Mnyama Simba anakwenda kushuka dimbani leo usiku katika mchezo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa ugenini Morocco dhidi ya Wydad Casablanca.
Mabingwa watetezi hao watawakaribisha Simba katika dimba la Mohamed wa tano katika Jiji tajiri la Casablanca wakikumbuka kipigo cha bao moja bila walichopata katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam katika mchezo wakwanza.
Simba wanakwenda kupambana katika uwanja ambao si mgeni kwao na wanalifahamu joto la uwanja huo kwani siku nyingi hazijamalizika tangu waingie katika dimba la Mohamed wa tano na kupoteza kwa mabao matatu kwa moja dhidi ya Raja Casablanca mahasimu wa Wydad Casablanca.
Mnyama Simba ataingia uwanjani huku akijua ana mtihani mzito mbele ya Waarabu hao kutokana na aina ya uchezaji wao wakiwa uwanja wao wa nyumbani huku wakichagizwa na mashabiki wao “machizi boli” wakiongozwa na kikundi maarufu cha Ultras ambao hushangilia kwanguvu mwanzo mwisho katika dakika zote 90 za mchezo.
Simba itamkosa mlinda mlango wake Aishi Manula tena lakini pia Ismael Sawadogo, Augustine Okrah na Mohamed Outarra hawajasafiri na timu wakibaki Tanzania. Lakini pia Simba itafaidika na urejeo wa utimamu wa mwili wa mshambuliaji wake Moses Phiri “Jenerali”.
Kikosi cha Simba huenda kikawa na mabadiliko machache katika mchezo huo ambapo mlinda mlango mzoefu Benno Kakolanya anategemea kukaa langoni mbele ya Ally Salim alieanza mchezo wa awali. Lakini pia Pape Sakho huenda akapata nafasi yakuanza leo mbele ya mkongwe Saidoo Ntibazonkiza.
Tayari mwalimu wa Simba Robert Oliveira kuelekea mchezo huo amesema “Haiwezi kuwa sawa na vile tulivyocheza mechi ya kwanza ya nyumbani, lazima tutakuwa na mbinu tofauti sababu tupo ugenini. Namuamini Mungu, pia nawaamini wachezaji wangu wataweza kufuata maelekezo tuliyowapa. Tumejipanga kucheza vizuri na kupata ushindi.”
Ni wazi Wanasimba wanategemea wachezaji wap kurudia kile kilichotokea miaka 20 nyuma yaani mwaka 2003 ambapo Mnyama alimtoa Zamalek ambae alikua bingwa mtetezi tena katika ardhi ya nyumbani kwake Misri.
Wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Simba wanapaswa kupigania ndoto yakufuzu nusu fainali katika Jiji tajiri la Casablanca baada ya kucheza robo fainali tatu za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika hivi karibuni.