Sambaza....

Watanzania kama ilivyo kwa mamilioni ya Watu duniani, ni wadau na wapenzi wakubwa wa mpira wa miguu. Kwa mapenzi yao hayo ndio hasa kisa cha hata kutofautiana kimtazamo na hata maono juu ya timu ipi ya kushangilia bila kujali inatoka ligi gani duniani.

Lakini bila kupepesa macho ligi yenye ushindani zaidi duniani ni ligi ya Uingereza yaani EPL. Ubora wa ligi hii haukuja tu kwa kulala na kuamka bali ni juhudi za watendaji na wasimamizi wa soka nchini humo katika kuhakikisha wanaweka mipango endelevu na yenye kutekelezeka.

Ukitaja sababu za umaarufu wa ligi ya Uingereza, hutoona aibu kuweka sababu kama ubora wa Miundombinu, Matangazo ya Televisheni, Ushindani wa timu, na uwekezaji. Lakini vyote hivi vinavutia matajiri kuwekeza kupitia timu mbalimbali na kuufanya mpira kuwa biashara yenye faida kubwa.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 600 wanaangalia ligi kuuya Uingereza kutoka zaidi ya nchi 200 kote duniani, lakini haya yote ni hatua kwani Uingereza wametumia zaidi ya miaka 30 kufikia hiki unachokiona sasa, ukilinganisha na miaka ya 1965 kipindi hicho BBC ikionyesha ligi hiyo kimawenge.

Watu walionyuma ya ligi hii wameifanya ligi kuwa bora, kiufupi wamefanikiwa kuifanya ligi hii kuwa kiungo fulani cha chakula. Kiungo ambacho ukikikosa wakati wa kula ni sawa na hakuna kitu. Ligi ipo bora kutoka hatua ya upangwaji ratiba, waamuzi, Luningani na hadi kwa wachezaji.

Uwekezaji na uweledi kwenye Ligi hiyo ndio matunda ya timu zao kufanya vizuri katika michuano ya Ulaya msimu ulioisha. Hebu tuangalie pesa inayotengenezwa katika Ligi hii kutoka kwa Wadhamini na Haki za Matangazo.

Mfano katika msimu wa mwaka 2017/2018, klabu nyingi za EPL zilijizolea mkwanja wa kutosha kutokana na haki za matangazo ya Televisheni. Kila klabu ilipata zaidi ya paundi milioni 34 kwa TV za ndani, zaidi ya paundi milioni 40 kwa TV za nje na Paundi Milioni 4 kutoka kwa wadhamini, kwa ujumla kila klabu ilipata zaidi ya Paundi Milioni 80, na hapo kuna haki za matangazo kwa baadhi ya mechi, kwa mikataba maalumu. Inakadiliwa kwa chini ya mechi 10, klabu zilijipatia zaidi ya Paundi milioni 12.

Yaani kwa mfano, klabu amabyo ilishika nafasi ya mwisho, yaani West Brom walijikusanyia jumla ya Paundi milioni 94.6 kwa msimu, huku klabu kubwa kama Man U ikijibebea kitita cha Paundi milioni 149.7. Kiujumla timu zote msimu huo ziligawana kiasi cha Paundi bilioni 2.42. Faida ilioje!

Turudi hapa kwetu, mara baada ya Ligi kumalizika wadau wengi walitoa maoni yao kuhusiana na mwenendo wa Ligi. Kubwa lilikuwa la mdhamini mkuu wa Ligi Kuu.

Ligi hadi inaisha haikuwa na mdhamini mkuu, pesa kubwa kwa kila timu ikionekana kuwa katika haki za matangazo ya Azam Tv.

Msimu wa mwaka 2017-18, ligi kuu ilikuwa ikidhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Kama Mdhamini Mkuu na ndio maana ilikuwa ikifahamika kama VPL yaani Vodacom Premier League.

Msimu huu hakukuwa na mdhamini kuu, Viongozi wa TFF, muda wote waliishia kutoa ahadi tu kwa  wadau wa soka nchini kwa kudai kuwa, mdhamini mkuu atapatikana muda si mrefu.

Lakini hadi Simba anakabidhiwa ubingwa , ligi imemalizika bila mdhamini mkuu. Athari ya hili ni timu nyingi kukosa japo fedha za kujikimu kwani Mdhamini mKuu alikuwa akizisaidia timu nyingi yakiwemo masuala ya vifaa na usafiri.

Udhamini wa Vodacom ulikuwa ni wa miaka mitatu na wenye thamani ya bilioni 6.6. kujitoa kwa Vodacom kulizifanya klabu kukosa milioni 80 zilizokuwa zinatolewa katika awamu nne yaani kila awamu ni milioni ishirini.

Udhamini huo pia uliambatana na zawadi za washindi wa ligi, ambao walipewa shilingi milioni 80.4, mshindi wa pili ,milioni 40.2, wa tatu 28.7, wan ne 22 na timu yenye nidhamu ilipata milioni 17.

