Muungurumo ni mkubwa mno tena wenye nguvu kubwa sana kutoka katika mbuga ya msimbazi, mbuga ambayo haikuwa na malisho kwa muda wa misimu minne (4).
Misimu minne (4) imekuwa misimu yenye mateso na njaa kali sana kwa Simba anayepatikana katika mbuga ya msimbazi. Kila kitu kilikuwa kigumu kwake hata afya yake ilizorota kwa kukosa malisho mazuri na kusimangwa sana na wapinzani wao Yanga.
Masimango ambayo yalikuwa yanawakosesha raha kwa kiasi kikubwa Simba , kitu ambacho kilisababisha Simba kujipanga ili kutafuta furaha yake binafsi.
Mwanzo wao bora ulianza kuonekana kwenye usajili wao bora walioufanya kabla ya kuanza msimu. Walisajili wachezaji ambao walionekana wanaweza kuibeba Simba na kitu hiki kimeonekana na kinawapa furaha kipindi hiki.
Furaha ambayo waliikosa kwa muda mrefu wa maisha yao, hakuna kinachoshindikana penye juhudi na maarifa ndiyo maana Simba wamefanikiiwa msimu huu kuchukua ubingwa ambao walikuwa wameukosa kwa muda mrefu.
Furaha mpaka sasa hivi imewajaa katika kila kiungo cha mwili wao, kitu ambacho ni kizuri na wanahaki nacho kukifurahia.
Kinachokuja kunisikitisha ni kipindi ambacho unapoona kiongozi ambaye kwa wakati huu angefikiria namna ambavyo angeigeuza furaha ya mashabiki wa Simba kuwa biashara yenye manufaa kwa Simba lakini yeye anafikiria namna ambavyo anaweza kuwafanya mashabiki wa Yanga waisusie mitandao ya kijamii!.
Nilitegemea vitu chanya katika masikio yangu kuhusu huu ubingwa wa Simba, kwa mfano kungekuwepo na Kampeni maalumu ambayo ingeanza katika mechi dhidi ya Singida United mpaka mechi ya mwisho.
Kampeni hii ingeongozwa na Hadji Manara kama mtu mwenye ushawishi mkubwa, kama msemaji mkuu wa Simba, kama mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba na kama mtu anayehusika na masuala ya mahusiano ya jamii ndani ya Simba ( Public relation).
Kampeni hii ingehusu nini? Tangu mwanzo dalili zilikuwa zinaonesha kuwa Simba ilikuwa inaelekea kutwaa ubingwa hii ni kutokana na ubora wao na mwenendo wa wapinzani wao wa karibu Yanga kuonekana mbovu.
Kwa hiyo kwa asilimia 70 Simba tulikuwa tumeingia mwezi wa nne wengi tukiwa na uhakika wa Simba kutwaa huu ubingwa, hivo viongozi wa Simba wangejiandaa mapema kuupokea huu ubingwa.
Inavyoonekana kwa sasa hawakujiandaa kuupokea huu ubingwa ! , kwanini nasema hivo? Zingeandaliwa jezi na skafu zenye nembo “SIMBWA BINGWA” Mapema ili zitumike kwenye michezo ambayo imebaki huku tukijua Simba ni bingwa.
Ndipo hapa umuhimu wa kampeni ambayo ingeongozwa na Hadji Manara ungeonekana. Jezi zingeenda mapema Singida United, kabla ya kupeleka jezi Singida United , Hadji Manara angeongoza kampeni kwa mashabiki kuwahamasisha wanunue jezi rasmi kutoka kwenye klabu na kuwaelekeza sehemu sahihi zinapopatikana.
Kampeni hii ingekuja na punguzo la gharama ya tiketi kwenye mechi za nyumbani, kwa mfano mechi ya Simba na Kagera Sugar ambayo itachezwa katika uwanja wa Taifa, Simba wangeweka utaratibu wa punguzo la tiketi kwa 10% kwa kila shabiki ambaye angekuja na jezi pamoja na skafu waliyonunua kwenye klabu ya Simba.
Kuna wakati Simba walianza kuuza jezi zao kwa punguzo la bei wazo lilikuwa zuri, wazo hili lingetumika na hapa ili kupambana na makanjanja wanaotumia nembo ya klabu kuchapisha jezi kwa manufaa yao.
Mashabiki wengi hununua jezi kutoka kwa hawa watu kwa sababu ya gharama ndogo ya jezi, hivo wangetumia wazo la kupunguza bei ili kuwafanya mashabiki wengi wanunue bidhaa hizi na timu inufaike.
Nadhani hii kampeni ingekuwa kampeni bora ambayo Hadji Manara angetakiwa kuifanya kwa sasa kuliko hii kampeni ya kuwafanya mashabiki wa Yanga kuikimbia mitandao ya kijamii.
Hii ni kampeni isiyokuwa na tija ya aina yoyote kwa klabu, ni kipindi sahihi kwa Hadji Manara kutumia ushawishi alionao kuiingizia Simba pesa nyingi kutokana na nembo ya klabu.