Kwenye soka la sasa mshambuliaji wa kati hana thamani kubwa sana ukilinganisha na mshambuliaji ambaye hufunga magoli na kutoa pasi za mwisho za magoli akitokea pembeni. Hawa watu wamefanya mahitaji ya mshambuliaji halisi wa kati yawe ya kawaida sana ukilinganisha na kipindi cha nyuma.
Kipindi cha nyuma mshambuliaji wa Kati alikuwa anategemewa sana kwenye kufunga magoli , lakini kwa sasa imekuwa tofauti , mshambuliaji anayetokea pembeni amekuwa anategemewa sana kwenye kufunga magoli .
Kocha anaweza akawa na false 9(namba tisa muongo ) kwenye kikosi chake kwa ajili ya kumfanya mchezaji wa pembeni afunge False 9 ( namba tisa muongo) huwa wanahakikisha wanatengeneza spaces (uwazi) kwa ajili ya washambuliaji wa pembeni kutumia hizo spaces (uwazi) kwa ajili ya kufunga magoli. Mfano, Liverpool wanamtumia Roberto Firmino kama false 9 (namba tisa muongo) kwa ajili ya kutengeneza spaces (uwazi) kwa wachezaji wa pembeni kufunga (Saido Mane na Mohamed Salah).
Saido Mane na Mohamed Salah ni ghali sana kwenye soko la wachezaji duniani kwa sasa. Wachezaji hawa wamekuwa ghali kwa sasa , ni wachezaji hawa hawa ambao wanahatarisha maisha ya washambuliaji wa kati. Siku hizi ni wachache sana, sijui wameenda wapi, kwa kifupi wanapotea kwa kasi sana.
Na watu hawashtuki kupotea kwao kwa sababu hakuna pengo ambalo wanalipata. Real Madrid hawakuwa na lawama kwa kupotea kwa watu kama Ronaldo De Lima kwa sababu walimpata Cristiano Ronaldo.
Hawa watu ndiyo wanaoitawala dunia ya mpira kwa sasa, na ndiyo wana thamani kubwa sana kwenye dunia ya mpira wa sasa. Kila uchwao thamani ya Jordan Sancho inazidi kupanda maradufu , Mbappe bei yake inazidi kuimarika kila uchwao.
Kuwa sasa kila jicho huwatazama wao, makocha hutamani kuwa nao kwenye kikosi, mashabiki hutamani kuvaa jezi zenye namba zao na hata makampuni ya kibiashara hutamani kuwapa mikataba minono ya kibiashara.
Huwezi kupata hasara kwa hawa watu kwa sababu ni vipenzi vya wengi. Muda mwingi hutumia kuwafurahisha mashabiki wao. Kwa sasa wanategemewa sana kwenye kufunga ilihali hutokea pembeni mwa uwanja wanapocheza .
Muda mwingi hutumia kuibeba timu yao, ndiyo maana Leo hii Mbappe ni muhimu zaidi ya Cavani, inawezekana Cavani anafunga sana lakini hatazamiki kwa umuhimu mkubwa kama Mbappe.
Mtu ambaye anafunga na kutoa pasi nyingi za magoli tena mbaya zaidi akitokea katika eneo ambalo siyo la karibu na goli ukilinganisha na Cavani.
Haya ndiyo maisha ya sasa ya mpira, ndiyo tunayoyaishi na tumeyachagua kwa kuyaamini ni bora zaidi kuliko maisha ya zamani.
Ndiyo maana tunatunga mashairi mengi sana kuwatukuza watu kama kina Neymar, na kuwasifu watu kama kina Ousmane Dembele. Kwa sababu tu hawa ndiyo huleta utukufu katika dunia yetu ya kisasa ya mpira. Dunia ambayo ni ngumu kuikwepa kabisa.
Dunia ambayo wenzetu Yanga walianza kuishi kwa muda mrefu sana. Yanga kwa muda sana hawajawahi kumtegemea sana mshambuliaji wa kati.
