MEDDIE Kagere alifunga goli lake la 12 tangu aliposainiwa Simba SC Julai iliyopita. Alifungamagoli manne na kuisaidia Simba kufika fainali ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, tayari amefunga magoli saba katika ligi kuu Tanzania Bara, na goli lake la 12 dhidi ya Mbabane Swallows FC jana jioni katika ligi ya mabingwa Afrika limemfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kufunga katika kila michuano ndani ya dakika 90 katika kila mchezo wake wa kwanza.
FUNZO
Wakati muda ‘ukiyoyoma’ na matokeo yakiwa 2-1, Swallows walianza kupoteza muda kwa kuamini itakuwa rahisi kuwaondoa mabingwa wa Tanzania Bara huku Mbabane Disemba 5 na Simba walikuwa wakipambana kutafuta goli/magoli zaidi kwa kuamini ushindi wa 2-1 nyumbani ulikuwa hautoshi.
Swallows walikuwa imara, walicheza kwa nidhamu na kujiamini hadi pale golikipa wao alipofanya kosa ‘la mwaka’ baada ya kuteleza na kupoteza mpira ambao haukuoneka kuwa na madhara dakika ya 85.
Kama ilivyo kwa washambuliaji wengi waliokamilika, Meddie aliamua kuufuatilia mpira ambao mlinzi wa kati wa Swallows aliurudisha kwa golikipa wake.
Wiki mbili zilizopita nilikuwa nikitazama luninga ya Manchester United ambayo walikuwa wakionyesha magoli yote ya mshambulizi Marcus Rashford tangu alipopandishwa kikosi cha wakubwa.
Katika magoli yake 33, Rashford alifunga magoli kati ya matatu hadi matano ambayo unaweza kusema yalitokana na makosa ya magolikipa, lakini kwa jicho la tatu, Rashford alifanikiwa kufunga Kutokana na tabia yake ya kufuatilia mpira- hasa ile ambayo walinzi wa timu pinzani hurudisha kwa golikipa.
Unajua kitu ambacho wengi hawafahamu katika mchezo wa soka magolikipa wengi hujiamini wakati wanapotumia mikono, na ni wachache sana wanaoweza kujiamini wakati mpira unaopokuwa katika eneo lao na hawaruhusiwi kuucheza kwa mikono.
Kama washambuliaji wengi wa Tanzania wataamua kucheza kwa kukimbiza pasi za kurudi nyuma ambazo wapinzani wao hucheza na magolikipa watanufaika mno kwa sababu magolikipa hupoteza kujiamini wanapozongwa na huku wakikosa uhuru wa kutumia mikono yao.
Goli la Kagere vs Swallows halivutii lakini ni funzo ambalo linapaswa kuchukuliwa na washambuliaji wa Tanzania. Wanatakiwa kuamini magolikipa wengi si mahiri katika matumizi ya miguu hivyo ni rahisi kwao kupoteza kujiamini wakati anapokabiliwa na mshambulizi.
Kufuatilia mpira unaorudishwa nyuma kunaweza kumfanya golikipa akapoteza kujiamini na kikawaida inapokuwa hivyo, mchezaji hufanya makosa na Meddie kama mchezaji wa kimataifa na mwenye uzoefu alifanikiwa kuifungia timu yake goli muhimu ambalo liliwapoteza kabisa Swallows.