Eric Ten Hag amekuwa Kocha wa 7 tangu kuondoka kwa aliyekuwa Kocha kipenzi na mwenye mafanikio makubwa ndani ya United Alex Ferguson mwaka 2013.
Tangu hapo tukashuhudia bandika bandua ya makocha kana kwamba United ni kichwa cha ‘mwendawazimu ‘ kila moja anakuja kujifunzia kunyoa.
Alianza David Moyes ambaye pia hakudumu kisha akafuati Mdachi mwenye uwezo mkubwa Luis van Gaal naye hadithi ikabaki ileile, akaja Special one Jose Mourinho kana kwamba aitoshi akampisha kijana wa nyumbani mwenye DNA aliyelelewa kwenye filosofi ya klabu hiyo Ole Gunnar Solskajer hawakufua dafu.
Baadaye akapewa kiungo mkabaji wa siku za nyuma wa mashetani hao Michael Carrick naye hakuaminika kupewa kandarasi iliyonyoka mwisho wa siku akaletwa Mwalimu wa walimu ( mkufunzi) Ralf Rangnick na sasa ni huyu Erik Ten Hag.
Ten Hag anatoka kwenye timu ya Ajax, binafsi namuona kaja muda mbaya sana hivyo lazima malengo ya timu yabadilike.
Awali United baada ya mtikisiko huu tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson nia ya kwanza ya timu ilikiwa ni kuchukua ubingwa kwa mara nyingine nje ya utawala wa mzee huyo kwenye benchi la ufundi.
Lakini mara nyingi timu ilikuwa ina uhakika kwenye ushiriki wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, tofauti na sasa ambapo Ten Hag anakuja kuikuta timu haipo kwenye Ligi ya Mabingwa bali wapo Europa league kitu ambacho sio mpango wa timu na wadhamini wake.
Hapo ndipo unaanza kuona ugumu kwenye kazi ya Ten Hag hasa kipaumbele ambacho waajiri wanataka na hata mashabiki.
Ki ukweli ni vigumu kwa United ya sasa kubadili upepo ghafla na kwenda kuwa mabingwa kwenye msimu ujao lakini wanaweza kuanza kuirudisha timu kwenye Ligi ya Mabingwa kwa maana ya kurudi ndani ya nne bora li wapate tiketi ya kushiriki.
Miye binafsi nina mashaka na Ten Hag kufanikiwa kwa haraka kwa kuwa mara nyingi walimu au makocha wanaotoka kufundisha timu zenye muonekano wa ki academy kama ilivyo Ajax huchelewa kubadilisha akili kwenye ushindani wa wakati uliopo.
Muda mwingi atataka kusajili na wachezaji vijana zaidi akiwa na imani ya kupata na kufanya vizuri kwenye mipango ya baadae tofauti na kiu ya ubingwa walionao mashabiki wa United.
Baada ya msimu ujao United atakuwa anatimiza miaka 10 tangu kutwaa ubingwa wake wa mwisho wakiwa na mstaafu Sir Alex Ferguson.