Sambaza....

Taratibu jua la mashariki linaanza kutoka ubavuni mwa mawingu , hii ni kama taa ya kijani inayoruhusu maisha kutembea. Maisha ambayo yamebebwa kwa ukubwa na wanadamu.

Huwezi kutenganisha maisha na wanadamu , wanadamu huyatazama maisha na maisha huwaangalia wanadamu kitu pekee ambacho huwa kinakuja kututofautosha ni namna ambavyo tunayatazama maisha.

Wengine huyatazama maisha katika jicho la kawaida na kuna wengine hutazama maisha katika jicho lisilo la kawaida. Jicho la njaa , jicho ambalo lina hasira kubwa ndani yake.

Jicho ambalo huwafanya wakimbie kwa nguvu , kasi na kwenye uelekeo ambao uko sahihi kufikia katika kilele cha mlima mafanikio. Wengi huwa hawatamani sana kuendelea kuwepo chini ya mlima mafanikio.

Mioyo yao hutamani nyao zao ziwe juu ya mlima mafanikio. Ndipo hapo matumizi ya vipaji vyao huchukua nafasi ili kufikia kwenye kilele hicho cha mafanikio. Hutumia vipaji vyao kama tiketi ya kuwafikisha wanapopatamani.

Tanzania imewahi kubahatika kuwa na mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana ndani ya muongo mmoja uliopita, Mrisho Khalfan Ngassa. Mwili wake ulikuwa umevishwa kipaji kikubwa sana.

Pamoja na kwamba alikuwa na kipaji kikubwa pia bahati ilikuwa ndani yake . Katika umri mdogo alifanikiwa kwenda kufanya majaribio kwenye ligi kuu ya England kwenye klabu ya Westham United.

Pamoja na kwamba hakufanikiwa lakini haya yalikuwa mafanikio makubwa sana, mafanikio ambayo yalitakiwa kuwa mwanzo wake wa kuendelea kutafuta malisho bora , malisho ambayo yangetumika kama alama ya mpira watu.

Sawa alifanikiwa kucheza Marekani , sawa alifanikiwa kukabwa na beki wa Manchester United Ferdinand lakini hakufanikiwa kuweka rekodi ambazo zingekuwa mlima mkubwa kwa wanaomfuata.

Leo hii Mbwana Samatta alitakiwa kuwa mtu ambaye anapigana kuvunja rekodi za Mrisho Ngassa na siyo mtu anayeweka rekodi zake mwenyewe. Alitakiwa kupigania kuvunja rekodi ya Mrisho Ngassa kucheza EPL.

Leo hii miguu yake ingekuwa inawashwa sana kucheza ligi kuu ya England kwa sababu ya kuvunja rekodi za Mrisho Ngassa. Leo hii Mrisho Ngassa alitakiwa awe angalau mmoja wa wachezaji ambao waliwahi kufika tatu bora ya wachezaji wanaowania tunzo ya mchezaji bora Afrika.

Leo hii Mrisho Ngassa alitakiwa kuwa mchezaji ambaye alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa England angalau hata kuwa mchezaji ambaye alifanikiwa kufunga magoli 100 kwenye ligi kuu ya England.

Leo hii Mrisho Ngassa alitakiwa awepo China akivuna mafao yake kwenye klabu kubwa nchini China huku nyumbani kwao Mwanza akiwa anajenga kituo kikubwa cha kuibua, kukuza na kulea vipaji.

Pale kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julisu Kambarage Nyerere palitakiwa wagonjwa mbalimbali wakiwa wanapishana kwenda kutibiwa nje magonjwa sugu chini ya Ngassa Foundation.

Foundation ambayo ingekuwa inasaidia serikali kwa kujenga kituo kikubwa cha kutibu magonjwa sugu hapa nchini. Haya ndiyo mafanikio ambayo yangekuwa yanamnyima usingizi Mbwana Samatta.

Tofauti na sasa hivi kila Mbwana Samatta akigeuka kumtazama Mrisho Ngassa anachokutana nacho ni Mrisho Ngassa kugombana na viongozi wa Yanga akidai Milioni 15 , pesa ambazo alitakiwa awe anazitoa kwa ajili ya ticket na malazi ya mgonjwa tu kwenda India kumtibu mama wa mmoja wa Mwanza chini ya Ngassa Foundation.

Sambaza....