Sambaza....

Tanzania ishawahi kubarikiwa washambuliaji wengi wazuri wa kati . Inawezekana kizazi hiki kipya kinaweza kisikuelewe sana kama ukiamua kutaja washambuliaji bora wa zamani na kikakuelewa sana unapoamua kutaja washambuliaji wa kisasa .

Kwenye ligi yetu kuna washambuliaji bora wa kati kwenye siku za hivi karibuni ambao walikuwa tishio na bado ni tishio kwa kiasi kikubwa. Ligi yetu haiwezi kumsahau Makambo , mshambuliaji ambaye aliibeba Yanga mgongoni kwake kipindi Yanga ina njaa.

Kwa sasa Meddie Kagere ndiye mshambuliaji anayetisha na kuogopeka na magolikipa kwa kiasi kikubwa kwa sasa. Huyu ni rafiki mkubwa wa nyavu za magoli na ni adui mkubwa wa magolikipa kwenye ligi kuu Tanzania bara kwa sasa.

Hawa wote niliowataja ni wachezaji ambao wanatoka nje ya nchi . Kwa bahati mbaya nchi yetu haijawahi kubahatika kuwa na mshambuliaji wa kati ambaye ana mwendelezo mzuri tangu aondoke Athuman Machupa , Mussa Hassan Mgosi na Eliud Ambokile.

Mfungaji Bora mwezi wa Tisa wa ligi Kuu Tanzania bara, Eliud Ambokile, akiwa na zawadi yake kutoka katika tovuti ya kandanda ya kumpongeza.

Kwa sasa amebaki mshambuliaji mmoja tu ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri kwenye ligi kuu Tanzania bara akiwa kama mchezaji mzawa wa Tanzania tofauti na wachezaji wengine wazawa wa Tanzania ambao huvuma kwa msimu mmoja na msimu mwingine hawavumi .

Hii imekuwa tofauti sana kwa John Bocco ambaye amekuwa mchezaji mwenye mwendelezo mzuri kwenye ligi yetu ya Tanzania bara akiwa kama mchezaji  mzawa, tofauti na wachezaji wazawa wengine ambao hucheza eneo la ushambuliaji wa kati.

John Bocco akishangilia goli baada ya kuifunga Lipuli fc.

Msimu uliopita alikuwepo Salim Aiyee ambaye mpaka sasa hivi hajafanya vizuri ukilinganisha na msimu uliopita . Hii imekuwa tofauti kwa John Bocco , misimu kumi na moja kwenye ligi kuu Tanzania bara huku akiwa amefanikiwa kufunga magoli zaidi ya mia moja.

Amekuwa mchezaji mahiri na bora sana kwenye ligi kuu Tanzania bara , leo hii yupo Simba Sports Club , sehemu ambayo hakuanzia safari yake ya mpira wa miguu. Safari yake ilianzia Azam Football Club.

Bocco akiwa Azam Fc, alifunga mabao 84

Sehemu ambayo alianza nayo kuanzia ligi daraja la kwanza na akafanikiwa kuipandisha ligi kuu Tanzania bara , Azam Football Club.  Amekaa Azam Football Club zaidi ya misimu saba akiwa kama nahodha na mchezaji mwandamizi wa kikosi hiki .

Jasho lake jingi lilivuja akiwa  Azam Football Club,  jasho ambalo lilianza kutiririka tangu akiwa ligi daraja la kwanza mpaka ligi kuu Tanzania bara . Inawezekana Azam Football Club haikufanikiwa kumpa mafanikio ya mechi za kimataifa kama Simba.

Timu ambayo amefanikiwa kufika nayo mpaka kwenye hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu uliopita.  Hatua ambayo hakuwahi kufika akiwa Azam Football Club,  lakini kuna vitu viwili ambavyo vinampa sababu John Bocco kwenda kustaafu mpira wake akiwa na jezi ya Azam Football Club.

Hii ndiyo timu ambayo imemtambulisha John Bocco , tangu ligi daraja la kwanza mpaka ligi kuu Tanzania bara. Azam Football Club ilimwamini John Bocco ikampa nafasi kubwa kwenye kikosi chao,  na nafasi ilikuwa nafasi ya heshima kwa sababu alikuwa mpaka nahodha wa Azam Football Club.

Hiyo ni sababu ya kwanza . Sababu ya pili na ya muhimu ni kuitumikia kwa muda mrefu Azam Football Club. Kama nilivyokuambia John Bocco jasho lake limetiririka kwa wingi akiwa Azam Football Club tangu akiwa ligi daraja la kwanza.

Anajua shida na raha zote za Azam Football Club,  wakati anaondoka Azam Football Club hakuondoka vizuri . Hakuagwa vizuri na viongozi wa Azam Football Club kama mmoja ya wachezaji muhimu waliowahi kutokea kwenye timu yao , kwa hiyo ni busara kwa John Bocco kurudi kwa kustaafu kwa heshima akiwa Azam Football Club miaka ijayo ambayo ataamua kustaafu soka.

Sambaza....