Unaweza kubofya mechi ambayo ungependa ifuatilia hapo.
Pazia La Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Kwa Msimu Wa Mwaka 2018/2019 Linatarajiwa Kufunguliwa rasmi Jumatano hii ambapo jumla ya viwanja sita vya miji ya Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Tanga, Singida na Bukoba vitawaka moto.
Mabingwa watetezi Simba Sports Club watakuwa nyumbani katika uwanja wa Uhuru ‘Shamba la Bibi’ jijini Dar es Salaam kuumana na Wajelajela Tanzania Prisons katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkali.
Katika mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu hizo uliisha kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao ambayo yalifungwa na Nahodha John Raphael Bocco na Mganda Emmanuel Anold Okwi.
Wafunga buti, timu ya soka ya Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani wao watakuwa katika uwanja wa Mabatini uliopo katika mji mdogo wa Mlandizi kucheza na Wanakuchele Ndanda FC.
Ndanda wamekuwa mdembwedo pindi wanapocheza na Ruvu Shooting kwani katika michezo Minne iliyopita wamefanikiwa kuibuka na ushindi mara moja pekee na kutoka sare mara moja hivyo watahitaji ushindi ili kuweza kujijengea heshima mbele ya Ruvu Shooting.
Wagosi wa Kaya Coastal Union, ambao waliwahi kuwa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1988 watakuwa katika uwanja wenye historia ndefu wa CCM Mkwakwani kucheza na Wanapaluhengo Lipuli FC.
Coastal Union watacheza mchezo huo ukiwa ni wa kwanza toka waliposhuka daraja katika msimu wa mwaka 2015/2016 na watakutana na Lipuli FC ambao huu ni msimu wao wa pili katika ligi Kuu toka wapande daraja.
Wachimba Almas Mwadui FC wao wamesafiri hadi mkoani Kagera kucheza na wenyeji Wanankurukumbi Kagera Sugar katika dimba la CCM Kaitaba lililopo mjini Bukoba, wakati huo huo Biashara United wao watakuwa mkoani Singida Kucheza na Singida United katika uwanja wa Namfua.
Jijini Mwanza kwenye dimba la CCM Kirumba Alliance School watakuwa na kibarua kizito watakapocheza na Wabishi Mbao FC.
Raundi ya kwanza, mzunguko wa pili itakamilika Alhamis ya Agosti 23 ambapo michezo minne itapigwa katika miji miwili ya Shinyanga na Dar es Salaam.
Jijini Dar es Salaam kutapigwa michezo mitatu ambapo Mabingwa wa Kihistoria Dar Young Africans watacheza na Mabingwa mara mbili wa taji la ligi kuu Bara, Wanatamtam Mtibwa Sugar katika uwanja wa Uhuru.
Mchezo mwingine siku hiyo ni ule kati ya Maafande JKT Tanzania dhidi ya Kinondoni Municipal Council (KMC) utakaofanyika kwenye uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mabingwa mara moja wa taji la Ligi kuu Tanzania Bara Azam FC nao watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kucheza na wanakomakumwanya Mbeya City.
Mchezo wa mwisho ni ule wa Wapiga Debe Stand United ambao watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani CCM Kambarage kucheza na African Lyon ya Dar es Salaam