Sambaza....

NAPAZA sauti juu yangu nikisema wazi Victor Moses amedhulumiwa jasho lake. Nitasema hivi kokote kule ambako nitaitwa kuelezea amedhulumiwaje. Nitakueleza huko chini.

Shusha pumzi kwanza. Haya ipandishe tuendelee. Jina la Moses haliko katika tatu bora ya wachezaji wa Afrika wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka huu. Majina yaliyoko ni Salah Mane na Aubameyang.

Kabla hatujaendelea na andiko tunapaswa kufahamu kuwa ndani ya mwaka huu Salah na Mane wamezifanya timu zao za taifa ziwe na tiketi ya kwenda Urusi mwakani kama ilivyo kwa Moses. Lakini Moses amewashinda wenzie kwa kutwaa EPL akiwa na Chelsea. Hapa siandiki kuhusu Aubameyang, sioni alilofanya kuanzia Borrusia Dortmund mpaka Gabon. Sioni haja ya kumuandika.

Katika msimu huu unaoendelea Salah anafanya vyema kuliko wapinzani wake na kila mmoja analijua hili. Salah amewazidi kwa mbali Mane, Aubameyang na Moses, lakini msimu huu haujaisha bado, hatuna haja ya kumzungumzia sana. Tumzungumzie Salah wa As Roma kisha Tumzungumzie Mane wa Liverpool.

Mwaka huu As Roma ya Salah ndani ya Italia haijashinda chochote kile. Taji la Ligi na Copa Italia vyote viko mikononi mwa Kibibi kizee cha Turin (Juventus). Ufungaji bora ulikwenda kwa Edin Dzeko, top assist hakuwa Salah, jamani mashabiki wa Salah niambieni mchezaji wenu kashinda kitu gani mwaka huu?

Mane tunajua alichokivuna na Liverpool mwaka huu, sihitaji kukirudia. Najua nikirudia nitawakera kaka zangu Joseph Silumbe, Ezekiel Kamwaga, John Msowoya, Sweddy Mkwabi, Mkubwa Kambi. Sitaki kuwakera wakubwa zangu. Nawaheshimu sana.

Binafsi sifahamu vigezo vilivyotumika kumuweka kando Moses kwenye hizi tuzo. Kama Moses hastahili kushinda tuzo hii nani mwingine aliyestahili?

Ninachokiona mafanikio ya Salah na Mane ni kuyawezesha mataifa yao kwenda Urusi kitu ambacho Moses nae amekifanya na Nigeria.

Nakubali msimu huu ambao unaendelea Salah na Mane wako katika kiwango bora kuliko Moses, lakini hatuwezi kuhesabia msimu haujaisha, lakini isifanye tuzipuuze nguvu za Moses. Kama tuzo zingekuwa zinatolewa kwa nusu msimu ‘kama hii ya Afrika’ nadhani tuzo ya mchezaji bora wa dunia aliyochukua Ronaldo wiki iliyopita alipaswa kuichukua Messi.

Ndani ya msimu huu Messi amefanya vyema kuliko Ronaldo, lakini msimu haujaisha bado hatuwezi kuujadili. Lakini tuzo ya mchezaji bora wa dunia imekwenda kwa Ronaldo aliyestahili kwa asilimia 100.

Kwa anayefahanu vigezo vipya vya CAF anisaidie juu ya tuzo hii. Inawezekana nikawa nimekosea kwa mchezaji bora kutakiwa kuwa na uwezo wa kupiga chenga nyingi na kupiga magoli ya video, huku timu yake ikikosa mataji. Nielewesheni jamani.

Moses hakufanyiwa fair. Mwaka 2015 ambao staa wetu Mbwana Samatta alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, alishinda kwa sababu aliisaidia TP Mazembe kushinda taji la Afrika. Hakuna sababu nyingine.

Samatta aliingia tatu bora akiwa na Bakri Al Madina (El Merreikh) na Robert Muteba Kidiaba (TP Mazembe ). Madina ndiyo alikuwa mfungaji bora akifunga mabao 9, Samatta alikuwa mfungaji bora wa pili akifunga mabao 8. Unadhani nini kimempa tuzo Samatta kama sio tuzo?

Sambaza....