Endelea kuisoma makala hii ya kuvutia kama maoni kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni Ligi Kuu.
Moja ya hoja ya Klabu ile kongwe ilikuwa ni kwamba kama katika Ligi ni timu mbili tu ndio zilikuwa na uwezo wa kusajili wachezaji hao 10 na wachezaji wengine 20 wakawa ni wazawa kutimiza kanuni ya kusajili wachezaji 30 kwa kila timu kwenye ligi ya timu 12 kipindi kile ina maana Ligi ilikuwa na jumla ya wachezaji 360 ambapo katika hao ni 20 tu ndio walikuwa wa kigeni, kabla ya ujio wa Azam FC kwenye Ligi kuu msimu wa mwaka 2008/09 hivyo huwezi kusema wachezaji 20 wanazuia vipaji vya wazawa, nieleweke vilabu vingine sio kwamba vilizuiwa kusajili la hasha TFF wakati huo iliweka kanuni kwamba mchezaji yoyote wa kigeni ili acheze basi alipaswa kulipiwa dola za kimarekani 2000 kama kibali hapa achilia mbali kibali kinachotolewa na Idara ya Uhamiaji kumruhusu mchezaji kufanya kazi (Kucheza mpira) nchini, kitu ambacho vilabu vingi vilishindwa isipokuwa Simba SC na Yanga SC na baadae AzamFC TFF ikaona hizi zilikuwa ni hoja za msingi japo kulikuwa na misuguano ya hapa na pale hivyo ikaruhusu vilabu vile viwili viendelee na sajili za wachezaji wa kigeni kufikia ukomo wa wachezaji 10.
Kwanza kabisa naomba nichague upande na hata wewe msomaji wangu upate kuelewa msimamo wangu, mimi naamini wachezaji 10 ni wachache sana kusema eti “wanaua vipaji vya wachezaji wazawa” na hili ni hata kama vilabu vyote ishirini vingeweza kusajili hao wachezaji 10 bado ningeweza kupinga ujio wa wachezaji hao sio “kifo cha vipaji vya wachezaji wazawa”, na hili naweza kulithibitisha beyond the reasonable doubt, kimahesabu ligi yetu ina timu 20 kwa maana hii kama zote zimesajili wachezaji 30 maana yake ligi kuu pekee ina wachezaji 600 katika wachezaji hao 600 ni Simba SC, Yanga SC na Azam FC ndizo zenye wachezaji zaidi wa kigeni hii ina maanisha kwa ujumla wana wachezaji 30. Simba (9), Yanga (8), Azam FC (6+), Namungo FC (1), Kinondoni Municipal Council FC (6) Alliance FC ina mchezaji 1, Biashara United Mara FC ina mchezaji 1, Mwadui FC (1), Mbeya City (1) hii itoshe kutupa uhalisia wa mahala tulipo kwa kifupi wachezaji wa kigeni kwenye timu zetu za ligi kuu wanafika ama wanakaribia 60 tu hii ina maana wageni kwenye ligi ni asilimia 10 tu huku wazawa wakiwa wamebeba asilimia 90 ya wachezaji wote wa Ligi kuu inachekesha sana!
Hichi kinachotokea sasa hivi hapa nyumbani ni sehemu ya kilichowahi kutokea miaka ishirini iliyopita pale Uingereza, wanaandika Simon Kuper na Stefan Szymanski katika kitabu Soccernomicskilichochapishwa mwaka (2009) wakiuliza “kwanini Uingereza inashindwa? Kwanini Brazili na Ujerumani wanashinda? Kwanini Marekani, Japani, Australia, Uturukina hata Iraq wanaelekea kuwa Wafalme wa mchezo unaopendwa zaidi Duniani?” Taifa la Uingereza wao wakiwa waasisi wa mchezo huu maridhawa kama ulivoitwa na Mfalme wa Soka Duniani Edson Arantse do Nascimento Pele, wamekuwa wakitafuta sababu zilizo nje na wao mara zote wanapofeli walipofungwa na Croatia pale uwanja wao wa taifa Wembley na kushindwa kufuzu kwa mashindano ya Mataifa ya ulaya mwaka 2008 wachambuzi wengi wa soka walisema sababu ya kutolewa kwao ni kwamba “Ligi yao imejaa wageni” hivyo kupelekea timu yao ya Taifa kukosa wachezaji mahiri huku vilabu vyao vikiwa vimejaza wachezaji wengi mahiri kutoka nje.
Akihojiwa kabla ya Uingereza kutolewa na Croatia kiungo wa timu ya taifa ya Uingereza na Liverpool wakati huo Steven Gerard alisema “I think there is a risk of too many foreign players coming over, which would affect our national team eventually if it is not already.It is important we keep on producing players.” Hii ina maana Gerard nae aliingia kwenye mtego wa Wachambuzi wale waliokuwa wanaona wageni wanatumika kuua vipaji vya waingereza kupelekea timu yao ya taifa kufanya vibaya; kwa haraka haraka nikapiga hesabu kwamba Je hapo kabla Uingereza na timu yao ya taifa walikuwa na mafanikio makubwa kiasi gani? Nikakumbuka mafanikio pekee makubwa zaidi ni kutwaa Ubingwa wa Dunia mara moja tum waka 1966 baada ya hapo wamekuwa wasindikizaji tu hii inatosha kusema kwamba kukwama kwa waingereza sio suala la wachezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa wa mtandao wa CIES Football Observatory kati ya mwaka 2009 hadi 2017 asilimia 23.6 ya wachezaji wanaocheza Ligi kuu ya Hispania walikuwa ni wazawa, wakati kwenye ligi kuu ya Ufaransa wazawa walikuwa ni asilimia 23.2, huku ligi kuu ya Ujermani ikiwa na asilimia 15.1 ya wazawa na Uingereza wakiwa ni asilimia 14.1 kwa kutazama taarifa hizo inaonesha namna gani ligi kubwa Duniani kote zilivyofurika wachezaji wageni na licha kuwa na wageni wengi kwnye ligi kuu zao Hispania alikuwa Bingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2010, Ujerumani Bingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2014 na Ufaransa bingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018 hii itoshe kutuonesha kuwa kuna sababu zaidi ya wachezaji wa kigeni katika nchi kutopata mafanikio ngazi ya timu ya taifa.
Baada ya Uingereza kutolewa na Croatia Rais wa FIFA wakati huo Sepp Blatter, Kocha wa Machester United FC wakati huo Sir Alex Ferguson na Rais wa UEFA wakati huo Michel Platini katika kusisitizia juu ya kauli ya Steven Gerrard walisisitiza kukosekana kwa vipaji Uingereza kumepelekea timu kwenda kusaka vipaji nje ya uingereza, Platini muumini mkubwa wa wachezaji wazawa kucheza kwenye timu zao za asili ili tu kudumisha asili ya mahala husika alijikuta anashindwa kuvishawishi vilabu kama Liverpool na Manchester United kukubaliana na hoja yake kwasababu; kama wachezaji wa kiingereza wenye vipaji dhaifu wangepewa nafasi kwenye vilabu vile vikubwa vya aina ya Manchester united, Liverpool, Arsenal, Manchester City, Tottenham Hotspurs ina maana wasingekuwa na uwezo wa kuongeza uwezo wao, hata kuwa sehemu ya kutajwa kama wachezaji bora alikadharika vilabu husika vingeshindwa kushindana na vilabu vingine vya nje ya uingereza kwenye mashindano makubwa barani Ulaya.
Soma mfululizo wake
Jadili na Mwandishi wa makala hii katika sehemu ya maoni….