David Efford Chabala alizaliwa tarehe 2 Februari mwaka 1960 na kufariki tarehe 27 Aprili mwaka 1993, akijulikana zaidi kwa jina la Efford Chabala alikuwa golikipa chaguo namba moja wa Zambia kutoka mwaka 1983 mpaka kifo chake katika ajali ya ndege iliyotokea katika pwani ya Gabon mwaka 1993 na ndiye mchezaji aliyeichezea mechi nyingi timu ya Taifa ya Zambia, kwa kucheza kikamilifu mechi 108 za Kimataifa.
Chabala alikuwa mtu muhimu katika mafanikio ya kwanza ya Zambia katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (East and Central African Championship) wakati alipookoa penati tatu katika ushindi wa 3-0 kwenye changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Malawi katika fainali mwaka 1984 nchini Uganda baada ya timu hizo kwenda sare ya bila kufungana katika muda wa mchezo mzima.
Mwaka 1985 alitajwa kuwa ndiye mchezaji bora wa mwaka wa Zambia.
KAZI YAKE YA KUCHEZA MPIRA:
Chabala alizaliwa Mufulira ambako baba yake alikuwa mchimbaji wa madini, yeye alikuwa mzaliwa wa nne katika familia ya watoto 12. Alianza kucheza mpira kama mshambuliaji katika timu ya ridhaa ya Lubuto Amateur Club mjini Mufulira ambapo uchezaji wake kama golikipa ulikuja kwa bahati mbaya tu wakati alipokuwa na umri wa miaka 17. Wakati fulani katika kipindi cha mazoezi, kipa ambaye ndiye Alikuwa kipa wa timu hakuwepo hivyo Chabala akalazimishwa na wenzie kuilinda ile milingoti mitatu. Alikubali kwa shingo upande lakini alicheza vizuri na alifurahia kucheza golini na akafanya maamuzi ya kuhamia sehemu hiyo moja kwa moja.
Baada ya muda mfupi akachaguliwa kama kipa wa akiba wa Mufulira Wanderers na Makocha Samuel Ndhlovu na Dickson Makwaza. Mara tu akambadili Bernard Kabwe katika timu ya kwanza, akianza kucheza kwa mara ya kwanza tarehe 27 Julai, mwaka 1980 katika pambano la ligi dhidi ya Lusaka Tigers katika uwanja wa Shinde mjini Mufulira. Huku Wanderers wakiwa nyuma kwa mabao 2–0 mpaka wakati wa mapumziko, Chabala alimbadili Kabwe na mwisho wanaume ‘Wenye nguvu’ wakashinda mechi hiyo kwa mabao 3–2.
Chabala alicheza pia golini kwa upande wa Wanderers ambao pia ilikuwa na wachezaji wakubwa wa kiwango cha juu kama Ashols Melu, Kalusha Bwalya, Frederick Kashimoto, ndugu wawili Philemon Kaunda na Philemon Mulala, na baadaye Charles Musonda na Johnson Bwalya. Timu hii ya Wanderers ilitawala soka la Zambia kwa kunyakua vikombe mbalimbali katika miaka ya themanini na miaka ya tisini mwanzoni, wakajipatia jina la ‘Wapambanaji wakongwe wa makombe’. Hata hivyo, Wanderers hawakuwahi kushinda ligi ya Zambia kwa kipindi hicho.
Alichaguliwa kuwa Mwanamichezo Bora wa Zambia mwaka 1985 na msimu wa mwaka1988, aliwashangaza wadau wengi wa soka wa Zambia pale alipoamua kuvaa jezi ya ushambuliaji ya Wanderers, lakini akaja kufunga goli 5, likiwemo goli la tatu wakati Wanderers walipoichapa Roan United mabao 3–0 katika Kombe la Uhuru kwenye fainali mwezi Oktoba mwaka huo. Hivyo basi akawa amefuata nyayo za kipa mwingine maarufu wa Wanderers Abraham Nkole, ambaye alifunga hat-trick katika fainali hiyo hiyo ya Kombe la Uhuru mwaka 1971.
Chabala alirejea katika nafasi yake ya ugolikipa lakini akarejea tena katika ushambuliaji katika msimu wa mwaka1990 kwa kucheza mechi chache na baada ya hapo akarudi tena katika milingoti.
