Wakati shirikisho la soka nchini TFF likiuhairisha mchezo kati ya Simba na Biashara United uliotakiwa kuchezwa siku ya jumatano katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, kule nchini Congo, TP Mazembe nao walitakiwa kucheza siku ya jana dhidi ya Maniema Union lakini mechi hiyo nayo imehairishwa.
Sababu kuu za kuhairishwa kwa mchezo huo katika ligi kuu nchini Congo inayojulikana kwa jina la Linafoot, ni maandalizi ya TP Mazembe kuelekea mchezo wao wa marudio dhidi ya Simba Sc ya Tanzania katika mashindano ya klabu bingwa Afrika.
Mchezo huo ulioahirishwa, ni dhidi ya Maniema Union inayoshika nafasi ya 4 katika msimamamo wa Linafoot ikiwa na alama 54, na katika mchezo huo TP Mazembe wangekuwa ugenini.
Katika mchezo wa awali TP Mazembe walipata sare ya kutofungana ugenini, na sasa chama cha Soka nchini humo kimewapa muda zaidi wa kujiandaa na mchezo wa marudiano ili kuhakikisha klabu hiyo inasonga mbele katika hatua ya nusu fainali.
TP Mazembe chini ya kocha Pamhile Mihayo Kazembe,
inashika nafasi ya 2 katika msimamo wa
Linafoot ikiwa na alama 58 wakicheza michezo 23 nyuma ya vinara AS Club Vita
wenye alama 65 katika nafasi ya kwanza wakicheza michezo 25.