Mchezaji kinda wa Juventus Moise Kean jana amekutana na wakati mgumu baada ya mashabiki kumtolea maneno ya kibaguzi wakati timu yake ikiwa uwanjani ikipambana na Cagriali kwenye muendelezo wa ligi kuu nchini Italia.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 alionekana akiushika mkono wake baada ya kufunga bao la pili, tafsiri ambayo ilikuwa ikimaanisha kuwadharau wale ambao walikuwa wakimtolea maneno ya kibaguzi, lakini hali hiyo ilionekana kuzidi sana.
Baadae aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa ile ilikuwa njia pekee ya kuwajibu waliokuwa wanamtupia maneno ya kibaguzi.
Hata hivyo meneja wa Juventus na beki Leonardo Bonucci wamesema haikuwa njia sahihi ya Kean kuitumia ili kuonesha kuwa anakerwa na kitendo cha mashabiki kumbagua kutokana na rangi yake “Hakutakiwa kushangilia kwa namna ile, ni kijana mdogo anatakiwa kujifunza, lakini kuna maneno kutoka kwenye umati ambayo hakutakiwa kuyasikia,” Allegri amesema.
“Unashangilia bao na wachezaji wenzako, labda alitakiwa kushangilia kwa namna tofauti kidogo, nafikiria lawama ni 50-50, Moise hakutakiwa kufanya vile lakini pia mashabiki hawakutakiwa kujibu kwa namna ile pia.
Hata hivyo rafiki wa Moise, Blaise Matuidi alijaribu kuzungumza na mwamuzi wa mchezo huo Piero Giacomelli na kutishia kuondoka uwanjani baada ya mashabiki kuimba maneno ya kibaguzi, Matuidi aliwahi kulalamika kubaguliwa mwaka 2018 katika uwanja huo huo uliopo kwenye kisiwa cha Sardegna.
Baada ya Kean kufunga bao katika dakika ya 85 mchezo ulisimama kwa takribani dakika tatu na matangazo yakatolewa uwanjani hapo kuwaonya mashabiki kuacha kutoa maneno ya kibaguzi ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuwaonya kabla ya mchezo kuahirishwa.
Wakati huohuo Nahodha wa Cagliari Luca Ceppitelli alizunguka kwenye upande wa mashabiki wake na kuwasihi kuacha kutoa maneno ya kibaguzi.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Sardegna Juventus waliweza kuongeza wigo wa alama kileleni na kufikia alama 18 baada ya ushindi wa mabao 2-0 mabao ambayo yalifungwa na kijana Kean pamoja na beki Leonardo Bonucci.