Sambaza....

Miaka ishirini na nane (28) iliyopita mishipa ya pua yangu ilipewa ruhusa na mwenyezi Mungu kuvuta hewa ya mji wa Bujumbura katika nchi ya Burundi.

Nchi ambayo ilikuwa na hali ya amani hafifu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sikuweza kujua ni eneo lipi sahihi ambalo litanifaa kusimama nikiwa mkubwa, sikuwa najitambua zaidi ya kulia kama ishara ya kuingia katika uwanja wa mapambano unaoitwa dunia.

Hapana shaka wazazi wangu walikuwa na furaha kuniona mbele ya macho yao na swali kubwa lililokuwa limebaki kichwani mwao ni moja tu nalo ni “mtoto wetu atakuja kuwa nani hapo baadaye?”.

Swali lilikuwa gumu sana kwao kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kuiona kesho yangu yenye majibu yote zaidi ya hapo walibaki kuwa na matamanio moyoni mwao tu. Sijui walikuwa wanatamani niwe nani?, sijui daktari?, mwalimu?, au nahodha wa meli nitumie muda mrefu nikiwa safarini majini nikisafiri nchi za ng’ambo?.

Hapana shaka walikuwa wananiombea mema sana na sidhani kama walitamani niwe mmoja wa vijana ambao watashika silaha kwa ajili ya kupigana kwenye vita vya nchini kwetu.

Matamanio yao yalijaa nguvu kubwa ya kheri ndani yangu kwani nilifanikiwa kuangukia sehemu ambayo inafuatiliwa na watu wengi dunia na sidhani kama wazazi wangu waliwahi kuwaza nitakuwa mchezaji wa mpira wa miguu katika maisha yangu.

Ardhi ya Bujumbura iliijenga miguu yangu na kunifanya niwekeze katika biashara ya miguu yangu, biashara ambayo ilinipa umaarufu. Umaarufu ambao ulinifanya niwe na uwezo wa kufika sehemu ambazo vijana wengi wanatamani kufika.

Sikuweza kubeza kazi ya miguu yangu, nyasi zilikuwa zinafurahia kila viatu vya miguu yangu vilipoƙuwa vinakanyaga na kuna wakati hata mpira ulikuwa unatamani uwe mguu wangu ili niusaidie kufika katika safari yake ya mwisho.

Nyavu zilikuwa zinashangilia kila mara na kuna wakati zilikuwa zinajiandaa kucheka kila zikiniona nikiwa uwanjani hali ambayo ilinifanya niwe adui mkubwa wa magolikipa wengi ndiyo maana nilifanikiwa kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Burundi kabla sijafika Tanzania.

Nilitamani sana kufika Tanzania, tena katika jiji la Dar es Salaam, jiji ambalo lilikuwa na sehemu ambayo ilikuwa na watu wengi sana, sehemu ambayo inabiashara nyingi sana na ndiyo sehemu ambayo ina wazazi wa mpira huu hapa Tanzania, yani Kariakoo.

Wachezaji wengi wanatamani na wana ndoto ya kuchezea kwenye timu za Kariakoo kwa sababu ya maslahi na ndiyo sehemu ambayo ukiwepo kuna asilimia kubwa ya kuonekana na watu wengi, kwa kifupi kariakoo kuna timu mbili ambazo zinafuatiliwa kwa karibu zaidi na watu wengi zaidi kuliko timu yoyote Tanzania.

Hata ujio wangu ulipambwa kwenye kurasa za mbele za magazeti Tanzania kuwa “Striker katili atua msimbazi”, “kiboko wa magolikipa asajiliwa Simba” na wengine walifikia kuwatisha Yanga kwa kuandika kichwa cha habari kinachosema “Kwa muuaji huyu, Yanga msilete timu uwanjani”.

Walikuwa sahihi kabisa kuandika hivo kwa sababu nilipokuwa awali nilikuwa mfungaji bora tena kwa magoli mengi tu. Magoli ambayo wengi walitamani kuyaona kwenye timu ya Simba.

Nilifanya kitu ambacho kilikuwa kinyume na mategemeo yao, sikuweza kufanya magoli mengi kama nilivyofanya sehemu ambayo nilitoka.

Maisha ya Kariakoo yana changamoto kubwa sana na yana presha kubwa sana ambayo inaweza kukufanya ufanye kitu ambacho kipo nyuma ya mategemeo yako na mategemeo ya watu wengi.

Leo hii Adam Salamba, Marcel Kaheza na Mohammed Hussein wamesajiliwa kwa matumaini makubwa kwa sababu ya kiwango kikubwa walichokionesha msimu ujao, kusajiliwa kunaweza kuwa na furaha kwao na kuwa na jambo chanya kwao lakini kazi kubwa inakuja kufanya kitu ambacho walikifanya katika timu ambazo walipitia.

Ndiyo maana nimeamua kuandika waraka huu ili kuwakumbusha kuwa wamefika katika mji wa Kariakoo, mji ambao huwezi kuona nyasi kama miji waliyotoka.

Sambaza....