Alicheza kwa muda mfupi nchini Argentina katika Klabu ya Argentinos Juniors msimu wa mwaka 1991/92 lakini akarudi Wanderers mwezi Machi mwaka 1992 akidai kuwa mazingira ya mkataba wake hayakuwa na manufaa, na Klabu haikutaka kuubadilisha.
Mwezi Desemba mwaka 1992, Chabala alifanyiwa mabadiliko katika mechi ya fainali ya Kombe la Uhuru dhidi ya Nkana Red Devils baada ya kuwa amefungwa mabao matatu wakati Wanderers wakiwa wanaongoza kwa mabao 2–0 lakini wakapoteza mechi kwa kufungwa mabao 3–2. Alihusishwa na madai yaliyosemwa kuwa hakuwa na furaha baada ya kuchaguliwa kwa Ashols Melu kama Kocha Msaidizi hivyo ikadaiwa aliuza mechi. Wote wawili Melu na Chabala walikataa kuwa na msuguano wowote kati yao, wakasema wao ni marafiki wakubwa na Chabala akasema siku ile hakuwa fit na mabadiliko ya kumbadili yalikuja yakiwa yamechelewa.
Aliachwa kupangwa katika mechi tano zilizofuatia za Wanderers lakini mara tu akarejea katika nafasi yake.
KUCHEZEA TIMU YA TAIFA:
Uwezo wa Chabala katika milingoti miwili pale golini ulionwa na wanaochagua timu ya Taifa hivyo kupelekea kwa mara ya kwanza kuvaa rangi za timu ya Taifa tarehe 27 Novemba mwaka 1980 kwa timu ya Zambia ‘B’ katika mashindano ya Kombe la Chalenji yaani Council for East and Central African Football Associations (CECAFA) Cup katika mechi ya kutafuta mshindi wa 3 na wa 4 dhidi ya Malawi ambapo Zambia walipoteza kwa bao 1–0.
Hata hivyo, mchezo kamili wa kimataifa ulikuja tarehe 10 Aprili mwaka 1983 katika hatua ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) dhidi ya Sudan jijini Khartoum, ambapo Zambia walipoteza kwa kufungwa mabao 2–1. Kutoka hapo, Chabala akawa mchezaji wa kudumu wa kila mechi katika lango la Zambia kwa sehemu kubwa katika miaka 10 iliyofuatia.
Aliiongoza Zambia katika michuano ya mwaka 1984 ya CECAFA katika Kombe la Chalenji la wakubwa kama nilivyokwisha kutangulia kusema hapo awali kuwa aliokoa penalti tatu katika ushindi wa mabao 3–0 katika kupigiana penalti dhidi ya Malawi baada ya kutofungana katika muda wa kawaida.
Chabala alikuwa golini katika jaribio la Zambia kutaka kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1986 ambapo Zambia waliondolewa katika hatua ya makundi.
Ushujaa wa Chabala dhidi ya Ghana mwaka 1987 wakati wa kufuzu kwa ajili ya michuano ya Olimpiki uliisaidia Zambia kupata nafasi katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1988 jijini Seoul, Korea Kusini.
Zambia walishinda mchezo wao wa kwanza nyumbani kwa mabao 2–0 na wakasafiri kwenda Accra na mashabiki wao wakitarajia timu yao kufanya vizuri. Ghana walishambulia toka dakika ya kwanza ya mchezo, wakifanya kila walichoweza kwa Wazambia ambao pamoja na kuwa walikuwa wameshafungwa goli katika kipindi cha kwanza na Tony Yeboah, walilazimisha kusonga mbele kwa kufungwa bao 1-0 hivyo tofauti ya mabao kuwa 2-1 huku nyota wa mchezo akiwa Chabala ambaye alisimamisha mashambulizi yote ya Ghana, ikiwemo kuokoa mkwaju wa penalti wa Emmanuel Quarshie.
Baada ya mchezo, kipa wa Ghana alimkimbilia Chabala na kumuuliza ni nini ilikuwa siri ya mafanikio yake na majibu ya Chabala kwa Kiwemba yakaja kuwa maarufu katika medani ya soka la Zambia – “Kuiposafye (You just have to throw yourself)”.
