Sambaza....

Mwanzo alisema ni sababu za kimakubaliano zinazomzuia kujumuika na wenzake klabuni, ikaripotiwa pia yupo kwao Zanzibar anaendelea na maisha yake ya kawaida nje ya soka wakati timu yake ikiwa tayari imecheza mchezo mmoja wa ligi kuu Tanzania Bara.

Haitoshi, ameibuka tena na kusema anaumwa magoti na uongozi wa klabu yake unafahamu. Yote haya yananipa maswali ya kujiuliza, je, Mohamed Issa ‘Banka‘ ni usajili mwingine ‘hewa‘ uliofanywa na utawala wa Frank Sanga ndani ya Yanga SC baada ya awali kufanya hivyo kwa beki Mcongoman, Feston Kayembe mwaka mmoja uliopita?

Kayembe

Kama sivyo, Banka yuko wapi ikiwa miezi miwili inakaribia tangu alipotambulishwa kama mchezaji wa Yanga? Kwanini uongozi unashindwa kutoa taarifa rasmi ili kupunguza maswali na sintofahamu ya wanachama na wapenzi wa klabu? Wanaogopa kudanganya kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo kwa Kayembe?

BANKA NI KAYEMBE MWINGINE?
Ni kiungo ambaye mwezi kama huu mwaka uliopita wapenzi wengi wa kandanda nchini walimtaja kama mchezaji bora wa kutawanya pasi timilifu katikati ya dimba la kati.
Pasi zake za kwenda mbele na jicho la ziada katika upigaji wa pasi za kupenyeza huku akimiliki vyema mpira viliifanya Mtibwa Sugar FC kuzibana mno Simba SC, Yanga na Azam FC katika michezo ambayo mabingwa hao wa FA walicheza na vigogo hao jijini Dar es Salaam.

Ndani ya uwanja, Banka alikuwa amepiga hatua kadhaa mbele lakini miezi 12 tangu alipotawaka kiungo katika Simba 1-1 Mtibwa, Yanga 0-0 Mtibwa mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar amerudi atua nyingi nyuma. Na kinachoendelea kumrudisha ni mambo ya nje ya uwanja.

Kama awali alisema sababu inayomzua kujiunga na timu ni uongozi kushindwa kutekeleza makubaliano yao ya mkataba Kwanini sasa aseme yu mgonjwa! Aliumia vipi, akiwa wapi, anafanya nini na kwa ruhusa ya nani pengine ingekuwa na maana kama uongozi wa klabu ungetoa tamko rasmi.

Banka akitambulishwa wakati akijiunga na Yanga

Banka ni mchezaji wa Yanga kwasababu pia walishamtambulisha hivyo kitendo cha uongozi kuendelea kukaa kimya ni sawa na kuwadharau wanachama wao ambao wamekuwa wakiwahamasisha kuichangia klabu yao iliyotetereka kiuchumi.
Wakati ule Kayembe ambaye ilisemwa alipewa milioni 20. uongozi ulisema hati ya usajili wa kimataifa- ITC imekwama na mlinzi huyo wa kati angeanza kuonekana akiichezea Yanga mwezi Januari iliyopita.

January ikapita wala hakuonekana Kayembe zaidi ya picha zake wakati alipotambulishwa akiwa amevaa jezi ya Yanga Agosti, 2017 uongozi wa Sanga aliyejiuzulu mwezi uliopita haukuwahi tena kuwaambia wanachama na wapenzi wa klabu chochote kuhusu Kayembe ambaye wakati anatambulishwa walisema kasaini Miaka miwili.
Sasa ni hivyo pia kwa Banka? Toeni Taarifa!

Sambaza....