Klabu ya soka ya Mbao ‘Wabishi’ umewatoa hofu baadhi ya mashabiki wa timu hiyo, wenye wasiwasi na uwezo wa kocha Ally Bushiri kuwa wanaimani kubwa na kocha huyo kuwa ataleta mafanikio yaliyoachwa na makocha Ettiene Ndayiragije na Amri Said.
Msemaji wa klabu hiyo Clisant Malinzi amesema wameuona uwezo wa kocha Bushiri toka katika mchezo wa kombe la Azam Federation Cup ambapo walitolewa na Dar City hadi katika michezo miwili ya ligi dhidi ya KMC na Kagera Sugar ambayo yote ametoa sare.
Malinzi amesema katika michezo miwili ya ligi kuu, ambayo walicheza na timu nguvu ndipo uwezo wa Ally Bushiri ulipojidhihirisha wazi na imani yao ni kuwa timu itaendelea kufanya vizuri hivyo mashabiki hawapaswi kulalamika kuondoka kwa kocha Amri Said aliyetimkia Biashara United.
“Ujio wa Ally Bushiri sisi tunaona umeleta chachu kubwa sana, ukizingatia tangu amefika hapa sisi tumesafiri kucheza game mbili ugenini, na michezo ambayo tulicheza na timu ngumu sana, timu hata ukiingalia inavyocheza sasa hivi ipo vizuri na imeongezeka baadhi ya vitu na hata baadhi ya wachezaji tuliwaongeza wanaonesha wazi wamekuja kwa ajili ya kuisaidia timu,” Malinzi amesema.
Bushiri
atakuwa na kibarua kizito Jumamosi hii kutafuta ushindi wake wa kwanza toka
atue Mbao FC pale atakapokuwa akiwakaribisha Alliance FC kwenye uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza.