Sambaza....

Kabla ya fainali za kombe la dunia 2002 huko Korea na Japan jina Ronaldinho halikuwa maarufu miongoni mwa wafuatiliaji wengi wa soka duniani. Hata kushiriki kwake katika michuano hiyo ilikuwa ni bahati ya mtende baada ya staa wa Brazil, Romario kukataa wito wa kocha Felipe Scolari kujiunga na kikosi hicho. Hivyo ilimlazimu Scolari kumwita Ronaldinho kwa jina la utani Gaucho azibe pengo hilo.

Wabrazil wengi hawakukubaliana na kocha wao na hata wengine wakamtishia kuwa asipobeba kombe basi asirudi Brazil. Hayo yote yalitokana na Romario kugomea kuitumikia nchi yake kwa sababu ambazo hazipo sana wazi.

Ronaldinho Gaucho

Binafsi kumuona Ronaldinho akitakata ilikuwa katika mechi ya robo fainali ya kombe la dunia 2002 dhidi ya wazee wa maneno mengi England, ambapo Gaucho alipiga bao la ushindi katika ushindi wa 2-1 kwa freekick maridadi iliyomshinda kipa David Seaman.

Kwa bahati nzuri Brazil ilifanikiwa kuchukua kombe huku Ronaldinho akiwa miongoni mwa wachezaji muhimu kwenye timu. Pamoja na kutoaminiwa kwa maamuzi yake Scolari alirudi nyumbani akiwa amebeb furaha ya Wabrazil.

Brazil baada ya kutwaa kombe la Dunia 2002.

Baada ya kumalizika kwa fainali za kombe la dunia Barcelona ilimsajili Gaucho akitokea klabu ya PSG na hapo ndio ukawa mwanzo wa dunia kufurahia mpira wenye kasi, ujuzi na madaha wa mtaalamu Ronaldinho.

Akiwa Barcelona alipata mafanikio makubwa kwa kubeba vikombe vingi ikiwemo la Champions League 2006 lakini pia alipata tuzo binafsi nyingi zikiwemo za mchezaji bora wa dunia 2005 na 2006.

Ronaldinho Gaucho (kushoto) akiwa na kocha wake Frank Rijkaard (kulia).

Chini ya kocha Frank Rijkaard mwisho wa Ronaldinho ndani ya Barcelona haukuwa mzuri. Taratibu alianza kukosa namba, fununu zikivuja kuwa haelewani na kocha.

Kwa nini ugomvi na Rijkaard? Ni baada ya Dinho kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Lindsay Rijkaard mtoto wa kocha.

Maji yalipokuwa ya shingo mwaka 2008 Ronaldinho alitimka Barcelona na kujiunga na miamba ya soka ya Italia Ac Milan. Huo ukawa mwanzo wa kupotea kwa fundi huyo wa mpira ambaye hajui kununa, muda wote anatabasamu iwe nje au ndani ya uwanja.

Na Henry Hamisi
Insta @ henry_the_massive

Sambaza....