Sambaza....

Sikuwa na mpango wa kuyaamini maneno ya mwalimu wangu, siku moja aliposema  “ ukitaka kulijua vizuri soka la Tanzania, basi kwanza inatakiwa ulijue soka la nje kwa mataifa yaliyopiga hatua” lakini baada ya mkutano wa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji) na waandishi wa habari naanza kuyakiri maneno ya mwalimu wangu.

Si kwamba nilikuwa nimeyapuuza bali sikuruhusu moyo wangu ujiridhishe na maneno yake, wala sikuipa akili yangu muda wa ziada wa kufikiria maneno yake niliyoyaona yamejaa unazi kwa mataifa ya nje kuliko kwa soka la nyumbani.

Kama ulipata nafasi ya kumsikiliza Mo Dewji kuna vitu vingi utakuwa umevipata, vingi vikiwa vya matumaini na kutia msisitizo juu ya mambo Fulani Fulani nje na hata ndani ya klabu. Kwa uwelewa wangu mdogo nimeona sio mbaya nikuletee  tafsiri 6 za maneno yake katika mkutano wake wa waandishi wa habari.

Mo Dewji ikiwa ni mara yake ya kwanza kuongea na vyombo vya habari baada ya Simba kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji na kuwa mwekezaji mkuu wa klabu, alianza kwa kutoa shukrani kwa mashabiki wa klabu ya Simba, kwa kile alichokidai ni umoja na mapenzi ya dhati waliyoyaonyesha kwa klabu katika mechi zake mbalimbali za ligi na klabu bingwa Afrika.

Mo Dewji.

Pia aliishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika harakati zao zote katika mashindano ya klabu bingwa Afrika. Katika utangulizi wake huo alimalizia kwa kutoa pole kwa mashabiki wa Simba kwa vichapo mfululizo kutoka dhidi AS Club Vita na Al Ahly  kwa jumla ya goli 10.

Baada ya utangulizi wake huo, Mo Dewji aliendelea na kile kiini cha mazungumzo yake. Alitumia takribani dakika 25 kuzungumza na wana habari maneno mengi yaliyonishawishi kuandika makala hii. Maneno yake yamenipa tafsiri 6 kama ifuatavyo;

Maana ya kwanza, ni panga pangua na bomoa bomoa kwa wachezaji ipo karibu. Mo Dewji ameonekana kukazia maneno juu suala la nidhamu kwa wachezaji na kuahidi kuwa wale wanaomaliza mikataba yao wakiwa hawana nidhamu, hawataongezewa mikataba.

“wapo wachezaji ambao hawana nidhamu na huenda hawajitoi zaidi kwa klabu, hao mikataba yao ikiisha hatutaendelea nao la sivyo waonyeshe kubadilika”

Mo Dewji ameonyesha kuwa Simba inahitaji aina fulani ya wachezaji, kwanza lazima wawe na uzoefu na wa daraja la juu, wasiohitaji kufanyiwa majaribio na wenye uwezo wa kushindana na klabu yoyote Afrika. Mo ameona kuwa Simba inatatizo kubwa hasa kwa wachezaji kiasi cha kusema kuwa Simba ina wachezaji wanne pekee wenye uwezo wa kuimudu hatua ya makundi Afrika.

Wachezaji wasumbufu kama Juuko Murshid, Haruna Niyonzima na wengine kama nawaona yanaweza yakawakuta yaliyosemwa na Mo Dewji japo amewapa nafasi zaidi kama watakaokuwa tayari kutoa jasho na damu zao kwa ajili ya klabu. Huyo ndiye Mo Dewji bhana, harembi, na hata mfumo unampa hiyo jeuri.

Juuko Mursheed.

Jambo la pili,Timua timua za makocha kuendelea Msimbazi. Mo Dewji ameonesha dhahiri kuwa anataka klabu inayoendeshwa kwa malengo. Ukitaka kulijua hilo, usajili wa Patrick Aussems kama kocha mkuu ulipitia  mikononi mwa jopo la makocha wakongwe nchini kumfanyia mahojiano na kumbaini kama ana kitu cha ziada.

Kisha klabu ikamkabidhi kiti cha ukocha na kumpa malengo mawili ya klabu kwa msimu 2018-19 ambayo ni kwanza, kutetea ubingwa wa Tanzania bara ili kupata nafasi ya kushiriki tena klabu bingwa Afrika, na pili ni kuipeleka Simba hatua ya makundi, ambapo tayari hili limesha fikiwa,bado la kutetea ubingwa ligi kuu.

