Sambaza....

WINGA/kiungo-mshambulizi wa Yanga SC, Mrisho Ngassa amewaomba mashabiki/wapenzi na wachama wa klabu yao kuendelea kuwaunga mkono katika kipindi hiki kigumu wanachopitia kiuchumi, na kusisitiza wao kama wachezaji wataendelea kusaka ushindi uwanjani.

Ngassa alifunga goli la ushindi katika mchezo wa Alhamis hii dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga na kuifanya timu yake ifikishe alama 29 baada ya kucheza 11.

‘Timu hiyo ya Wanachi’ imeanza vyema kampeni yake katika viwanja vya ugenini na wengi walikuwa waKiamini mabingwa hao mara 27 wa kihistoria watashindwa kufanya vizuri mikoani kutokana na hali yao ya kiuchumi na Ngassa amewaonya wote wanaokibeza kikosi chao.

“ Ni ushindi mzuri kwetu kama timu.’ Anaanza kusema winga huyo ambaye usajili wake Julai mwaka huu ulibezwa na wengi. “ Kocha wetu ( Zahera Mwinyi) amekuwa nasi bega kwa bega, na naweza kusema ni kati ya walimu wazuri ambao najivunia kucheza chini yake.” Anaongeza kusema kiungo huyo mwenye magoli matatu katika ligi kuu msimu huu.

Yanga ilicheza michezo 10 mfululizo katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushinda nane huku wakitoa sare mara mbili, baada ya kuifunga Mwadui FC timu hiyo itakuwa Kaitaba Stadium, Bukoba siku ya Jumapili kuwavaa Kagera Sugar FC.

“ Mashabiki na wachama wa klabu wanapaswa kuendelea kutuunga mkono kwa kujitokeza uwanjani kutupa sapoti kila tuinapocheza. Sisi kama wachezaji tutaendelea kufanya kazi yetu kwa kujitolea ndani ya uwanja na kusahau matatizo yaliyopo katika masuala ya uchumi hivyo nao wanatakiwa kutupa nguvu kwa kuendelea kuja uwanjani hata kuchangia kile walichonacho.” Anasema Ngassa nilipofanya nae mahojiano mafupi akiwa Shinyanga.

“ Tunaenda Kagera na lengo letu ni kushinda. Kama nilivyowahi kukwambia mwanzoni mwa msimu huu, tunapaswa kushikamana kama timu na kupambana kwa msimu mzima kama tunataka kurudisha ubingwa tuliopoteza msimu uliopita.”

Sambaza....