Nimesoma mahala Benard Morrison amepewa mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya FAR Rabat inayomilikiwa na Jeshi pale Morocco.
Nimeona ni mkataba wenye masharti magumu. Ameambiwa asifanye matukio ya utovu wa nidhamu kwa miezi 12 ya mkataba wake.
Mkataba huo umeenda mbali, ukimtaka awe anaishi kwenye kambi za jeshi. Hapa sasa! Kiufupi tu, Morrison anapaswa kuwa mtiifu katika kipindi chote cha mkataba wake.
Endapo atakiuka masharti atavunjiwa mkataba. Nimebaki kushangaa na kalamu yangu mkononi. Lakini sidhani kama Morrison mwenyewe anajali kuvunjiwa mkataba.
Super Ben ni kama msichana mrembo anayekatisha katikati ya kundi la wanaume. Kila mwanaume atageuza shingo yake kumtazama na atatamani kuwa nae.
Sehemu zote ambazo Super Ben ameshindwana na timu sio ubora wake. Ni tabia zake. Super Ben yuko vile na ngumu kumbadili.
Mara nyingi timu huwa zinambadilisha yeye, yeye hajawahi kubadilika. Sijui nini kitatokea pale Rabat kwa Wanajeshi.
Huenda tukamuona Super Ben wa tofauti, lakini kuna sehemu ya moyo wangu inanikataa. Ngoja tuone atakuwa Super Ben wa namna ipi.
Kipaji kikubwa mguuni, uwezo mkubwa wa kuamua mechi na kumuhadaa mpinzani, lakini hujui ndani ya dakika mbele atafanya nini. Huyu ndiyo Super Ben. Yuko kama alivyo, hajali.
Super Ben anaingia katika kundi la Mghana mwenzake Super mwingine. Ni Super Mario Balloteli. Kipaji kikubwa mguuni, kichwani anajielewa mwenyewe.
Kinachotokea wachezaji wa namna hii hawawezi kukosa timu ya kuchezea. Ni kama mwanamke mrembo mwenye tabia mbaya hawezi kukosa mahusiano, licha ya tabia zake mbaya alizonazo.
Kila timu inayomsajili mchezaji wa namna hii inajipa matumaini atabadilika mbeleni, baadae wanakuja kushindwana na kila mmoja anashika njia yake.
Haishangazi unapoona ndani ya misimu mitatu Super Ben na Super Mario wamebadili timu kama wamebadili nguo zao za ndani.