Mimi na wewe tusishangae kama hatutamuona Aussems akiwa  kocha mkuu wa Msimbazi msimu ujao kutokana na kile kilichoonekana kwa Mo juu ya utekelezaji wa malengo yaliyowekwa. Mo Dewji amedhirisha kuwa yeye ni mfanya biashara, kwa kuwa wafanyabiashara huwa hawapendi longolongo hasa pale wanaposhindwa kutimiza malengo waliyojiwekea.

Kocha wa Simba Sc, Aussems

Aussems akishindwa kutimiza lengo la msingi la klabu la kutetea ubingwa wake wa TPL ni lazima atafungashiwa mikoba yake, na hata mwingine atayekuja ni lazima apewe malengo ya timu kwa msimu husika naye akishindwa bila shaka atatimuliwa. Hii ina maana kuwa kuna uwezekano mkubwa Simba itakuwa na kocha mpya kwa kila msimu.

Tatu ni kukubali kuwa Simba ni “Underdog” katika kundi D. ni maneno tu ndiyo yanayoleta maana, Mo Dewji amelionyesha hilo kwa msisitizo kuwa Simba imepangwa katika kundi ambalo lina vilabu vizuri zaidi, kuanzia kwenye uendeshaji na hata pesa, hivyo viwango wa wachezaji wao wanaowasajili ni kubwa maradufu ukilinganisha na viwango vya wachezaji wa Simba.

“Ukiongelea Al-Ahly unaweza kuilinganisha na Real Madrid kwenye mataji, juzi wamenunua mchezaji kwa zaidi ya bilioni 10 na huyo mchezaji ametoa pasi za mwisho zaidi ya tatu kwenye mechi tuliocheza nao”

Kama ulikuwa hujui, Simba ipo kwenye kundi lenye vilabu viwili vilivyofika fainali za klabu bingwa Afrika na shirikisho katika  msimu ulipita. Fainali iliyopita klabu bingwa Afrika ilipigwa kati ya Esperence de Tunis na Al-Ahly, huku upande wa fainali za shirikisho zilimuhusisha AS Club Vita dhidi ya Raja Casablanca.

Kwa mujibu wa viwango vya Soka kwa  klabu za Afrika na duniani kwa ujumla, Simba inaonekana kuwa ya Mwisho katika kundi D. Al-Ahly wako juu, kwa Afrika ndio klabu ya kwanza kwa sasa, kwa dunia ni ya 91, na kwa Misri ni ya kwanza pia. AS Club Vita kwa Afrika ni ya 5, kwa kongo ni ya 2 na duniani ni ya 176. JS Saoura ni ya 53 kwa Afrika, ni ya 4 kwa Algeria na ni ya 644 kwa dunia.  Wakati Simba ni ya 326 kwa Afrika, ya 1 kwa Tanzania na ni ya 1817 kwa dunia.

wachezaji wa Al-Ahly.

Viwango hivyo vya soka vinaonyesha kuwa, Simba ina utofauti mkubwa sana ukilinganisha na vilabu vingine katika kundi D. Mo Dewji amekiri utofauti huo na kuonesha kuwa hawana mpango wa kuwekeza sana katika hatua hii kwa kuwa ni nje ya malengo ya timu.

Jambo la nne, ni Simba kuwa klabu kubwa Afrika. Kila mtu anaruhusiwa kuwa na ndoto, tofauti inakuja kwenye utekelezaji wa ndoto hiyo, ndivyo ilivyo kwa tajiri Mo Dewji na ndoto zake za kuijenga Simba kuwa klabu kubwa. Kwa kinywa chake amesema kuwa, ndoto zake ni kuibebesha Simba taji la klabu Bingwa  Afrika, Simba kuwa miongoni mwa vilabu vitano vikubwa Afrika, na mwisho ni Simba kujijengea uwezo binafsi (sustainability).

“ndani ya miaka mitano ijayo ndoto yangu, bodi na wanasimba kwa ujumla ni kuwa mabingwa wa Afrika na hilo linawezekana”

Katika kufanikisha hilo Mo Dewji amesema kuwa wao kama bodi ya wakurugenzi wamekuja na  mipango mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu. Mipango ya muda mfupi ni kubeba taji la TPL, ya kati ni kumiliki uwanja wa klabu na Academy mbalimbali, kuimarisha benchi la ufundi likiwa limekamilika yaani kuwa na  vitengo vingi vya kitaalamu.

