Hapana shaka msimu ujao hatutakuwa na Makambo kwenye ligi yetu hii, na Yanga wanajua hilo na wanahangaika kila siku kutafuta mbadala wake.
Kuna taarifa kuwa aliyekuwa mchezaji wa Simba, Mavugo anatakiwa na Yanga. Je kama akija anaweza kufanya vizuri kuzidi Makambo, kwangu mimi jibu ni ndiyo, Mavugo ana ubora kuzidi Makambo , kwa sababu zifuatazo:
MIJONGEO
Moja ya vitu ambavyo vinamfanya Mavugo kuwa bora kuzidi ni Makambo ni mijongeo ya hawa wachezaji wawili.
Mavugo mara nyingi ana mijongeo ambayo humfanya atengeneze uwazi katika eneo la mbele kwa wachezaji wenzake.
Mavugo hawezi kusimama eneo moja kama Makambo. Kutosimama katika eneo moja huwafanya mabeki wa timu pinzani kumfuata mshambuliaji husika, wanapokuwa wanamfuata husababisha uwazi katika eneo la nyuma.
Uwazi huu hutumika na washambuliaji wengine kufunga. Ngoja nikupe mfano mdogo, Makambo msimu huu ana magoli 16 mwangalie mtu anayemfuata kwa idadi ya magoli pale Yanga.
Mchezaji anayemfuata kwa idadi ya magoli Makambo hafiki hata nusu ya magoli ya Makambo, unajua kwanini ? Makambo alikuwa hatengenezi uwazi kwa wachezaji wenzake wa mbele kwa muda mwingi kukaa eneo lake na kutofanya mijongeo.
KUKIMBIA NYUMA YA MABEKI
Mavugo ni mzuri kwenye eneo hili kuzidi Makambo. Mavugo anatabia ya kukimbia nyuma ya mabeki. Kuna faida kubwa kwenye hili kwa sababu hizi mbili.
Mshambuliaji anapokimbia nyuma ya mabeki humchanganya beki husika kwa namna mbili, moja beki huanza kufikiria namna ya kumzuia mshambuliaji aliye nyuma yake. Pili beki hufikiria namna ya kuzuia mpira ulio mbele yake. Kwa hiyo kumchanganya hivi beki humlazimisha kufanya makosa beki husika.
MIPIRA ILIYOKUFA
Mavugo ni mzuri kupiga mipira ya adhabu kuliko Mavugo hiki ni kitu kingine cha ziada ambacho kinamuongezea ubora Mavugo mbele ya Makambo.
KUKABIA JUU
Mavugo ni mzuri kuzidi Makambo kwenye Highpressing(kukabia juu). Unapokabia juu humfanya beki asiwe na uhuru wa kuanzisha mashambulizi kuanzia nyuma.
KUKABIA CHINI
Moja ya madhaifu ambayo Makambo alikuwa nayo ni kipindi ambacho Yanga inapokuwa haina mpira, Makambo siyo mzuri sana kwenye kukaba kipindi timu ikiwa haina mpira ukilinganisha na Mavugo. Mavugo huwa anashuka chini kuisaidia timu kukaba.
MWISHO
Mavugo alishindwa Simba kwa sababu mashabiki walimpa presha kubwa. Presha ambayo alishindwa kuimudu, Makambo kakuta mazingira tulivu ambayo yamemsaidia, kama Mavugo atakuta mazingira mazuri kama aliyoyakuta Makambo anaweza kuisaidia Yanga zaidi kuzidi Makambo.