Francisco José Rodrigues da Costa ‘Costinha’ huyu ndiye ‘mtu mwaminifu’ aliyetambulisha soka mbinu kali za kujilinda linaloambatana na ushindi kutoka kwa kocha Mreno, Jose Mourinho. Nani anasahau ‘usiku wa Costinha’ pale Old Trafford Machi 9, 2004?
Baada ya kuruhusu magoli manne katika michezo mitatu ya ugenini dhidi ya Partizan Bergade, Marseille na Real Madrid katika hatua ya makundi, Mourinho alikwenda Old Trafford kwa mara ya kwanza kama kocha akiwa mbele 2-1 dhidi Manchester United ya Sir Alex Ferguson.
Golikipa ‘gwiji’ katika soka la Ureno, Victor Baia, Paulo Ferreira katika beki ya kulia, Nuno Valente katika beki ya kushoto, Jorge Costa na Ricky Carvalho katika beki ya kati mbele yao kidogo alisimama ‘kiungo mlinzi’, Costinha na ‘ukuta’ huu wa watu sita licha ya kuruhusu goli la Paul Scholes dakika ya 32’ waliweza kuhimili vishindo, huku wakishambulia kwa nguvu kwa ‘nyakati maalamu’.
Naikumbuka sana mechi hiyo- kama shabiki wa Manchester United ama klabu nyingine yoyote ambaye aliitazama mechi hii ya hatua ya 16 bora. Awali sikuwa nimeitazama FC Porto na sikuwa nikiifuatilia kwa ukaribu klabu hiyo kubwa ya Ureno, na hata baada ya ushindi wao wa 2-1 pale Estadio Dragao niliamini United ilikuwa na kazi rahisi nyumbani-lakini mbinu za Jose zilimtambulisha vizuri katika soka.
Costinha alisawazisha dakika ya 90’ ya mchezo kwa kichwa cha kuparaza na United ikajikuta nje ya michuano. Jose ni kocha wa aina yake na nimekuwa nikivutiwa na mbinu zake za kujilinda na kushambulia.
Ingawa miaka ya karibuni amekuwa akipata shida katika kazi yake, huku akishutumiwa mara kadhaa kuongoza soka lisilo na mvuto, kila nikiikumbuka ‘muunganiko’ wa viungo Deco ( Mbrazil kiasili licha ya kwamba alianza kuichezea Ureno miezi mitatu baadae baada ya kiwango bab-kubwa Old Trafford’, Pedro Mendez ‘mtaalamu wa pasi na mikwaju ya mbali’, sambamba na Maniche ‘fundi mpira’ ambaye alikuwa na uwezo wa juu katika kutengeneza nafasi za kufunga na kufunga kwa kiki za mbali.
Kama ulipata kuwaona viungo hao watatu niliowataja-Deco, Mendes, na Maniche utaelewa ni kwanini Mourinho ana kipaji cha kutengeneza timu yoyote anayohitaji kama atapewa ‘uaminifu’. Ukiitazama Porto yake ilikuwa na mbinu nyingi za kulinda lakini bado waliweza kushambulia vizuri na kufunga magoli muhimu.
JONAS MKUDE…..
Mara baada ya kuondolewa katika kikosi cha timu ya TAIFA YA Tanzania ‘Taifa Stars’ siku ya jana, nilipata kuzungumza na kiungo-mshambulizi wa zamani wa Polisi Morogoro na timu ya Taifa ya Tanzania ambaye kwa sasa yupo Morogoro na aliniambia; alitaraji kuona Mkude akitemwa katika kikosi cha Stars kilichoelekea Misri Ijumaa hii.
Sehemu ya maelezo yake hayo alisema, “ Namtazama Mkude kama mchezaji asiyejitambua kwa sababu amekuwa akizurura tu hapa Morogoro wakati aliomba ruhusa kuwa ana matatizo ya kifamilia.” Hii ni sehemu tu ya maelezo yake na kwa kweli kwa mwenendo wa kijana huyo mwenye miaka 26 bila shaka ana kazi kubwa ya kufanya kama kweli anajhitaji kucheza soka la kiwango cha juu nje ya klabu yake ya sasa-Simba SC.
Inawezekana kocha wa Stars, Emmanuel Amunike amemuondoa mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo kutokana na kutokuwepo katika kambi ya Dar es Salaam, lakini kwa kipindi cha miezi sita aliyopo Tanzania, Amunike kama kocha anayehitaji kupata matokeo mazuri hakuvutiwa na mbinu za kiuchezaji za Mkude.
Mkude ni staa wa Simba lakini katika kipindi cha miaka saba sasa ameshindwa kuwa sehemu ya vikosi vya Stars hata chini ya Kim Poulsen, Martin Nooj, Charles Mkwassa, Salum Mayanga na Amunike pia ameendelea kumtosa katika kikosi chake. Naamini sababu kubwa inayomuangusha ni aina yake ya uchezaji.
Kwa nafasi anayocheza Mkude anapaswa kuwa ‘mwaminifu’ –kwa maana ya kuzishika mbinu anazopewa na maelekezo ya namna anavyotakiwa kucheza. Mkude amekuwa na makosa mengi binafsi kiuchezaji- pasi zake nyingi hazifiki kwa mlengwa, ana piga chenga zisizo na uhakika na kupoteza mipira katika eneo ambalo wapinzani hutumia kutengeneza magoli yao.
Kocha wowote hupendelea kukabidhi mbinu zake kwa mchezaji mwaminifu kama Mourihno alivyofanya kwa Costinha, Claude Makelele, Pepe na Estabian Cambiaso, lakini ni kocha gani anayeweza kumpa mbinu zake za siri Mkude ili kuibeba timu mchezoni wakati mchezaji huyo amekuwa akikosea mara nyingi uwanjani.
Siwezi kumlaumu Amunike katika suala hili la kumuacha Mkude Zaidi mchezaji mwenyewe anapaswa kujipambanua zaidi kimbinu, kiakili na kiuchezaji. Kwa mchezaji aliyecheza mchezo wake wa kwanza wa kimataifa akiwa U20 Februari 23, 2012 kucheza michezo 17 tu Stars katika kipindi cha miaka saba huku akiwa katika kikosi cha kwanza cha klabu kubwa kama Simba ni ‘aibu’ Mkude anapaswa kubadilika, bado ni kijana mdogo, ana kipaji kikubwa cha soka lakini kiuwajibikaji bado ana safari ndefu katika mchezo wake.
Usikivu wa Costinha na utayari wake wa kubeba mbinu zote za Mourinho ndio sababu ya mafanikio ya FC Porto mwaka 2004, hivyo ni funzo pia kwa wachezaji wetu pia-kama Mkude ambaye ni bonge la kiungo-mlinzi kama atajibiidisha na kurekebisha pasi zake, ukabaji na uwezo wa kubeba mbinu za mwalimu wake.
Alishindwa kucheza Stars ya Kim, Noorj, Mkwassa, Mayanga na sasa Amunike kutokana na ukweli hawezi kubeba majukumu ya kimbinu ambayo makocha hao wanahitaji kumpatia kiungo namba sita kama yeye. Kwa aina ya uchezaji wake hawezi kucheza nje ya klabu yake ya sasa Simba labda kwa timu zisizo na malengo makubwa.
Tumlaumu Mkude mwenyewe kwa kushindwa kwenda CAN 2019 nchini Misri si Amunike kwa sababu hata Jose Mourinho angemtema katika kikosi chake kwa sababu si ‘mchezaji mwaminifu’ ambaye unaweza kumpa mbinu zako na kuijenga timu kupita yeye.