Sambaza....

MTANZANIA, Mbwana Ally Samatta jana ilikuwa ndio siku ya kipekee kwake baada ya kuandika rekodi mpya na kumfanya kuwa ndio Mtanzania wa kwanza kufunga goli katika michuano mikubwa duniani ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Usiku wa Uefa umerudi tena, na kwa Tanzania, Samatta naye amerudi vyema baada ya jana kufunga goli la pili katika kipindi cha pili dakika ya 52 akiunganisha krosi safi kutoka kwa Theo Bongonda na kuifanya Genk kuwa nyuma klwa goli 5-2 dhidi ya RB Salzburg kabla ya Waaustria hao kuweka kamba nyingine dakika ya 66 kupitia kwa Andres Ulmer na kuwafanya Genk kulala ugenini kwa goli 6-2.

Kwa upande wake Samatta, ameonekana kuwa na furaha japo wamefungwa lakini furaha yake kubwa ni goli alilolifunga kwa kichwa cha kuogelea (diving header).

“nina furaha kubwa kufunga goli, lakini pia haina maana kwa kuwa tushapoteza mchezo… ulikuwa ni mchezo mgumu kwetu, goli lao la mapema lilituvuruga kiasi cha kushindwa kufanya lolote..”

Samatta pia amekiri kuwa Ugeni katika mashindano hayo ndio sababu ya kufungwa lakini hata hivyo wana nafasi nyingi kwani wanaweza fanya vizuri katika michezo yao iliyosalia katika kundi

” Hii ni mechi moja tu, tuna zingine tatu, tena katika uwanja wetu wa nyumbani tukiwa na mashabiki wetu” aliongezea Mshambuliaji huyo.

Genk imetupwa katika kundi E ambalo lina vigogo kama Liverpool, Napoli na RB Salzburg. Kundi hili lilicheza michezo yake siku ya Jana Jumanne, Napoli wakiibuka na Ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Liverpool nyumbani, kisha RB Salzburg ikaichapa Genk.

RB Salzburg wanaongoza kundi hilo wakiwa na alama 3 na tofauti ya magoli manne, Napoli katika nafasi ya pili ikiwa na alama 3, Liverpool ya tatu na Genk inaburuza mkia.

Samatta anatarajiwa kujitupa uwanjani tena Octoba 2 mwaka huu kuwavaa Napoli ya Italy katika uwanja wao wa nyumbani katika michuano hiyo ya Uefa.

Sambaza....