Endelea kusoma sehemu hii ya tano ya mfululizo wa makala ya ‘Mh. Mwakyembe, Winners take control’
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2018 Makocha wa Timu za Ligi kuu uingereza walianza kuona ubora wa wachezaji wazawa wa kiingereza na asilimia 91 ya wachezaji wa EPL waliokuwa na umri chini ya miaka 23 walikuwa ni waingereza kama Rahim Sterling, wa Man City, Trent Alexander-Arnold wa Liverpool, Marcus Rashford wa Manchester United ambao wote kwa pamoja na Tom Davies wa Everton walikuwa ni sehemu ya Kikosi cha timu ya Taifa ya Uingereza iliyo chini ya Kocha Gareth Southgate.
Ukiachana mradi wa St. Georges Park, mnamo mwaka 2012 Ligi kuu ya Uingereza EPL ilianzisha program ya wachezaji wasomi na kufanya vizuri program iliyopewa jina la Elite Player Performance Program (EPPP) wakiwa na lengo la kuzalisha na kuendeleza wachezaji bora wazawa anasema Mkuu wa Ligi kuu soka la vijana Bwana Neil Saunders huu ni sawa na mfumo wa Wajerumani wa kuwekeza kwa nguvu zote kwenye taaluma ndani ya shule zao za michezo“hiyo inamaanisha uboreshaji wa vifaa vya mafunzo, walimu na makocha bora wa kudumu, mafunzo ya wachezaji ili wachezaji wachanganye mpira wa miguu na elimu.” Hii ni sawa na Nukuu ya gwiji la soka Uholanzi Johanny Cruijff aliyepata kusema “Soka ni mchezo unaochezwa kwa kutumia kichwa” Cruijff hakumainisha kwamba mpira unachezwa kwa kupigwa na kichwa tu la hasha bali mpira unachezwa kwa kutumia akili hivyo alitaka wachezaji kuendelezwa katika Elimu ya Darasani na uwanjani, hapa ndipo walipatikana wachezaji wasomi kama Ruud Gullit, Dennis Bergkamp, Tostao, Socrates, Osvardo Ardiles, Jorge Valdano, Josep “Pep” Guardiola, Fernado Redondo, Ricardo Leite Izecson Kaka kitu ambacho hakikuwepo kwa Waingereza kwa vijana wao kuacha shule wakiwa na miaka 16 wakidai walichagua mpira zaidi, tatizo ambalo Tanzania ni kubwa kupindukia kwa wachezaji wengi vijana kusema waliacha shule kwasababu waliupenda sana mpira niaje uje kuwa na wachezaji bora wakati hawajui umuhimu wa elimu ilhali mpira ni mchezo unaochezwa kwa kutumia akili?
Tamaa yangu nilikuwa ni kuonesha namna gani wale watu ambao tumekuwa tukiiga kwao walivyoamua kutuacha kwenye mataa na sisi kuendelea kubaki kung’ang’ana na mitazamo yao ya miaka 20 iliyopita, unajua kwanini Waingereza wameamua kuachana na wimbo huo uliowashinda kuupa tiba? Jibu ni moja tu Mpira ni biashara na kitu kibaya juu ya biashara hii kwamba matokeo chanya ya uwanjani pekee ndio yanayosababisha timu ipate faida sasa unafikiri nani yupo tayari kupoteza wachezaji mahiri kisa tu sio wazawa? Wachezaji mahiri ndio wanaosababisha washabiki ambao ndio wateja wa vilabu kwenda kujaza viwanja pindi mechi za timu zao zinapocheza, wachezaji mahiri ndio wanasababisha vifaa vya timu vinunuliwe sokoni na kuongeza mapato kwa timu zinazowamiliki, wachezaji mahiri ndio wanaoiuza timu kwa gharama ya juu sana kwenye kupata haki ya matangazo ya TV, wachezaji mahiri pekee ndio wanaotumika kama nembo ya mchezo huu maridhawa haijalishi wanatokea kusini ama kaskazini mashariki mwa Dunia, hivi washauri wa Waziri mnakwama wapi?
