Mengi yalisemwa baada ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) kutajwa na kocha mkuu, Emmanuel Amunike.
Kikosi ambacho kimeleta mjadala mkubwa sana, mjadala ambao mpaka sasa unazidi kuwa wa moto katika maeneo mbalimbali.
Siyo dhambi kabisa kuibuka kwa mjadala. Mpira siku zote ni mchezo wa makosa. Mpira haujawahi kukamilika kwa asilimia mia hata siku moja.
Na wanavyosema mpira ni mchezo wa makosa huwa hawaishii kumaanisha pekee kuwa makosa haya hufanyika ndani ya uwanja.
La Hasha!, makosa huanzia nje ya uwanja. Jinsi unavyoiandaa timu yako. Unaiandaa katika misingi gani bora ?, unaiandaa katika mazingira gani bora ?
Kocha anakuwa na aina gani ya wachezaji ndani ya kikosi ?. Hapana shaka wachezaji ndiyo wana nafasi kubwa katika maamuzi ya matokeo ya mpira.
Kwa hiyo makosa ndani ya mchezo wa mpira wa miguu huanzia nje ya uwanja na kuna uwezekano mkubwa sana makosa ambayo hufanywa nje ya uwanja kuchangia makosa ya ndani ya uwanja.
Hapa ndipo watu wengi wanapopata hofu kuhusiana na kikosi cha Emmanuel Amunike, na ndipo hapo mjadala unapokuja.
Mjadala unaanzia kwenye hofu ya watu kuhusiana na uteuzi uliofanyika kwa ajili ya kupata wachezaji hao ambao watacheza mechi ya kuamua kama tunaweza kupita kwenda Afcon.
Hofu inatokana na wengi kuamini kocha amefanya makosa kwenye baadhi ya teuzi zake ambazo amezifanya.
Makosa ambayo yanaweza kusababisha sisi tufanye makosa mengine ndani ya uwanja kwenye mechi dhidi ya Uganda.
Hapa ndipo mwanzo wa hofu unapoanzia na ndipo hapo mjadala umekuwa mkubwa sana. Sawa, Watanzania tuna kiu kubwa sana.
Kiu ya kufuzu Afcon. Ni miaka mingi sana hatujafuzu na mechi ya mwisho dhidi ya Uganda ndiyo ambayo itaamua kama tunaweza kata kiu yetu au tutaendelea nayo.
Yani ile tamaa ya kufuzu ipo kubwa sana ndani yetu. Lakini tunasahau kitu kimoja. Kuna kitu alichokifanya Emmanuel Amunike kiko ndani ya taaluma yake.
Yeye ndiye mwenye hiyo taaluma. Taaluma ambayo ilitufanya tumwamini kumpa kazi kwa kuamini atatuongoza kufika tunapopatamani.
Tulimwamini tukamkabidhi timu, kazi yetu ilikuwa moja tu, kuishi na imani ndani ya taaluma yake. Tuiamini taaluma yake.
Tuiunge mkono taaluma yake, hicho tu ndicho ambacho tunatakiwa kukifanya. Tuamini kitu ambacho amekifanya ni kwa sababu anaona ni sahihi na kinaweza kutufikisha mbali.
Kuna kitu kimoja ambacho wengi hatujui. Kocha hukaa muda mrefu kutafakari jinsi gani ambavyo anaweza kukabiliana na adui wake.
Atatumia muda mwingi kumtazama adui yake, atatazama ubora wa adui yake, udhaifu wa adui yake atakayepambana naye.
Baada ya hapo ndipo atakapoamua kuchagua aina gani ya mfumo ambao unaweza kumpa ushindi dhidi ya adui yake.
Na mfumo huu unaweza lazima ukamilike kwa kuwa na wachezaji. Na siyo kila mchezaji anaweza kuingia moja kwa moja kwenye mfumo ambao kocha ameuchagua.
Kwa hiyo Emmanuel Amunike mpaka sasa hivi yeye ndiye anayejua ni aina gani ya mfumo ambao utakuwa na msaada mkubwa kwetu sisi, ndiyo maana ameamua kuchagua aina ya wachezaji ambao wanaweza kuingia kwenye mfumo wake.
Unaweza ukaona kuwa mchezaji fulani anafaa kuingia kwenye kikosi cha timu ya Taifa na ukawa na sababu za msingi kabisa, lakini akawa hafai kuingia kwenye mfumo wa kocha.
Kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ni jambo moja, kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa kocha ni jambo jingine.
Nina imani kabisa Emmanuel Amunike amechagua wachezaji sahihi watakaoingia kwenye mfumo wake ambao ameupanga kwa ajili ya Uganda!.
Tubaki na kitu kimoja tu ambacho ni cha msingi, tuheshimu maamuzi yake aliyoamua kuyachagua.
Yeye ndiye aliyekaa muda mrefu, akatafakari jinsi gani ya kushinda hii mechi, ubora upi ambao Uganda walionao kwa sasa.
Ni madhaifu yapi Uganda wako nayo kwa sasa. Mwisho wa siku akaja na aina gani ya wachezaji ambao watakuwa sahihi kabisa kutumika kwenye mfumo na mbinu zake katika mechi ya Uganda.