Kuna kitu kingine cha muhimu ambacho nataka kukumbusha ambacho ndicho msingi wa makala hii.

Unaikumbuka safu ya kiungo ya Pierre Lenchantre ambayo ilikuwa imepangwa siku hiyo ?. Ngoja nikukumbushe kidogo.

Siku ile Jonas Mkude, Shomari Kapombe na Shiza Kichuya walicheza kama viungo wa kati. Na ndiyo siku ile Pierre Lenchantre alitaka kumtoa Shiza Kichuya lakini wachezaji wakamuomba wasimtoe.

Matokeo yalikuwa 2-2. Lakini umegundua kitu kwenye hicho kiungo cha kati. Ngoja nikufunue kidogo.

Jonas Mkude ni mchezaji wa kiungo cha kuzuia, Shomari Kapombe ni beki na Shiza Kichuya ana sifa mbili kuu ambazo wengi huwa wanazipenda kutoka kwake.

Anashambulia na kukaba. Kila mahali yupo , ana hardwork kubwa sana ndani ya uwanja kwa hiyo ana faida kubwa sana kipindi timu ikiwa na mpira na kipindi ambacho timu haina mpira (yani kukaba).

Twende taratibu tu rafiki yangu. Hapa Pierre Lenchantre alipanga wachezaji ambao wana asili kubwa ya kuzuia katika eneo la katikati.

Hata kipindi alipoenda kucheza katika mechi ya marudiano kule Misri, Pierre Lenchantre aliwapanga hao hao watu watatu katika eneo la katikati.

Na Simba hii ambayo imefuzu katika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa msimu huu haijawahi kucheza vizuri ugenini msimu huu ukilinganisha na Simba ile ya Lenchantre iliyocheza Misri.

Lengo lao kubwa lilikuwa kuzuia, kuendana na presha ili wasitoke mchezoni na kuhakikisha wanapata goli ambalo lingewasaidia.

Lengo Mama la kuzuia walifanikiwa sana. Walizuia vyema. Hata kipindi ambacho timu ilikuwa inaonekana iko kwenye presha kubwa ya kushambuliwa ilikuwa na utulivu sana.

Haikutoka nje ya malengo yao kisa tu wanashambuliwa sana. Walifanikiwa kutembea ndani ya ile presha kubwa ambayo walikumbana nayo siku ile.

Ratiba ya Ligi ya Mabingwa iliyotoka hivi karibuni

Na mwisho wa siku matokeo yalikuwa 0-0 na Simba ikicheza mchezo bora ugenini , mchezo ambao Simba hii ambayo ni bora haijawahi kuucheza msimu huu kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika.

Kwenye hatua ya awali hawakufungwa hata goli moja kwenye uwanja wa ugenini dhidi ya Mbabane Swallows.

Wakaenda Zambia kucheza na Nkana na kufungwa magoli 2-1. Na kwenye hatua ya makundi hali ilikuwa ngumu sana kwao.

Walifungwa 5-0 na As Vita, wakaja kufungwa 5-0 na Al Ahly na wakafungwa 2-0 na Soura. Yani kwa kifupi katika mechi tano za ugenini msimu huu kwenye ligi ya mabingwa wamefungwa magoli 14.

Wanaenda kwenye hatua ya mtoano. Hatua ambayo ni tofauti sana na hatua ya makundi. Hatua ambayo ukiruhusu kufungwa magoli mengi ugenini unakuwa na mlima mrefu wa kupindua matokeo.

Unatakiwa ujue kucheza ugenini. Hapa ndipo jina la Pierre Lenchantre linapokuja kichwani mwangu. Hapa ndipo mechi kati ya Simba na Al Masry inapojirudia.

Ile mechi iliyochezwa Misri, mechi ambayo Simba ilicheza kwa nidhamu na malengo mazuri ugenini.

Kitu ambacho kwa sasa hakipo kabisa ndani ya kikosi cha Simba kwenye mechi za ugenini kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika.

Sambaza....