Bila kusahau mchezaji bora na mfungaji bora kila mmoja alipewa shilingi milioni 5.7, kipa bora milioni 5, huku kocha na mwamuzi bora walipewa milioni 8.6 kila mmoja.

Ligi kuu inaangaliwa na mamilioni, Azam anategemea sana Ligi hii kufanya biashara zake. Licha ya faida mbadala kwa vilabu na wachezaji kuonekana mbali, lakini vilabu hivi vinahitaji pesa zaidi kutoka Azam Tv.

Timu zinapata 100,000,000 kwa mwaka kutoka Azam, ikiwa ni sawa na 2,631,579 kwa kila mechi. Hii ni pesa ndogo sana. Maanayake udhamini huu Azam inatoa 2B kwa msimu kwa timu zote kwaajili ya Kuonekana katika mechi zake. Mkataba kuhusu malipo haya upo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Utaratibu huu unaweza ukaangaliwa tena kwa kuangalia mfumo rafiki wa kuingiza mapato katika mechi za timu kwa mfumo pia wa timu mwenyeji na mgeni. Lakini si kwa kuzilipa zote kiwango kimoja cha pesa.

Mbadala wake, vilabu vitumie mwanya huu kumuweka mdhamini mkubwa kifuani ambaye ataonekana na mamilioni. Mfano, milioni 200 kwa mdhamini wa timu kifuani au hata 350 ni biashara nzuri kwa mwaka.

Mwisho wa siku, naweza sema, mdhamini mkuu wa ligi yetu lazima ajue ligi yetu inataka nini, lazima ajue ligi yetu ipo wapi nay eye anatakiwa aipeleke wapi na kwa wakati gani, lazima ajue asili, sifa na aina ya timu zilizopo  ili kujua ni jinsi gani anaweza tengeneza faida nzuri ya kumfanya arudi tena na tena.

Mdhamini lazima ajue kuwa, ndani ya ligi hii kuna vilabu ambavyo vitamtegemea kwa zaidi ya asilimia 90, yaani vilabu hivi havina mdhamini mwingine mbali na kutegemea udhamini wake. Maana vilabu vyetu vingi vinaendeshwa “kishikaji” kwelikweli yaani kama ni suala la kutia nembo tu kwenye jezi ni rahisi kama kumsukuma mlevi.

Mdhamini anatakiwa kujua ligi yetu ina jumla ya timu 20 hatutaki yatokee kama yaliyotokea maana wengi tumeyasahau na hata hatuyakumbuki. Mdhamini aheshimu mkataba wake na kuulinda pia nimkumbushe kuwa Uongozi wa shirikisho sio wa kudumu, huja na kuondoka.

Nani adhamini Ligi Yetu?

Ligi yetu imevutiwa na wachezaji wengi, na sasa ni bora zaidi kwakuwa inatoa timu nne katika michuano ya Afrika (Mbili Ligi ya Mabingwa na Mbili Kombe la Shirisho Afrika). Inahitaji mdhamini mkubwa mwenye uzoefu wa kufanya biashara kupitia Ligi hii, bila kusahau wadhamini wa vilabu vyote. Wadhamini wa vilabu wanauwezo wa kutangaza bidhaa zao Afrika nzima iwapo timu itafanya vizuri na kushiriki michuano ya Afrika.

Wapo wadhamini wengi ambao wametajwa kama tetesi za kutaka kuidhamini ligi hii. KCB, Azam, NBC, Sportpesa, DTB na NMB ni miongoni mwao. KCB na Azam tayari wanahusika na Ligi hii, Sportpesa na NMB pia ni wadhamini wa vilabu kadhaa na wanajihusisha na mpira wa Tanzania, DTB wao wana timu kabisa na; NBC bado kwa kiasi fulani.

NBC  kwa muundo wake wa ndani inaelekea kuwa sehemu ya ABSA Bank. Moja ya benki kubwa Afrika baada ya kuungana na Barclays Afrika. Kupitia ABSA, watakuwa na uzoefu katika kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania, kwakuwa wanadhamini Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Ni muda sahihi wa kumpata mdhamini mwenye afya ya kutosha katika ligi yetu, wote tunajua kuwa ligi yetu kwa sasa imeongeza umaarufu hasa baada ya Klabu ya Simba kufanya vizuri kimataifa na kuisaidia nchi kuingiza timu nne katika mashindano ya Afrika, maana yake umaarufu bado unaendelea, pili ni mafanikio ya timu yetu ya taifa hasa baada ya kufuzu Afcon.

Nafasi ya mdhamini mkuu ni kubwa katika ligi yetu ni kubwa, mdhamini mkuu atazisaidia timu kupambana na ukata ambao matokeo yake huwa ni upangaji wa matokeo, Mdhamini mkuu atatoa motisha kwa wliofanya vizuri, kwa kutoa zawadi nono kwa waliofanya vizuri wakiwemo wachezaji, makocha na waamuzi.

Sina hofu na watendaji wa TFF kupitia bodi ya ligi naamini msimu huu hawatoanguka tena, maana Waswahili walisema, mtu hupotea njia wakati wa kwenda tu na wala sio wakati wa kurudi.

Sambaza....