Katika michezo ya Olimpiki, Zambia kwa kiasi fulani iliweka rekodi ya kuvutia kwa Charles Musonda kutawala eneo la kiungo na Kalusha Bwalya akiwa kwenye kiwango kizuri, wakatoka sare na Iraq 2–2 na kuzichakaza Italia na Guatemala kwa mabao 4–0 kila mmoja na kusonga mbele kwenye robo fainali. Hata hivyo, kiama kiliwakuta kwenye robo fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi wakati nao Zambia walipochezea kichapo cha mabao 4–0, huku Jürgen Klinsmann wa Ujerumani Magharibi akiwa katika kiwango kizuri.
Pamoja na kukatishwa tamaa huko, wengi nchini Zambia waliamini kuwa hatimaye timu ilikuwa na wachezaji wazuri wanaoweza kuipeleka nchi katika fainali za Kombe la Dunia mwaka1990 nchini Italia.
Baada ya kushinda michezo yao yote ya nyumbani, Zambia walishindwa kupata matokeo mbali kutoka nyumbani na hawakufanikiwa kufuzu kwa kwa Kombe la Dunia.
Chabala aliibuka tena na kung’ara katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1990 ambapo waandishi wa habari walimpigia kura na kumchagua yeye kuwa kipa bora wa mashindano, akiwa na “clean sheets” nne katika michezo mitano na kuisadia Zambia kushinda nafasi ya tatu.
Mara yake ya mwisho kuonekana katika Kombe la Mataifa ya Afrika ilikuwa mwaka 1992 nchini Senegal pale ambapo Zambia kwa mara nyingine tena hawakufanikiwa, wakiangushwa kwa bao 1-0 na washindi Ivory Coast katika pambano lililokwenda katika dakika 120 kwenye robo fainali.
Tarehe 20 Desemba mwaka 1992, Zambia walipoteza pambano la kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa kufungwa na Madagascar mabao 2–0, matokeo ambayo yaliwaweka katika hatari kwenye kampeni yao ya kufuzu. Mara moja Chabala aliachwa kwenye timu na alikosa michezo miwili ya Zambia ya kufuzu. Hata hivyo alisema hakushangazwa na kitendo hicho na akadai kuwa alikuwa analipia garama kwa mawazo yake aliyoyaeleza kabla ya uchaguzi kwa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ) kwamba uongozi usibadilike, kwa sababu hautafanya vizuri chini ya Rais mpya Michael Mwape. Mwape naye akajibu mapigo kwa kusema kuwa Chabala aliachwa baada ya ripoti kusema kuwa alikuwa amesimamishwa na Klabu yake, kufuatia timu yake kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Uhuru kwa Nkana. Wanderers walithibitisha kwamba Chabala alitumikia adhabu ya kusimamishwa mechi 5 ambayo adhabu hiyo iliisha muda mrefu kabla ya mechi na Madagascar. Baada ya hili, FAZ ikamruhusu kuichezea tena Zambia na mara moja akarejea katika nafasi yake katika timu ya Taifa ambayo ilikuwa inachezwa na msaidizi wake Richard Mwanza.
Pia kwa mujibu wa mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Tanzania, Sekilojo Chambua ambaye amenikumbusha kuwa Chabala alifika kucheza Tanzania mara tatu katika mji wa Mwanza.
“Ni kweli nami nakumbuka kuwa mara ya kwanza ilikuwa mwezi Januari mwaka 1986 pale timu yake ya Mufulira Wanderers ilipocheza na Yanga Africans ya Dar es salaam katika pambano la nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na pambano kumalizika kwa sare ya bila kufungana katika muda wote wa mchezo hivyo kupelekea changamoto ya mikwaju ya penalti na Yanga kushinda pambano lile na kwenda fainali jijini Dar es salaam walikopoteza kwa kufungwa na El Mereikh ya Sudan kwa penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 2-2 katika dakika 120 za mchezo.” Sekiloja Chambua.
Chabala alikuja tena Mwanza, Tanzania mwaka 1992 katika michuano ya Chalenji ya CECAFA na timu ya Taifa ya Zambia na Zambia kutolewa na Uganda katika mikwaju ya penalti baada ya kwenda sare katika muda wa kawaida, pambano ambalo Zambia
Waliupiga mwingi sana hadi mwingine kumwagika” huku Uganda ‘wakipaki treni la Dar- Mwanza’ muda wote wa mchezo na mwisho wa siku timu bora ikapoteza kwenye nusu fainali na Uganda kucheza fainali na KAKAKUONA ya Tanzania Bara ya Nahodha Gaspar Lupindo, beki Mustapha Hozza, mshambuliaji Jimmy Mored na kiungo kinda wa wakati huo, Sekilojo Chambua ambaye katika michuano hiyo mechi ya nusu fainali dhidi ya Malawi, alifunga penalti ya kifundi iliyoipeleka KAKAKUONA fainali dhidi ya Uganda na Uganda kushinda kwa bao 1-0 la mshambulizi Issa Sekatawa.
