Sambaza....

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Alliance ya jijini Mwanza, Kessy Mziray ameutaja muda wa saa nane mchana ambao mchezo wao wa ligi dhidi ya Mbeya City utachezwa kama sehemu muhimu ya kuweza kupata alama tatu.

Mziray amesema anaamini muda huo utakuwa mgumu sana kwa Mbeya City ambao wametoka kwenye sehemu yenye hali ya hewa ya baridi, wakati wao wamekuwa wakifanya mazoezi katika muda huo wa jua kali.

“Muda huu unaweza ukawa na faida kwetu, kwa sababu ya hali ya hewa ya jiji la Mwanza ukilinganisha na jiji la Mbeya, lakini kwetu sisi ni kawaida kwani huu utakuwa ni mchezo wa nne ama watano kucheza mchana, kwa hiyo sisi haitatuathiri na hasa ukizingatia muda wetu mwingi wa mazoezi tunafanya mchana, ninaimani muda huu utakuwa na faida kubwa kwetu,” amesema.

Alliance wanashuka dimbani jumapili hii kucheza na Mbeya City kwenye uwanja wa Nyamagana wakitoka kupata alama moja dhidi ya Tanzania Prisons baada ya sare ya bao 1-1, na Mziray anasema maandalizi yamekamilika lakini watamkosa mshambuliaji raia wa Burundi Bigirimana Blaise.

“Bigirimana ni kweli bado anaumwa, aliumia katika mechi yetu dhidi ya Prisons, na mbadala wake yupo kwa sababu tunakikosi kibana na ataziba vizuri pengo lake, ila niwaombe wadau na wapenzi wa Alliance wafike kwa wingi kutupa support,” amesema.

Alliance wanashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi kuu wenye timu 20 wakiwa na alama 25 wakati Mbeya City wao wakikalia nafasi ya nane baada ya kujikusanyia alama 26.

Sambaza....