Ligi Kuu ya wanawake ya Serengeti ipo mapumzikoni baada ya michezo ya raundi ya kwanza kumalizika huku Simba wakiwa kileleni baada ya michezo tisa ya raundi hiyo ya awali kumalizika.
Simba Queens ipo kileleni ikiwa na alama 22 ikifwatiwa kwa karibu na JKT Princess Tanzania wanaoshika nafasi ya pili wenye alama 21, Fountain Gate wenye alama 20 sawa na Yanga Princess wakikamilisha nne bora.
Katika chati ya ufungaji bora Opa Clement ameendela kuwakimbiza washambuliaji wenzake katika Ligi hiyo akiwa kinara kwa mabao yake 9 aliyoyafunga katika michezo 9 ya raundi ya kwanza.
Anaemfwatia kwa karibu ni mshambuliaji wa Fountain Gate Princess mwenye mabao 8 na Deonisia Minja wa JKT Queens na Jentrix Shikangwa wa Simba Queens wakiwa na mabao 7.
Opa Clement ambae pia ni nahodha wa Simba ameendela kuuwasha moto katika Ligi hiyo tangu ilipoanza na kuonekana ameongezeka makali kutoka na uzoefu mkubwa alioupata katika Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake iliyofanyika nchini Morocco ambapo Simba walishiriki kwa mara ya kwanza mwaka jana na kushika nafasi ya nne.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena mwezi March mwaka huu ambapo itakua inaingia hatua ya lala salama na Simba watakua ugenini kufungua raundi ya pili dhidi ya JKT Queens katika Dimba la Meja Generaji Isamuhyo.