Katika ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Young Boys katika uwanja wa Old Traford, katika muendelezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya (UCL) Kocha wa Manchester United Jose Mourinho alishangilia goli la kiungo Mmbeligiji Marouane Fellaini kwa staili ya aina yake.
Mourinho alionekana kumwaga chupa za maji nje na ndani ya uwanja kama mtu aliyechanginyikiwa kutokana na goli hilo lililofungwa dakika za nyongeza.
Baada ya mchezo kocha huyo alieleza sababu za kushangilia kwa staili hiyo na kusema kuwa furaha ilipitiliza ndio sababu ya kushangilia hivyo.
“Kabla ya goli nilichanganyikiwa kwa kiasi kikubwa, goli la Fellain lilikuwa msaada na faraja kwangu”
“Bila shaka hatukuwa tunacheza ili tutoke sare, tulikuwa tunatafuta ushindi katika mchezo huu na hatukukata tamaa mpaka dakika za mwisho”
Mourinho aliongeza kwa kusema kuwa, isingekuwa David de Gea kuokoa mpira uliombabatiza mshambuliaji Ulisses Garcia wa Young Boys, kusingekuwa na goli la ushindi katika mchezo huo.
Mourinho alitumia nafasi hiyo kutuma ujumbe kwa mashabiki na wapenzi wa Man U kwa kusema kuwa uzoefu wake katika michuano mikubwa barani ulaya utaisaidia kuifikisha timu hiyo mbali.
Takwimu zinaonesha kuwa Jose Mourinho kama kocha amecheza michuano ya hii kwa miaka 16 na alifuzu kwenda katika hatua ya mtoano mara 14 na kucheza michuano ya Europa mara 2 na kufanikiwa kubeba ndoo.
Ushindi huo wa Man U unawafanya kukutana na Valencia mwezi ujao wakiwa tayari wameshafuzu kwenda katika hatua ya mtoano baada ya Valencia kukubali kipigo cha goli 1-0 dhidi ya vibibi kizee vya Turin, Juventus.