Klabu ya Wananchi Yanga leo imeingia makubaliano na Benki inayosikiliza, Benki ya CRDB katika kutengeneza kadi za Wanachama wa Yanga kupitia kadi ya CRDB Tembo Card.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika hafla ya utiaji saini na Yanga afisa biashara wa benki wa CRDB Boma Raballa alisema “Tuna furaha kubwa kuingia makubaliano na klabu ya Yanga leo ambayo yatawawezesha mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania Bara kujisajili na kulipia michango yao ya uanachama kupitia mtandao wetu matawi zaidi ya 230 nchi nzima,” alisema na kuongeza
“Kupitia kadi maalum ya TemboCard Young Africans, mwanachama wa Yanga ataweza kufanya miamala kwenye ATM, malipo ya mtandaoni na mashine za POS.”
“Kadi hii pia inamuwezesha mwanachama wa Yanga kupata bima ya maisha ambayo itampa mkono wa pole pindi atakapofiwa na mke/mume, kufariki au kupata ulemavu wa kudumu,” alimalizia Raballa.
Nae rais wa klabu ya Yanga Hersi Said wakati wa hafla hiyo amekiri CRDB ni benki kubwa na ni furaha kufanya kazi na benki inayokua na inayojitanua zaidi.
“Tunayofuraha leo kuwa na ushirikiano na benki kubwa nchini benki inayokua kwa kasi zaidi nchini lakini pia inayoendelea kujitanua zaidi nje ya nchi,” alisema Hersi
Benki ya CRDB ikiwa ni benki inayomsikiliza mteja zaidi nchini ikiwa na mshine za ATM zaidi ya 500 nchini, matawi zaidi ya 230 yaliyosambaa mikoa yote nchi nzima.
Benki hiyo ambayo imekita mizizi nchini lakini pia ikiendelea kujitanua na nchi jirani kama Burundi ina mawakala zaidi ya 30,000 na sehemu zaidi ya 5,000 za kufanya malipo nchini. Pia Uwezo wa kusimamia na kubadili kadi au kuomba kadi ya TemboCard iwapo itakuwa imepotea au kuharibika kupitia SimBanking.
Kwa huduma zote hizo zinawapa nafasi mamilioni ya mashabiki wa Yanga “Wananchi” kupata huduma bila mkwamo nchi nzima wakiwa na kadi zao za CRDB Tembo Card za Young Africans Sc.