Sambaza....

Ukimuuliza Kylian Mbappe wa PSG, nani kiigizo chake kikubwa katika Soka, atakutajia jina la mshindi mara tano wa Ballon d’or, Mreno Christiano Ronaldo.

Kila mtu ana kiigizo chake, kinachomfanya ajitume japo kufikia mafanikio kama yake au kupita njia alizopita kiigizo chake ili naye afanikiwe. Hii ni kutokana na asili ya mwanadamu kutaka mafanikio kwa kila alitendalo.

Clatus Chama, Mwamba wa Lusaka, kiungo fundi kutoka nchini Zambia. Alitua katika mitaa ya Msimbazi mwezi juni mwaka jana, akipewa kandarasi ya miaka miwili kuwatumikia  mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Tanzania bara.

Na uzito wake wa kilo 65 na urefu wa mita 1,77m ilimchukua takribani mechi tatu hadi nne, kuwaaminisha mashabiki kuwa yeye ni “mwamba wa Lusaka”. Mguu wake wa kulia uliibua hisia za mashabiki zilizojaa msisimko na mapenzi ya dhati ndani ya mioyo yao, kiasi cha kulitamka jina lake bila kukereka nafsi.

Clatus Chama.

Huyo ndio Chama, utampenda akiwa anaupokea mpira na kuanza kuukokota, pasi zake za mwisho “mpenyezo” zenye ulinganifu yakinifu, zenye macho ya hadubini na uelekeo sahihi kwa John Boko, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Hana haraka akiwa na mpira mguuni, kwa kuwa anajua jinsi ya kuulinda, kasi yake si kubwa akiwa na mpira lakini huakikisha mpira huo unafika eneo analolita yeye ufike. Si hivyo tu, Chama pia ni fundi wa kucheka na nyavu.

Hadi Simba inafuzu hatua ya makundi, yeye ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa klabu, kwa kuwa na goli nne, zote akizifunga katika mechi muhimu. Alifunga katika mechi ya kwanza dhidi ya Mbabane Swallows, nyumbani goli moja na ugenini 2, kisha akaifunga Nkana Red Devils ya huko kwao Zambia, goli moja nyumbani, goli lililoivusha Simba hatua ya makundi.

Katika mechi za awali za makundi, Chama amekuwa akiaminiwa na kocha Patrick Aussems na kuanzishwa katika kikosi cha kwanza. Ukitaja timu zenye viungo wazuri katika TPL hutosita kuitaja Simba. Simba ina Mzamiru Yasin, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Mohammed Ibrahim, Rasid Juma James Kotei, Haruna Niyonzima, lakini wengine watakaa benchi lakini Chama ni lazima aanze.

Kiwango chake kimeanza kuonekana kuwa cha kawaida kwa baadhi ya mechi. Nakiri kuwa, katika soka , mchezaji hawezi kuwa na kiwango bora katika kila mechi, bali hupitia vipindi vigumu pia. Vivyo hivyo, Chama nae anajikuta katika kipindi hiki hasa katika mechi za makundi.

Kwanini Chama anaonekana kuwa wa kawaida katika mechi za makundi? Kwa sababu kuna vitu vingi kiufundi anakosa na hivi vinamfanya asiwe na msaada kwa timu katika mechi zenye ushindani mkubwa.

Simba katika  kundi D, tayari imeshakwaana na  vigogo Al Ahly, JS Saoura na AS Club Vita ya Congo. Mechi ya kwanza, Taifa dhidi ya Saoura, Simba ilishinda 3-0, Mechi ya pili dhidi ya AS Club Vita Ugenini ikapigwa 5-0, na mechi ya tatu dhidi ya Al Ahly ugenini imepigwa tena 5-0, kisha ikaja kupata ushindi wa goli 1-0 nyumbani dhidi ya Al Ahly.

Katika mechi hizo zote, Simba alizopoteza, Chama hakuwa na msaada mkubwa kwa timu, tena muda mwingine alikuwa ndio chanzo cha goli, mfano dhidi ya AS Club Vita.

Katika mchezo dhidi ya Al Ahly, Simba walizidiwa katika kila idara, yaani mashuti 11 kwa 9 ya Simba, yaliyolenga lango 6 kwa 2, umiliki wa mpira 71% kwa 29% za Simba, pasi 749 kwa 300, usahihi wa pasi 88% kwa 74% za Simba, faulo 10 kwa 16 walizofanya Simba, kadi za njano 0 kwa 1 ya Simba.

