Msemaji wa klabu ya Azam FC Thabit Zakaria ametoa maoni yake baada ya klabu iliyopanda daraja msimu huu Kitayosce inauojulikana kama Tabora United kumsajili mlinda mlango kutoka Nigeria.
Tabora United imekamilisha usajili wa mlinda mlango na nahodha kutoka Enyimba Fc John Noble akiwa pia ni kipa wa timu ya Taifa ya Nigeria.
Kupitia ukurasa wake wa instagram Zakaria Thabit ama Zaka ZaKazi ameandika “Golikipa namba moja na nahodha wa mabingwa wa Nigeria, Enymba FC, John Noble, amejiunga na Tabora United ya Tanzania,” alisema na kuongeza “Enyimba ni klabu kubwa kuliko zote Nigeria. Klabu iliyofanikiwa zaidi kuliko zote Nigeria, na ndiyo klabu yenye mashabiki wengi kuliko zote Nigeria.”
Zaka za Kazi ameuelezea wasifu wa nyota huyo mkongwe na mzoefu lakini pia ameonyesha pia jinsi Azam Tv inavyowapa nguvu ya kiuchumi vilabu vyetu nchini.
“Mwaka jana, 2022, klabu hiyo ilimtangaza kipa wake John Noble kuwa nahodha wao. Noble alichukua usinga huo baada ya nahodha Austin Oladapo kutumika TP Mazembe ya DRC.
Mwaka 2021, John Noble alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria kilichoshiriki AFCON.”
“Kipa wa daraja hili ndiyo ametua Tabora United ya Tanzania ambayo imepanda ligi kuu msimu huu. Hiki siyo kitu kidogo hata kidogo. Ligi ya Tanzania imekuwa kubwa na kuvutia wachezaji wengi kutoka sehemu mbalimbali.
Vyombo vya habari vya Nigeria vimeandika kwamba John Noble ameenda Tanzania kutafuta malisho bora. Mstari huu ndiyo kiini cha andika langu kwamba hii kitu haizungumzwi vya kutosha.”
“Nahodha wa mabingwa wa kihistoria wa nchi kubwa kama Nigeria, anaenda klabu ya Tanzania iliyopanda daraja kutafuta malisho bora. Tanzania kwa sasa kuna malisho bora sana kwa wachezaji.
Yaani kwa sasa inachoifanya Afrika ligi ya Tanzania kinakaribia ligi ya Saudi Arabia inachoifanya Ulaya. Yaani kupora wachezaji bora na muhimu kutoka sehemu mbalimbali, fedha ikiongea.
Na hii yote ni mkataba wa Azam TV, Azam TV wanatoa dola milioni 10 kwa mwaka kwa ajili ya haki za matangazo ya ligi. Hongera sana Azam TV. Hongera sana Bodi ya Ligi. Hongera sana TFF. Mpira wetu unakua sana, tusijichukulie poa!”