Ni msimu huu na msimu uliopita ndiyo wameanza sana kuwategemea washambuliaji wa kati. Kuna msimu zilihitajika juhudi za Obrey Chirwa kuibeba Yanga lakini haikufika popote.
Msimu jana kila mwana Yanga alitegemea miguu ya Makambo katika ufungaji wa magoli. Huyu ndiye mfungaji wao bora kwa msimu uliopita .
Kwa kifupi huyu ndiye aliwabeba sana na ndiye alionekana ana thamani kubwa kwa sasa ndani ya kikosi cha Yanga. Kitu ambacho hakikuwepo kipindi cha nyuma.
Kipindi cha nyuma Yanga ilikuwa inawategemea sana wachezaji ambao walikuwa wanacheza pembeni. Hawa ndiyo walikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa pasi za mwisho.
Masikio yangu yalianza kupevuka kimpira kwa kuanza kumsikia Edibily Lunyamila. Mchezaji bora wa Yanga. Huwezi kutaja kikosi bora cha wakati wote cha Yanga bila kumtaja Edibily Lunyamila. Hakuwa mshambuliaji wa kati.
Alikuwa anatokea pembeni mwa uwanja, alifunga magoli na kutoa pasi za mwisho nyingi akitokea pembeni. Baada ya Edibily Lunyamila alikuja Said Maulid.
Huyu naye alikuwa anafanya kile kile ambacho Edibily Lunyamila alikuwa anakifanya kipindi chake. Mrisho Ngassa ndiye alikuja kuwa lulu. Huyu alikuwa mchezaji mwenye thamani kubwa sana. Na alikuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana ambacho hakikufika sehemu kubwa.
Tuachane na hii mada , ni mada ya siku nyingine. Turudi kwenye mada yetu. Mrisho Ngassa alifunga sana akitokea pembeni.
Na inasemekana ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa timu ya taifa ya Tanzania bara. Magoli ambayo aliyapata akitokea katika eneo la pembeni mwa uwanja.
Alipoondoka yeye alikuja Simon Msuva, huyu naye alikuwa na sifa zile zile za kina Ngassa. Alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu mara mbili akitokea pembeni mwa uwanja.
Alikuwa na thamani kubwa sana, lakini baada ya yeye kuondoka Yanga walikosa mtu ambaye anaweza kuishi kwenye dunia yao , dunia ya kisasa.
Dunia ambayo kwa sasa watu wengi wanaishi, dunia ambayo wachezaji wanaotokea pembeni mwa uwanja wanahitajika sana.
Lakini kuna kitu kimoja ambacho Yanga nimetamani kuwakumbusha na kuwauma sikio tu kwa wema. Pale GorMahia kuna kijana anaitwa Dickson Ambundo.
Mchezaji ambaye msimu juzi kwenye ligi daraja la kwanza alikuwa mfungaji bora akiwa na magoli 11. Msimu jana kwenye ligi kuu ya Tanzania bara amefunga magoli 7, magoli manne nyuma kufikia idadi ya magoli yake msimu juzi akiwa Alliance FC.
Ni aina ya wachezaji ambao Yanga huwatumia sana kwa kipindi kirefu na kwa kipindi hiki wamepotea kwenye kikosi cha Yanga. Ana kipaji kikubwa sana, ni moja ya vijana ambao wakipewa nafasi kubwa wanafanya makubwa, ni vyema Yanga wamuwahi kabla hawajawa wa gharama.
Mrisho Ngassa bado yupo Yanga , hana nguvu sana ukilinganisha na nguvu alizokuwa nazo misimu mingi iliyopita , kwa kipindi hiki ambacho Yanga inasubiri Mrisho Ngassa aende ulikuwa mtu sahihi kumwingiza mtu ambaye ana sifa nyingi ya Mrisho Ngassa na anakidhi mahitaji ya soka la kisasa ambaye ni Dickson Ambundo.