Chabala alifika tena Mwanza, Tanzania mwezi Februari, mwaka 1993, na timu ya Taifa ya Zambia, kucheza na Taifa Stars katika mchezo wa awali wa kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia, na Zambia kushinda kwa mabao 3-1 lakini Chabala akiwa golikipa wa akiba akimpisha msaidizi wake Richard Mwanza kusimama golini, huku vilevile Zambia ikiwa imekuja na nyota wake waliokuwa wakisakata soka barani Ulaya akiwemo Kalusha Bwalya na Charles Musonda ambaye Sekilojo Johnson Chambua alipambana naye vilivyo pale katikati katika dimba la CCM Kirumba mjini Mwanza.
KUFARIKI:
Tarehe 28 Februari, mwaka 1993, Zambia, wakihitaji ushindi ili kufuzu kwa ajili ya makundi katika kampeni yake kwa ajili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia waliichapa mabao 3-1 Madagascar jijini Lusaka. Wazambia tena wakajikuta wamepangwa kundi moja na Morocco na Senegal na wengi walidhani muda sasa umefika kwa Zambia kufuzu kwenda kwenye Kombe la Dunia kwa sababu walikuwa na timu mzuri ambayo ilikaa pamoja kwa muda, na benchi la ufundi ambalo lilionekana linahamasisha timu.
Tarehe 10 Aprili, mwaka 1993, Zambia walitoka sare ya bila kufungana nyumbani na Zimbabwe katika michuano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika. Wiki mbili baadaye, Wazambia waliirarua Mauritius mabao 3–0 mjini Port Louis wakiwa na Chabala kama Nahodha na Kelvin Mutale akipiga hat-trick.
Kutoka huko, timu ikafunga safari kwenda Senegal kwenye mechi yao ya kwanza kati ya mechi zao za kufuzu kwa Kombe la Dunia hatua ya makundi. Usafiri wa timu ulikuwa ni wa ndege ya jeshi la anga la Zambia (Zambia Airforce DHC-5D Buffalo plane). Baada ya kujaza mafuta jijini Libreville, Gabon ndege ilipata hitilafu na kuanguka baharini tarehe 27 Aprili mwaka 1993 ikiuwa watu wote 30 waliokuwa katika ndege hiyo akiwemo Rais wa chama cha soka cha Zambia Michael Mwape na wafanyakazi wa ndege hiyo. Taifa zima lilipatwa na mshtuko na msiba ulikuwa mkubwa zaidi wakati majeneza 30 yaliyobeba mabaki ya wapendwa wao yaliporudishwa nyumbani kwa ajili ya maziko ya kitaifa.
Ajali ya ndege ilileta siyo tu mwisho wa uchezaji wa Chabala bali karibu timu nzima ya wachezaji wenye vipaji wa Zambia na makocha wao.
Chabala aliacha wake wawili Joyce na Petronella Mwamba Mulenga na watoto sita, watano kutoka kwa Joyce na mmoja kutoka kwa Petronella (jina la mtoto huyo wa kiume ni Kalasa Efford David Chabala).
TUZO ALIZOTWAA:
Kombe la Zambia (Kombe la Uhuru/Kombe la Mosi) mwaka 1988.
Kombe la Chalenji la Zambia (Kombe la Chalenji la Shell/Kombe la Chalenji la BP/ Kombe la BP la Nane Bora) 1984, 1986.
Kombe la Umoja na Mashujaa: 1985, 1987, 1988.
Kombe la Bingwa wa Mabingwa 1985, 1988, 1992.
Ngao ya Jamii: 1992, 1993.
TIMU YA TAIFA:
Kombe la Chalenji la CECAFA 1984.
Kombe la MPLA 1986.
Kombe la SADCC 1990.
TUZO BINAFSI:
Mwanamichezo bora wa mwaka wa Zambia1985.
Huyu ndiye Efford David Chabala, mlinda mlango wa zamani wa Kimataifa wa Mufulira Wanderers na timu ya Taifa ya Zambia.
Maka Patrick Mwasomola.