Sambaza....

Baada ya kimya kirefu, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzim wa klabu ya Simba, Mohamedi Dewji ameibuka  leo na kusema kuwa Simba kamwe haiteteleki kutokana na matokeo iliyoyapata dhidi ya UD DO Songo katika mchezo wao wa klabu bingwa Afrika.

Simba ilitoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Songo katika uwanja wa taifa, matokeo ambayo yameitupa klabu hiyo nje ya mashindano kutokana na goli la ugenini licha ya mchezo wa kwanza kutoka sare tasa.

Mo amedai kuwa matokeo mabaya ya Simba katika katika mchezo huo ndiyo yaliyomuweka nje ya chaki kwa kipindi sasa kabla ya kujitokeza leo.

“Wanasimba naomba mnisamehe kwa ukimya, Maumivu ya matokeo yametupata sote. Naomba tukumbushane : Sisi ni SIMBA, Simba lazimaanyanyuke, hawezi kukata tama” alisema Mo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mo ameendelea kwa kuwaomba Wanasimba kutovunjika moyo na badala yake wakitumie kipindi hiki kujipanga zaidi ili kurudisha furaha ya Wanamsimbazi msimu ujao.

“Roma haikujengwa kwa siku moja, tuwe wavumilivu tutafika tu Insha’Allah” alimalizia.

Baada ya kutolewa katika mashindano hayo ya kimataifa kwa sasa Simba imejipanga kuhakikisha inatetea taji lake la ligi kuu Tanzania bara, huku ikianza vizuri kwa ushindi wa goli 3-1 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa kwanza wa ligi.

Kwa sasa ratiba ya Simba itasimama kidogo kupisha ratiba ya taifa stars katika maandalizi ya kucheza mchezo wa kufuzu kombe la dunia dhidi ya Burundi. Mechi ya Simba inayofuata itachezwa tarehe 17/9/2019 dhidi ya Mtibwa katika dimba la uhuru endapo ratiba haitabadilika.

Sambaza....