Shirikisho la soka barani Afrika ‘CAF’ limeipa uwenyeji nchi ya Misri kuandaa michuano ya Mataifa Afrika kwa mwaka 2019.
CAF imeitangaza Misri kuchukua mahala pa Cameroon ambaye alipokonywa uwenyeji huo baada ya kugundulika kushindwa kufanya maandalizi, hasa baada ya nchi washiriki kuongezeka na kufikia 24.
Misri iliomba uwenyeji sambasamba na Afrika Kusini mara tu baada ya Cameroon kupokonywa lakini CAF wameona waipe uwenyeji Misri kuandaa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Misri imeandaa Mashindano hayo mara nne na kutwaa mara tatu, iliandaa mwaka 1959 na kutwaa ubingwa, mwaka 1974 ilishika nafasi ya tatu, wakati mwaka 1986 na 2006 pia ilifanikiwa kutwaa ubingwa.
Mpaka
sasa jumla ya timu 14 zimekwishafuzu kushiriki michuano hiyo ya mwaka huu, Huku
Tanzania wakiwa na nafasi ya kufuzu kama watashinda katika mchezo wao wa mwisho
dhidi ya Uganda huku wakiombea matokeo ya sare ama ushindi kwa Cape Verde dhidi
ya Lesotho.