Sambaza....

BAADA ya kucheza michezo tisa kati ya 38 wanayotakiwa kucheza msimu huu katika ligi kuu Tanzania, timu ya Ndanda FC ya Mktwara imekuwa klabu ya kwanza kushindwa kusafiri kutokana na ‘ukata’. Ndanda baada ya kuchapwa 3-1 na Singida United katika mchezo uliopita walishindwa kuomndoka mjini Singida kutokana na sababu za kiuchumi.

Hii inamaanisha ukosefu wa wadhamini wakuu wa ligi msimu huu ni tatizo kubwa ambalo litapelekea kupunguza msisimko na ubora unaotakiwa na watu wengi wa mpira. Ndanda FC haina mdhamini kama klabu, na kwa misimu yote minne wanayocheza ligi kuu hata wakati wa udhamini wa Vodacom-timu hiyo ya Mtwara imekuwa ni kati ya klabu zenye kusumbuliwa mno na ukata.

Kuna wakati, Toto Africans kabla haijashuka katika ligi za chini, JKT Mgambo kabla nayo haijaremka daraja, Africans Spotrs, Majimaji FC, Stand United ni baadhi ya timu ambazo licha ya kuzalisha wachezaji wengi wazuri katika ligi kuu Tanzania Bara, klabu hizo zimeteremka daraja kutokana na ukosefu wa pesa.

African Lyon imekuwa ikipanda na kushuka daraja nayo pia ni ‘klabu ukata’ hii imepelekea kwa kiasi kikubwa ligi kushindwa kuwa bora. Leo hii Ndanda bado wana michezo 29 wanayotakiwa kucheza siku zijazo lakini tayari wanashindwa kusafiri kurejea kwao Mtwara kutoka Singida kutokana na ukosefu wa pesa.

Tunaweza kuwalaumu viongozi wa klabu kushindwa kutafuta wadhamini au wafadhili wanaoweza kuwasaidia kumudu gharama za uendeshaji timu lakini kwa kiasi kikubwa tunapaswa kulitupia lawama Shirikisho la soka katika hili kutokana na ‘mipango yao ya zimamoto’

Uongozi huu wa rais wa TFF, Wallace Karia uliamua kuongoza timu nne kutoka 16 hadi 20 katika ligi kuu bila kufanya athimini wala kuwashikirikisha wadhamini waliokuwa katika maongezi nao ya kuongeza mkataba. Kuwa na timu 20 si vibaya, lakini kuna kuwa na athari nyingi kiuendeshaji hasa pale unapokosa kabisa msaada kutoka kwa wadhamini au wafadhili.

Kilio hiki cha Ndanda FC ligi ikiwa ‘changa’ kabisa ni mwanzo tu way ale ambayo tulisema awali kuwa TFF ilikuwa ikifanya makosa na huenda ikazalishwa ligi mbovu isiyo na ushindani wa kweli kutokana na klabu nyingi kushindwa kujiendesha hata wakati ule ligi ikiwa na timu 16 na udhamini juu.

Ndanda wameanza kukwama na kulia kwa mkuu wa Mkoa Mtwara awasaidie, unadhani ofisi ya mkuu wa mkoa kila mara itakuwa na uwezo wa kufanya hivyo? Kama siku ikishindwa nini hatma yake? Je, TFF itaishusha daraja Ndanda FC siku ikishindwa kufika uwanjani kucheza kutokana na ukata?

Ili tupate mwanga wa ligi bora, TFF inapaswa kupigana kufa na kupona kuhakikisha wanapata udhamini wa ligi kuu vinginevyo, kilio hiki cha Ndanda FC kitaanza kusambaa kwa klabu nyingine na hilo litakuwa jambo la hatari kwa ligi.

Sambaza....