Sambaza....

Golikipa wa Simba na timu ya taifa, Aishi Salumu Manula amesema kuwa uwepo magolikipa wengine wazuri ndani ya timu ya taifa na klabu sio changamoto kwake bali ni sehemu ya kutimiza majukumu yake ya kuhakikisha lango linakuwa salama.

Akianza na nafasi yake ndani ya timu ya taifa, Manula amesema kuwa uwepo wa Kaseja unaleta tija kubwa kwa taifa kwa sababu ya uzoefu na umahiri wake akiwa langoni hata nje ya lango.

‘…. Kuwa na Kaseja ni kitu kizuri, hata siku akistaafu kucheza, ana umuhimu wa kubaki timu ya taifa kwa sababu ni miongoni mwa magolikipa waliokwisha fanya makubwa kwenye nchi hii lakini pia bado wana muendelezo na mchango mkubwa kwa magolikipa wengine..’

Kwa mara ya kwanza Manula alikutana na Kaseja mwaka 2012 kwenye timu ya taifa. Manula amekiri kuwa ameendelea kujifunza kutoka  kwake tangu akiwa mdogo na hata sasa akiwa kama kipa namba moja wa Simba na timu ya taifa.

‘.. kwa hapa nilipofikia, Kaseja  ana mchango wake kwangu kwahiyo kamwe hawezi kuwa tatizo kwangu, ni furaha kuwa na mwalimu wako karibu..”

Akizungumzia upande wa Kakolanya, Manula amekiri kuwa na mahusiano mazuri na Beno tangu akiwa Prisons, timu ya taifa na hata Yanga. Kuhusu Kakolanya kuchukua nafasi yake, Manula amedai kuwa jicho lake ndilo jicho la klabu , anaamini kuwa Simba ilimsajili Beno sio kwa ajili ya kuua kiwango chake bali ni kushirikiana ili lango la Simba liwe salama zaidi.

Kakolanya akiwa Taifa Stars

‘…akifanya vizuri kwa nafasi yake na mimi nitakuwa nimefanya vizuri, mimi nikifanya vizuri kwa nafasi yangu, naye atakuwa amefanya vizuri kwa kuwa wote lengo letu ni kuifikisha Simba kule inakokutaka..”

Manula kwa sasa yuko nje ya uwanja kutokana na majeraha, hata hivyo anatarajia kuanza mazoezi mepesi leo.

Sambaza....