Sambaza....

Mshambuliaji kinda wa Paris Saint-Germain Kylian Mbappe amesisitiza kwamba alitakiwa kufunga mabao mengi zaidi katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Lyon jana Jumapili licha ya kufanikiwa kufunga mabao manne pekee yake.

Mbappe mwenye umri wa miaka 19 amesema kama angekuwa makini kuanzia katika dakika za mwanzo basi angefunga mabao mengi zaidi kwani alikosa nafasi nyingi kama zile nafasi tatu za wazi ambazo kipa wa Lyon Anthony Lopes alimzuia kufunga.

“Nilipoteza nafasi nyingi, nilipaswa kufunga mabao mengi zaidi, naendelea kujifunza na kupambana, katu sijawahi kukata tama, nilijua nina support ya wachezaji wenzangu, mara zote nasema kama mshambuliaji kutengeneza nafasi ni kitu muhimu, mengine yote yanakuwa sawa,” Amesema.

Mbappe amekuwa na rekodi nzuri kwenye ligi kuu nchini Ufaransa (Ligue 1) mpaka hivi sasa akifunga mabao nane katika michezo mitano ambayo ameshuka dimbani mpaka hivi sasa, na anasema bado anakiu ya kufanya vizuri zaidi na kuendelea kuisaidia timu yake.

Vilevile ushindi wa jana unawafanya PSG kukwea kileleni kwa tofauti ya alama nane na kuvunja rekodi iliyodumu kwa miaka 82 iliyowekwa na Olympique Lillois mwaka 1936, huku Mbappe mwenye akiendelea kuamini kwamba anaweza kujiwekea rekodi ya kutwaa taji la ligi mara tatu mfululizo akiwa na timu mbili tofauti.

“Ni kazi ya wachezaji wote kwenye timu katika ushindi dhidi ya Lyon, lakini kitu muhimu zaidi ilikuwa ni kuvunja rekodi ya muda mrefu, nasisitiza tunazungumzia kuhusu umoja, tulitaka kushinda, tulihitaji kufikia hii rekodi kwa muda mrefu,” Amesema.

Ikumbukwe mpaka sasa PSG wameshinda michezo yote tisa ambayo wamecheza mpaka sasa katika ligi kuu nchini Ufaransa na kufanya ndoto za kunyakua ubingwa kuwa rahisi kwa upande wao kwa msimu wa pili mfululizo.

Bao lingine katika ushindi huo wa jana wa mabao 5-0 dhidi ya Lyon lilifungwa na Neymar kwa njia ya penati katika dakika ya 9 ya mchezo huo.

Sambaza....