Leo hii waingereza wamejikita pale St. Georges Park kutengeneza wachezaji mahiri sana, vivyo hivyo Vilabu vikubwa vimeendelea kupambana kutengeneza wachezaji mahiri na wasomi pia, Marcus Rashford baada ya kutoka kuifunga goli mbili Arsenal FC ikiwa ndio mechi yake ya kwanza kabisa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza siku ya jumapili tarehe 28/2/2016 na jumatatu tarehe 29/2/2016 alikuwa anatakiwa kwenda kufanya mtihani wa Chemistry huko shuleni kwake Jijini Manchester, hii inakuonesha namna gani mpira na wachezaji wake wanavyopaswa kutengenezwa, Manchester City ikiwa ndio iliowatengeneza wachezaji vijana kama Jadon Sancho anaetamba sasa akiwa BvB pale Ujerumani akitajwa kuwa mchezaji bora zaidi kwa vijana kwa sasaa, Phil Foden mchezaji bora wa Kombe la Dunia U17 ambalo waingereza walibeba wakiifunga Hispania katika fainali na wengine wengi, Arsenal FC wana akina Bukayo Saka, Eddie Nketiah, Reiss Nelson na wengineo, Liverpool wana vijana wa aina ya Rhian Brewster, Curtis Jones, haravey Elliot, huku Everton FC wakiongozwa na kijana wake Dominic Calvert-Lewin, Mason Holgate, Anthony Gordon na wengineo, Chelsea FC wana vijana wengi zaidi wa kiingereza waliopata nafasi kucheza Ligi kwenye msimu huu wa 2019/20 wakiongozwa na Mshambuliaji Tammy Abraham, Mason Mount, Reece James, Billy Gilmourna wengineo wengi tu kama Callum Hodson Odoi, Aston Villa wana Jack Grealish, Leicester City yupo James Maddison, Watford yupo Todd Cantwell na huko Manchester United wapo Aaron Wan-Bissaka, Mason Greenwood kuwataja wachache tu na hao wote ni zao la mapinduzi ya soka la waingereza huku vijana hao wakiwa ni vinara kwenye Ligi kuu ya EPL wakisaidiwa na wachezaji wengi mahiri wa kigeni wanaocheza katika Ligi hiyo;hili liwe funzo kwetu pia.
Wakati timu iliyosheheni wachezaji wa Kigeni ya Arsenal FC ikiingiza washabiki elfu 60 kila wiki kwenye Dimba lao la Emirates kiwango kikubwa zaidi kwa vilabu vyote vya London hii ina maana kwamba Uingereza inaweza kuwa na Ligi Bora ama kuamua kuwa na Ligi ya Waingereza lakini hawawezi kuwa navyo vyote viwili kwa wakati mmoja kwamba ligi bora ya wachezaji wa kiingereza; basi ndivyo vivyo hivyo nionavyo kwenye Ligi ya Tanzania, ukizingatia Washabiki wanaenda kwenye mechi kuona mchezo utakaowakutanisha wachezaji bora ili wapate mchezo bora, na kwa maana hiyo timu kuwa na wachezaji bora ina maanisha ni kuwa na bidhaa bora katika msingi huu itakuwa na washabiki wengi wanaoifata na kuiunga mkono, kwa maana hawa washabiki ndio wateja wa timu na vilabu kwa ujumla wake, zingatie ile kitu tunaita TABIA YA MTEJA kama wasemavyo wasungu “Customer Behavior” kwamba mteja atakuwa tayari kununua bidhaa iliyo bora tu na si vinginevyo. Kuna mtu hapa ananiambia eti wao wameendelea sana kwenye nyenzo, tafiti, uwekezaji na hata miundo mbinu sisi hatuwezi kufanya walichofanya; nikacheka na kumuuliza kwahiyo tukifukuza wageni ndio tutaboresha hivyo vitu ambavyo hatuna?
Aliyekuwa makamu wa Rais na General Manager wa Barcelona kwa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2008 Ferran Sorrianokatika kitabu chake alichokiita GOAL: The ball doesn’t go in by chance anasema Biashara ya mpira ni biashara tofauti na biashara nyingine sababu hii inataka upate matokeo uwanjani, kama unapata matokeo ya ushindi basi unaonekana unapata faida na si vinginevyo, na ili upate matokeo na hayo matokeo yawe endelevu basi yataletwa na vitu vitatu (Kujitolea x Mizania)Talanta yaani Kujitolea zidisha kwa Mizania kwa root ya Talanta; kujitolea ni jambo unaloweza kulipata kwa mchezaji yoyote yule lakini Mizania ama Balance hii inahitaji jicho la mwalimu kwenye kung’amua mapungufu ya timu yake ila Talanta ni aidha mtu anazaliwa nayo na kuendelezwa ama mtu anajifunza na kuwa na utayari wa kupokea anachofunzwa kitu ambacho kimekuwa shida kubwa sana kupatikana nchini; hivyo kupelekea vilabu vingi sio vyetu tu kwenda nje ya nchi zao kutafuta Talanta ili tu kui square kwenye Kujitolea na Mizania.
Soma mfululizo wake....
Jadili na Mwandishi wa makala hii katika sehemu ya maoni….