José Mário dos Santos Mourinho Félix ndiyo majina ambayo alipatiwa miaka 55 iliyopita. Ilikuwa ni ngumu kugundua mapema kuwa huyu atakuja kuwa kocha bora duniani.
Kocha ambaye alikuja katika kipindi ambacho vijana wengi walikuwa hawapewi nafasi ya kuwa makocha wakuu katika timu zao.
Mikono yake ilifanikiwa kufuta hiyo dhana, kila kijana aliyekuwa na ndoto ya kuwa kocha bora kwa baadaye alibaki akimwangalia Jose Mourinho.
Kocha ambaye hakucheza katika soka la ushindani licha ya kwamba katika maisha yake ya uchezaji aliwahi kuwa kiungo.
Ndiye kocha ambaye aliwashangaza wengi kipindi ambapo alipofanikiwa kuchukua ligi ya mabingwa barani ulaya akiwa na FC Porto.
Lilikuwa jambo ambalo wengi hawakutegemea na ikizingatiwa kuwa tulikuwa tumezoea timu kubwa kutoka barani ulaya ndiyo wakiwa wamiliki halali wa hilo kombe.
Dunia ilishtuka, kila mtu akageuza jicho kumwangalia ni nani huyo aliyefanikiwa kuipa ubingwa wa klabu bingwa ulaya FC Porto!?, tena mbele ya Barcelona, Bayern Munich, Real Madrid, Manchester United!?.
Ulikuwa mshangao mkubwa sana , na mshangao huu ulizidi kuongezeka kipindi ambacho jina la Jose Mourinho lilipokuwa linatajwa kama kocha ambaye aliipa FC Porto mafanikio hayo.
Hakuwa kocha mwenye jina kubwa, hata mafanikio yake kipindi cha nyuma kabla hajafika FC Porto yalikuwa hayatishi sana.
Mafanikio yake makubwa awali ni kuwa mkalimali wa Sir Bobby Robson pale Sporting Lisbon pamoja na Barcelona.
Hata baada ya Sir Bobby Robson kuondoka Barcelona, Jose Mourinho aliendelea kubaki chini ya Louis Van Gaal.
Hata ndiyo yalikuwa mafanikio makubwa kwa Jose Mourinho, kuwa chini ya makocha bora duniani tena chini ya timu bora yenye wachezaji bora ndicho kitu ambacho kilimpa nguvu ya yeye kuamini anaweza kuishi na kila aina ya wachezaji na wakamsikiliza.
Ujasiri huu ulimfanya aamini anaweza kuiongoza timu yoyote ndiyo maana aliwahi kuomba kazi katika timu ya Barcelona.
Ujasiri huu ulimfanya arudi Ureno, nyumbani kwao ambapo ndipo milango ya mafanikio yake ilikuwa imejengwa.
Alifanikiwa kupata funguo za kufungulia milango ya mafanikio yake. Chini ya FC Porto kila timu ilitamani kuwa naye.
Kila mchezaji alitamani kuwa chini ya Jose Mourinho, kocha kijana ambaye alionekana anauwezo mkubwa wa kumfanya mchezaji awe na njaa ya mafanikio.
Na inawezekana ndiye kocha ambaye aliyetambulisha matumizi makubwa ya fedha kwenye mpira akiwa na Chelsea miaka ya 2000.
Chelsea ndiyo yalikuwa na bahati ya kumpata Jose Mourinho, tena alikuja Chelsea kipindi kizuri. Kipindi ambacho Abrahamovich alikuwa anatamani kufanya mapinduzi makubwa katika soka.
Alifanya chochote kile ambacho aliambiwa kuwa kinafaa kufanyika ili timu yake iwe imara.
Alimleta Jose Mourinho, Jose Mourinho akamwaminisha Abrahamovich katika matumizi ya pesa ili kupata mafanikio makubwa.
Neno “hapana” halikuwepo katika kinywa cha tajiri wa Chelsea, alifanya kila ambacho Jose Mourinho alikitaka ili mradi Chelsea iwe nyumba ya vikombe.
Ndicho kitu ambacho kilikuja kutokea, baada ya miaka 50 , Chelsea ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya England chini ya Jose Mourinho (The special one) tena akiweka rekodi ya timu ya kwanza kumaliza ligi kuu ikiwa na alama 95.
Ikaonekana Jose Mourinho ana damu ya mafanikio, akili yake ilikuwa inawaza vikombe ndiyo maana kila alipoenda baada ya kutoka Chelsea alifanikiwa kuzifanya timu zibebe makombe.
Kwake yeye ilikuwa kawaida kuchukua vikombe alipokuwa chini ya Intermilan kwa sababu aliamini hiyo ndiyo kazi ambayo ilimleta duniani.
Kazi ambayo iliwafanya RealMadrid wamchukue kwa sababu ni timu ambayo inaamini makombe yalianzishwa kwa ajili yao.
Waliamua kumleta kocha mwenye DNA ya makombe. Hata baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka na Manchester United kujaribu makocha wawili, waliamua kumfikiria Jose Mourinho.
Waliamini ndiye mtu pekee ambaye angewarudisha kwenye ladha waliyokuwa wanapata chini Sir Alex Ferguson.
Ladha tamu ya vikombe, ladha ambayo iliwafanya mashabiki wa Manchester United watembee kifua mbele wakiamini kuwa wao ndiyo Wafalme wa England ndigo maana waliipiku Liverpool katika usukani wa kuchukua vikombe vya ligi kuu ya England mara nyingi.
Miaka mitano imepita bila wao kuchukua kombe la ligi kuu ya England. Hii ndiyo kiu waliyonayo mashabiki wengi wa timu ya Manchester United.
Ndiyo maana walimleta Jose Mourinho, kocha ambaye alichukua ligi kuu ya England mara tatu kabla hajafika Manchester United.
Ni silaha moja tu ambayo ilikuwa anaitumia kipindi ambacho alifanikiwa kuchukua kombe la ligi kuu ya England nayo ni kuwa na timu imara kwenye safu ya ulinzi.
Aliamini kuwa timu yenye safu imara ya ushambuliaji inakuwezesha kushinda mechi lakini timu yenye safu imara ya ulinzi inakuwezesha kushinda vikombe.
Ndicho kitu ambacho ilikuwa anatembea nacho Jose Mourinho kila alipokuwa anapita.
Na alifanikiwa sana kupitia hiki kitu alichokuwa anakiamini. Safu imara ya ulinzi ilimpa vikombe.
Ndiyo maana ametumia muda mrefu na fedha nyingi kusajili wachezaji wa ulinzi akiwa Manchester United.
Pamoja na kusajili wachezaji wa ulinzi lakini Manchester United msimu inaonekana haiko vizuri katika eneo la kujizuia.
Msimu huu karuhusu magoli saba (7) katika mechi tatu. Wastani wa kufungwa goli mbili kila mechi.
Kitu ambacho awali hakikuwepo kwa Jose Mourinho kwa sababu safu ya ulinzi kwake ndiyo ilikuwa nguvu yake lakini kwa sasa nguvu zake zinaonekana zinaelekea kuisha.