Ardhi yetu inakila aina ya baraka, ina kila aina ya uzuri. Kwa kifupi nchi yetu imebarikiwa sana. Kuna vingi sana vya kujivunia ndani ya nchi yetu. Mungu alileta amani na kuifanya nchi yetu iwe kisiwa cha amani. Tunajivunia amani ambayo tuko nayo, tunajivunia utulivu tulionao. Hakutunyima vitu vingi vizuri. Hata vivutio vya utalii aliviweka hapa ili viweze kuvuta watu wa mataifa kuja kukanyaga ardhi yetu. Mtu asipoletwa na mlima Kilimanjaro, basi hifadhi ya kuu ya Serengeti itamleta. Serengeti isipomleta basi Ngorongoro itamleta, ili mradi tu aje afurahie zawadi kubwa ambayo mwenyezi Mungu alitupa sisi.
Tanzania ambayo iliwahi kuishi na Shaban Nonda. Ilimpa hifadhi, ingawa hatukumtazama katika kiwango kikubwa ila ni yeye pekee alijitazama katika kiwango kikubwa. Alijua ni kipi ambacho ameamua kukifuata katika ardhi hii ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndiyo maana aliishi Tanzania kwa malengo. Hakutaka kabisa kupatazama Yanga kama sehemu sahihi kwake yeye kukaa. Alipaona kama daraja la yeye kufika sehemu ambayo ni bora zaidi ya Yanga.
Ndicho kitu ambacho alitembea nacho, akakimbia nacho. Hakuwahi kukiacha hata siku moja. Alikiamini sana hicho kitu na kila alipokuwa anaingia uwanjani nafsi yake ilizungumza na yeye kuwa Tanzania ni sehemu ya kupita kama watalii wanavyokuja na kuondoka.
Aliupa nafasi muda, alikuwa na subira huku akipigana na kusubiri muda sahihi kwake yeye kuondoka Tanzania ili aende sehemu ambayo ni bora zaidi. Ndivyo hivo mbingu zilivyofunguka kwake. Muda ulipofika aliondoka Tanzania na safari yake ilifika mpaka nchini Ufaransa.
Miguu ile ambayo ilikanyaga katika kiwanja cha Uhuru (enzi hizo uwanja wa Taifa), ndiyo ikawa miguu ambayo ilikanyaga katika viwanja bora vya ligi kuu ya Ufaransa(ligue 1). Hakuridhika sana na kelele za mashabiki wa Yanga ambao walimshangilia kipindi alipofanya vizuri. Yeye alitamani masikio yake siku moja yasikie kelele za wazungu wakiimba jina lake.
Hiki ndicho kilichomtofautisha yeye na wachezaji wengi ambao waliwahi kupita Tanzania. Na hiki ndicho ambacho Chama anatakiwa kutembea nacho. Muda huu makelele yanaelekezwa kwake. Kila mtu anatamani kulitamka jina lake kwa kujivunia kuwa jicho lake limeshuhudia burudani nzuri kutoka kwake.
Hapana shaka ana kipaji kikubwa cha kucheza mpira, na kikubwa zaidi anauwezo mkubwa wa kusoma mchezo na kufanya maamuzi ya mwisho ambayo huwa na tija kubwa kwa timu. Hii ndiyo sifa kubwa ya mchezaji bora katika mpira wa sasa. Hastahili tena kuishi Tanzania. Hastahili kuwa mkazi wa hapa, anatakiwa awe mtalii kama alivyokuwa Shaban Nonda.
Aliitumie Tanzania kama daraja, aiitumie Tanzania kama ambavyo Shaban Nonda alivyoitumia ili afike sehemu sahihi ambayo anastahili kuwepo.
Sifa ambazo anazisikia kwa sasa azitumie kama nguvu ya yeye kuongeza mbio za kufikia sehemu ambayo ni kubwa. Kitu ambacho wachezaji wengi huwa wanakosea ni pale ambapo wanaposifiwa sana na hizo sifa huchangia kwao kudumaa.
Ni dhambi kubwa kudumazwa na sifa za mashabiki, ila ni vyema sifa zitumike kumuonesha kuwa hapo alipo hastahili kwenda. Yale makelele anayoyasikia jukwaani ni makelele ya kumfukuza hapa. Mmoja wa watu ambao wanamfukuza Chama ni Mimi. Binafsi naumia na sipendi kuona miguu ya Chama ilikanyaga nyasi za viwanja vya Tanzania