Mshambuliaji kinara wa Simba Meddie Kagere leo amepokea mvinyo pamoja na jozi moja ya viatu yenye jina lake kutoka kwa Tovuti ya Kandanda.co.tz kama ilivyo ada kwa tovuti hiyo kusheherekea na Galacha wa mabao kila mwezi.
Meddie Kagere aliibuka Galacha wa mabao kwa mwezi wa tatu baada ya kufunga mabao matano na hivyo kuwa mshindi wa mwezi March. Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona ilisababisha tovuti ya Kandanda kuchelewa kukabidhi tuzo hiyo na hivyo kupelekea tuzo ya mwezi March kukabidhiwa kwa mshindi mwezi huu wa Julai.
Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Meddie alikua na haya ya kusema “Kwangu mimi ninajua kwamba siri ya mafanikio (kufunga mabao) ni Mungu kwani nimekuwa nikimuomba kila wakati na mimi pia ninaongeza juhudi katika kazi yangu.
Ushirikiano ambao ninapewa na wachezaji wenzangu unanifanya ninakuwa katika kiwango ambacho nipo nacho kwa sasa na wakati ujao pia” Alimalizia Kagere ambae ndio mfungaji bora wa Simba na Ligi Kuu Bara mpaka sasa.
Meddie Kagere ameibuka kinara wa Galacha wa mabao mara mbili katika msimu huu baada ya kufanya hivyo mwezi wa nane na kukabidhiwa pia mvinyo na jozi ya kiatu ili kuweza kusheherekea katika ufungaji wa mabao.
Mpaka sasa katika chati ya ufungaji mabao Meddie Kagere anashika usukani akiwa na mabao 22 huku michezo miwili ikiwa imesalia. Anaemfawatia ni Yusuph Mhilu wa Kagera (mabao 12) na Leriant Lusajo wa Namungo mwenye mabao 12 pia.
Kwa upande wa Kandanda Afisa masoko wa tovuti Thomas Mselemu hakusita kuishukuru Mgahawa Cafe&Restaurant ambao ndio wadhamini wakuu wa tunzo hii tangu mwanzoni mwa msimu.
Thomas Mselemu “Tunawashukuru Mgahawa Cafe&Restaurant kwa kuwa pamoja nasi tangu mwanzo wa msimu mpaka sasa, wametuwezesha sisi (tovuti) kuweza kusheherekea vyema na Galacha wa mabao katika Ligi yetu. Ni kitu kikubwa kwetu tunaamini tutaendelea nao pia msimu ujao.”