Kiwango chake huonekana kibaya zaidi akicheza na timu kubwa, na yenye presha kubwa “high pressing” hii humfanya acheze kama Jonas Mkude, yaani chini ya eneo lake analopaswa kucheza kama kiungo mshambuliaji.

Mechi dhidi ya Nkana Red Devils ugenini, timu ilizidiwa eneo la kati, Chama akishuka zaidi kwa lengo la kujilinda. Kushuka kwake kunaifanya Simba kuwa na viungo wa Chini watatu katika eneo moja, yaani Mkude, Kotei na Chama.

Jonas Mkude.

Mrundikano huu, hukaribisha mashambulizi, huwafanya mabeki wa timu pinzani kuchezea juu ya eneo lao la hatari, matokeo yake ni kuwaleta maadui karibu na lango la Simba. Hiki huchangia kwa kiasi kikubwa timu kufungwa goli nyingi.

Acha nikurudishe kwenye mechi ya Simba dhidi ya Al Ahly, ambayo Simba waliibuka na ushindi wa goli 1-0. Chama alicheza, lakini hakuwa na kazi kubwa sana kiasi cha kuwa muhimili wa timu, badala yake Simba ilicheza mipira mirefu, yaani inayoruka eneo la kati kwenda kwa Emmanuel Okwi upande la kulia.

Aina ya mipira ya Simba ilisaidia Chama kucheza kwa muda mrefu bila kuonesha udhaifu mkubwa japo alitolewa kipindi cha pili lakini kidogo alionyeha uhai.

Dhidi ya Yanga, Chama alicheza kwa dakika 45 pekee, nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Dilunga. Chama alionekana kuzidiwa eneo la kati, kasi ndogo yake ndogo wakati wa ushambuliaji unaifanya timu  nzima kubaki nyuma. Aussems alibaini hili kuwa Simba inamiliki mpira  haina uhatari katika mashambulizi yake.

Hassan Dilunga na Haruna Niyonzima.

Hadi kipindi cha kwanza kinakamilika Simba ilikuwa imepiga mashuti manne pekee na yote hayajalenga lango (off target), licha ya kuwa na umiliki wa asilimia  55 kwa 45 za Yanga.

Ujio wa Dilunga eneo la kati ulileta hamasa kubwa, na faida timu inapomiliki mpira. Dilunga aliingia akiwa na kasi kubwa, kuipandisha timu na kushambulia kwa kasi, hii iliwapa fursa eneo la chini yaani Mkude na Kotei kupanda zaidi juu na kuliandama lango la Yanga na ndio sababu ya goli la dakika ya 71 la Meddie Kagere.

Chama anatakiwa afanye nini?.

Chama lazima abadilike hasa aina ya uchezaji wake. Kwanza lazima awe mwepesi kuongeza kasi anapokuwa na mpira, kasi ya kwenda mbele.kuna wakati anatakiwa kuwa Rashid Juma, yaani akiwa na mpira cha kwanza ni kwenda mbele kwa kasi, kuwalazinisha mabeki kufanya makosa na kuongeza presha.

Pili, kuna wakati Chama anatakiwa awe Saidi Ndemla, awe na uwezo wa kuachia fataki nje ya 18, na akafunga. Simba inaweza kukutana na timu yenye uwezo mkubwa wa kujifunga kuanzia nyuma, yaani beki jiwe, lazima timu ishikwe pabaya, kwa sababu inawapigaji wawili tu yaani Mkude naye kidogo sana na Okwi.

Chama angekuwa mpiga mashuti nje ya 18 basi angekuwa na goli nyingi, kwa hili mwalimu wake lazima awe Said Ndemla atake asitake.

Said Hamis Juma Ndemla.

Kitaalamu, unaambiwa Chama anakosa “Game Intelligence” yaani uwezo wa mchezaji kufanya maamuzi sahihi ndani ya uwanja, tena kwa haraka. Lazima sehemu ya kushuti, afanye hivyo, kuna sehemu timu inatakiwa kuongeza kasi ni lazima  afanye hivyo, lazima ajue jinsi ya kuusoma mchezo na mahitaji yake. Ajue asaivi timu imezidiwa mimi natakiwa kufanya nini, au nichezee eneo lipi lenye tija kwa timu.

Haya yote sio lazima ayasikie kutoka kwa Aussems ni lazima aujue mchezo kama mchezaji. Na hapa ndio utapata maana halisi ya maneno ya Meddie Kagere kuwa “Game Intelligence is better than age” na ndio maana kila siku Emmanuel okwi anaonekana kuwa mtu muhimu kwenye klabu kwa sababu ya hiki.

Sambaza....