Kikosi kamili cha Yanga kimeondoka leo asubuhi kuelekea nchini Algeria katika mchezo wa mkondo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhdi USM Algier.
Yanga watashuka dimbani majira ya saa nne usiku siku ya Jumamosi June 3 mwaka huu kwenda kutafuta ushindi baada ya kupoteza mchezo wa nyumbani kwa mabao mawili kwa moja na nyota wa Yanga Fiston Mayele amesema wao hawana cha kupoteza katika mchezo huo wa ugenini.
“Tangu nipo Tanzania mechi niliyocheza ikiwa na mashabiki wengi ni mechi ile ya juzi dhidi yao (fainali dhidi ya USM Algier), watu walikuwa wengi ni walitusapoti sana,” alisema na kuongezea “Kule kwao tumewahi kucheza na watu wakiwa wengi uwanjani nadhani wao ndio watakua na presha kwasababu watatakiwa wacheze vizuri na wawaonyeshe mashabiki wao, sisi tutakua hatuna cha kupoteza tunakwenda kutafuta matokeo,”
Pia Mayele amewaomba mashabiki wa Yanga wawe pamoja nao na kuwaombea ili waweze kurudi na kombe Tanzania licha ya tayari kuwa nyuma kwa bao mbili kwa moja.
“Mashabiki wa Yanga watusapoti na watuombee kwa Mungu ili mambo yaende vyema,” alimalizia Mayele.