Leo Simba wanakabidhiwa kombe lao kwenye mechi ya ligi kuu dhidi ya Namungo FC kwenye uwanja wa nyumbani wa Namungo FC. Uwanja ambao unaonekana ni uwanja ngumu sana kwenye ligi kuu msimu huu. Kutokana na sababu ya ugumu wa uwanja huu nimekuletea sababu tatu (3) ambazo zinaweza zikaifanya Simba kupoteza mbele ya Namungo FC.
1: MECHI YA KISASI na KUWEKA HESHIMA
Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Simba ilifanikiwa kuwafunga Namungo FC goli 3-2. Namungo FC wanaingia kwenye mechi hii wakiwa na kisasi dhidi ya mechi iliyopita waliyopoteza kwenye uwanja wa Taifa. Kisasi hiki kitatengeneza ugumu wa mechi kwa Simba.
Namungo FC wapo katika uwanja wao wa nyumbani , uwanja ambao utatumika kwa Simba kukabidhiwa kombe lao. Kwa namna yoyote ile Namungo FC hawatakuwa na nafasi ya kuwakubalia Simba kupata ushindi ili sherehe yao ya kukabidhiwa ubingwa iwe nzuri. Namungo FC watapigana kuweka heshima kwa kuepuka kufungwa mbele ya uwanja wao wa nyumbani.
2: SAFU YA USHAMBULIAJI
Moja ya timu ambayo ina wachezaji wa eneo la mbele ambao wanauwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi nyingi za magoli pamoja na uwezo mkubwa wa kufunga ni Namungo FC. Reliants Lusajo ana magoli 12 mpaka sasa hivi , Birigimina Blaise ana magoli 7 mpaka sasa hivi.
Ukiachana na eneo hili kuna wachezaji ambao wanatengeneza nafasi nyingi za magoli kama Lucas Kikoti, John Mbisse pamoja na Hashim Manyanya. Pia Namungo FC kwenye mechi ngumu hata walinzi huhusika kwenye ufungaji , mfano kwenye mechi dhidi ya Yanga , beki Manyama alifunga magoli 2 katika sare ya 2-2, kwa hiyo Namungo FC haitegemei mchezaji mmoja kwenye kufunga , timu inahusika kwenye ufungaji hapa ndipo ugumu wa Simba kushinda unapoanzia pia.
3: UNBEATEN RUN
Mara ya mwisho kwa Namungo FC kufungwa ilikuwa dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Taifa walipofungwa magoli 3-2 . Tangu hapo wamepitia mechi 19 bila kufungwa na leo watakuwa wanatafuta mechi ya 20 bila kufungwa . Kucheza mechi 19 mfululizo bila kufungwa inaonesha hii ni timu ambayo ina ushindani mkubwa , ushindani ambao unaweza kuisumbua Simba katika mechi ya leo.