Sambaza....

Kumekuwa na hali ya kutoelewana kati ya mshambuliaji wa Yanga kutoka Congo , David Molinga pamoja na kocha msaidizi wa Yanga , Charles Boniphace Mkwasa. Kwa mujibu wa David Molinga ambaye amekiri kuwa anaonewa kwa kiasi kikubwa na kocha huyo tangu timu yao irudi mazoezini.

“Kocha ananiambia sina fitness , fitness gani wakati wachezaji walikuwa ndani muda mrefu , kocha ameniambia nimeongezeka kilo 12 kitu ambacho ni uongo , jina langu analikata bila sababu”- alilalamika mshambuliaji huyo wa Yanga.

Alipoulizwa kwanini alipoitwa na meneja wa timu ili wakakutane na kocha Charles Boniphace Mkwasa , David Molinga alidai kuwa yeye ni mchezaji mkubwa ndani ya Yanga na ndiye anayeongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye kikosi cha Yanga kwa hiyo anatakiwa kuheshimiwa.

“Mimi ni mchezaji mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga , nimekuja Tanzania law ajili ya kucheza mpira wa miguu na ninaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye kikosi cha Yanga kwa hiyo natakiwa kuheshimiwa” alizidi kuongea mshambuliaji huyo ambaye anajulikana kwa jina la utani la Falcao.

David Molinga alizidi kusema kuwa Charles Boniphace Mkwasa hampendi ndiyo maana hata awali alikuwa anamwacha kwenye kikosi cha Yanga kabla ya kuja kocha mkuu wa Yanga kwa sasa Luc Eymael.

“Kabla hajaja kocha mkuu wa Yanga , Luc Eymael , Charles Boniphace Mkwasa alikuwa ananiacha sana na baada ya kuanza mazoezi tena Charles Boniphace Mkwasa anaendelea kuniacha , Mkwasa hanipendi mimi”- alimalizia mshambuliaji huyo aliyeletwa na Mwinyi Zahera.

Sambaza....