KAMA kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ataamua kumchezesha rasmi Jonas Mkude katika nafasi ya kiungo mlinzi na kumuanzisha nje Mghana, James Kotei katika mchezo wao wa Jumatano hii dhidi ya Mbabane Swallows FC, Simba SC haitapata matokeo katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika umri wa miaka 27 Mkude anapaswa kutambua kwamba ameingia sehemu ya pili katika maisha ya soka, hivyo anapaswa kujifunza kwa haraka kuwa ´hawezi kuufanyia mpira kila kitu´ anachojisikia, zaidi kwa nafasi yake anatakiwa kuichezesha timu na kupiga pasi kwa wakati mwafaka.
Kwenye mchezo uliopita wa ligi kuu Tanzania Bara vs Lipuli FC, Mkude alicheza kama kiungo wa kwanza wa ulinzi- nafasi ambayo amekuwa akipangwa Kotei na ni mara chache sana aligusa mpira akiwa robo ya tatu ya uwanja kutoka golini kwake kwenda eneo la Lipuli.
Na Kutokana na hilo mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania anatakiwa kufikiri upya kuhusu uchezaji wake huo. Alikuwa akicheza pasi nyingi za kurudi nyuma, alipiga pasi nyingi zisizofika, alipenda kukaa na mpira kwa sekunde nyingi hata wakati ambao alitakiwa kupiga pasi, na mchezo wake wa taratibu anapaswa kuachana nao.
Kotei amekuwa kiungo bora mlinzi katika kikosi cha Simba kwa msimu wa pili sasa, na wakati Erasto Nyoni akiwa na uwezo wa kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji kwa usahihi.
Kuna faida gani kuwa uwanjani na kiungo ambaye licha ya kushindwa kusogea katika eneo la hatari la wapinzani bado anapoteza mpira mara nyingi huku pasi zake nyingi zikiwa ´pasi mkaa?´
Mkude amekuwa akipiga sana chenga, lakini amekuwa akifanya hivyo akiwa katika maeneo ya hatari ya timu yake hivyo sitashangaa kama Swallows watanufaika na uchezaji wake huo siku ya kesho.
Hakufanya ´tackle´ hata moja katika mchezo dhidi ya Lipuli hivyo unaweza jiuliza mchezaji huo ana msaada gani kwa walinzi wake wa kati anapochezeshwa kama kiungo pekee wa ulinzi- alishindwa kuisukuma timu mbele, hakuwa makini katika kujilinda na alipoteza sana mpira.
Kama yupo mchezaji anayeweza kuzuia na kuanzisha mashambulizi, huku akilinda mpira na kupiga pasi zinazofika kwanini Aussems aendelee kumng´ang´ania Mkude? Mkude anajiona kama mchezaji aliyekamilika, hakuna anayebisha hilo, lakini bado anapaswa kujifunza zaidi kutoka kwa Kotei.
Mchezo wa Mkude bado haujapevuka vizuri, ndiyo maana anaona ni jambo la kawaida kupiga chenga zisizo na faida, na hajali kupoteza umiliki wa mpira akiwa eneo lake la hatari.
Naona kuna ugumu kwa kocha Aussems kufanikiwa dhidi ya Swallows na hata katika ligi kuu kama atamfanya Mkude kuwa kiungo wake mlinzi pekee katika mechi, hasa wakati huo kiwango cha Kotei kikiwa juu ya Mkude.