Katika usajili wa dirisha dogo wa msimu huu wa 2022-2023 vilabu vyote vya Ligi Kuu ya NBC viliingia sokoni na kufanya usajili ili kuongeza katika nguvu katika timu zao, ni Kagera Sugar pekee ya Mecky Mexime ndio haikusajili hata mchezaji mmoja.
Yanga iliingia sokoni ikasajili wachezaji wanne, wawili wakiwa wageni na wawili ni wazawa. Yanga ilimsajili Mamadou Doumbia kutoka Mali, Charlie Musonda kutoka Zambia halafu ikawasajili wazawa Metacha Mnata (mkopo kutoka Singida Big Stars) na Mudathir Yahya (mchezaji huru).
Kati ya sajili zote nne ni Mudathiri na Musonda ndio tayari wameonyesha kuanza kurudisha hela kwa Yanga kutokana na jinsi walivyoongeza kitu katika klabu, zaidi ni Mudathir anaecheza eneo la kiungo wa kati.
Mudathir aliemaliza Ligi ya msimu uliopita na Azam Fc kabla ya kuachana nao na kukosa timu msimu ulipoanza ameonekana kuingia na mguu mzuri Yanga huku Profesa Nabi akimuamini na kumpa majukumu ndani ya kikosi.
Kiungo huyo wa Timu ya Taifa ya Zanzibar “Zanzibar Heroes” ameonekana kuwa bado yupo fiti licha yakukaa nusu msimu akiwa hana timu. Na inasemekana alikua kwao Zanzibar akifanya mazoezi na KMKM.
Licha ya utitiri wa wachezaji katika eneo la kiungo la Yanga lakini Mudathir ameweza kupambana na kupata nafasi ya mara kwa mara tena katika michezo yote ya mashindano yote wanayoshiriki Yanga. Kombe la FA, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika.
Si tu anaisaidia Yanga katika kiungo haswa cha ukabaji lakini pia tayari Mzanzibar huyo ameandikisha jina lake katika ukurasa wa ufungaji baada ya kufunga bao zuri dhidi ya TP Mazembe katika ushindi wa Yanga wa mabao matatu kwa moja.
Wakati Yanga wakisubiri Doumbia aingie kwenye mfumo na Metacha asubirie kumsaidia Diara tayari yeye amewapiku wenzake aliosajiliwa nao dirisha dogo na kuonyesha mchango mkubwa katika timu.