Nyota wa zamani wa Simba sc na KRC Genk Mbwana Samatta amemtaja mlinzi wa Liverpool na timu ya Taifa ya Uholanzi kama mlinzi mgumu zaidi aliekutana nae uwanjani. Licha ya kufunga mabao mawili pindi Genk walipokutana na Liverpool katika Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini Samatta hakusita kumpa sifa zake nyota huyo wa Uholanzi.
Mshambuliaji huyo aliesajiliwa na Aston Villa akitokea KRC Genk katika dirisha dogo mwezi January amezungumzia ni kwanini Virgil Van Dijk wa Liverpool ndiye mpinzani mgumu zaidi ambaye amewahi kukutana nao hapo awali.
Samatta “Virgil Van Dijk ndiye mchezaji mgumu zaidi ambae nimekutana nae. Nakumbuka wakati sisi (Genk), tulicheza kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool ilikuwa ngumu kumpita.”
Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania pia aliongea juu ya muda wake mfupi katika uwanja wa Villa hadi sasa, malengo yake na changamoto ambazo amekutana nazo England.
“Nimekuwa hapa kwa miezi mitano na ninajaribu kuzoea na kuwa mzuri kama wachezaji wenzangu. Ninafanya kazi kwa bidii kuisaidia timu kubaki kwenye Ligi Kuu. Siwezi kudhibitisha nini cha kutarajia lakini nitafanya kila kilicho bora kwangu.” Mbwana Samatta.
“Nadhani bado sijatulia kikamilifu lakini ninajaribu. Nadhani ninaendelea vizuri kwa sababu kama ninaanza kuelewa mambo mengi juu ya England na mpira wa miguu hapa, kilabu, wachezaji wenzake, na kila mtu karibu.” Alimalizia nahodha huyo wa zamani wa TP Mazembe.