Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba wameshindwa kutakata mbele ya Wauawaji wa Kusini Namungo Fc kwa kuambulia sare ya bao moja kwa moja katika Dimba la Majaliwa Ruhangwa Lindi.

Katika mchezo huo uliokua na kasi ya kawaida Simba ndio waliokua wakwanza kupata bao katika dakika ya 28 kupitia Jean Baleke akiunganisha krosi safi ya Saidoo iliyotokana na mpira wa adhabu. Kwa goli hilo sasa Baleke anafikisha mabao nane wakati Saido yeye anafikisha pasi ya kumi ya goli.

Kabla ya mpira kwenda mapumziko Namungo walichomoa bao hilo dakika ya 38 kupitia kwa Salum Kabunda aliyenufaika na makosa ya Ally Salim kwa kushindwa kuuokoa mpira wa kona vyema uliopigwa na Shiza Kichuya.

Baada ya mchezo huo kocha Juma Mgunda alisema “Mchezo dhidi ya Namungo umemalizika tumepata sare, tunarudi uwanja wa mazoezi kujiandaa na mechi zilizosalia. Sisi hatuangalii nani kafanya nini tunahitaji kushinda mechi zetu zote.”

“Tulijua isingekuwa mechi rahisi, Namungo ni timu nzuri hasa inapokuwa nyumbani lakini mpira una matokeo matatu tunarudi kujipanga kwa mechi zilizo mbele yetu,” alimalizia Mgunda.

Katika hatua nyingine mlinda mlango namba tatu wa Simba Ally Salim ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi ya klabu ya Simba akiwazidi Jean Baleke na Kibu Denia alioingia nao fainali.

Kwa kushinda tuzo hiyo inayotolewa kwa kupigiwa kura na mashabiki Ally Salim amejinyakulia kiasi cha milioni mbili pamoja na tuzo kama zawadi baada ya kuibuka kinara.

Simba sasa wanaelekea mkoani Mtwara katika mchezo wa nusu fainali wa kombe la FA dhidi ya Azam Fc utakaopigwa katika Dimba la Nang’wanda Sijaona.

Sambaza....