“benchi la ufundi tunahitaji likamilike sio kocha msaidizi tu, tutakuwa na mkurugenzi wa ufundi, watu wa Saikolojia na idara nyingine pia ziwe na wataalamu wa mpira”

Simba itaongozwa na kuendeshwa kama zinavyoendeshwa Real Madrid na Man U na vilabu vingine vikubwa duniani.  Haya yote ni kutimiza lengo la muda mrefu la kuifanya Simba kuwa miongoni mwa timu bora 5 barani Afrika. Hii ndio ramani iliyojichora katika ubongo wa Mo Dewji, ramani yenye matumaini mengi kwa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Je ramani hii itakuwa imechorwa kwa penseli kwa maana itafutika mapema au kwa kalamu ya wino inayovujaa? Mimi na wewe tusubiri.

Maana ya tano, ni kwamba Mo Dewji alikuja kumsafisha Haji Manara kwa mashabiki wa Simba. Jiulize maswali yafuatayo (hasa mkutano na waandishi)  ili kunielewa ninachokimaanisha, Simba ina viongozi wengi akiwemo msemaji wa klabu kwanini Mo Dewji? Mo Dewji ameongea nini hasa mbali na kuwashawishi mashabiki wajae uwanjani? Kwa kile kilichotokea kati ya Msemaji wa klabu na mashabiki, unahisi ni nani mwingine mwenye uwezo wa kuwashawishi mashabiki nje ya Manara?.

Manara na Mo Dewji(Mwekezaji)

Asante! Manara hakuwa na uwezo wala nguvu tena ya kuujaza uwanja kwa kutumia ushawishi wake, maana mashabiki walishaanza kumpuuza na wakiamini kuwa wao ni wazalendo kwa klabu kuliko hata msemaji wao. Mo Dewji aliliona hilo ndio maana, mkutano na waandishi wa habari, aliuita yeye kwa kuwa alijua wazi kuwa, Manara tayari ameshapoteza umaarufu na ushawishi.

Maneno ya Mo, yalidhihirisha hiki ninachokwambia kwa maana, Mo alilazimika kuchukua nafasi ya Manara japo haku-fit , ndio maana katika kuhakikisha anarudisha imani kwa mashabiki alilazimika  kutaja vipaumbele vyake kwa klabu. Vipaumbele hivyo ni kama  ahadi kwa mashabiki. Na ni kweli mashabiki watajitokeza hiyo tarehe 12, na huo ndio utakuwa mwanzo wa Manara kuamka tena japo atakuwa anachechemea na hajachangamka kama hapo awali.

Sita, kupata kazi katika klabu ya Simba ni mchakato. Mo Dewji amelisistiza hilo na kuwaahidi watanzania wenye taaluma  mbalimbali wakae tayari kwa ajili ya kuomba nafasi za ajira klabuni hapo hivi karibuni lakini pia wajiandae kuhojiwa na wataalumu katika taaluma husika ili kupata walio sahihi zaidi.

“pia hivi karibuni tutatangaza nafasi za kazi kwa watu wenye taaluma mbalimbali kwenye mpira ili katika mabadiliko haya ya mfumo tuweze kufanya uwekezaji ulio sahihi ili kufikia matarajio yetu kama klabu”

Yale mambo ya “kujuana” bila shaka yatakuwa ni mwisho, yaani kila atakayeajiriwa lazima awe mtaalamu katika kitengo fulani. Hii ndio dhana halisi ya mpira wa kisasa ni biashara, hakuna anayependa kuajili mfanyakazi hovyo na ampe hasara.

Hii ni ule muendelezo wa ramani ya Simba ijayo chini ya Mfumo mpya wa uendeshaji katika akili ya Mo Dewji. Kama ndoto hizi zitatimia ujue kabisa Simba inaenda kuwa klabu kubwa Afrika, yaani usajili kuanzia kwa wachezaji, makocha na wengine katika idara ya benchi la ufundi na uendeshaji lazima wapatikane kwa mchujo ulioenda shule.

Mwisho kabisa, Mo Dewji aliwapongeza waandishi wa habari kwa kuandika vizuri kuhusu Simba, kiasi cha kuwatia moyo wachezaji. Japo hili nalo linaweza kuwa tatizo kama tu, waandishi wataandika vizuri tu bila kuangazia mapungufu ya timu kiufundi. Ukweli unaifanya klabu  ijue na mashabiki wajue kinachoendelea.

Mwekezaji mkuu wa Simba, Mo Dewji na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Kassim Majaliwa wakiwa uwanja wa taifa.

“Mimi nina imani siku ya jumanne tutashinda dhidi ya Al-Ahly niwaombe sana mashabiki waje uwanjani mimi nitakuwepo na kiingilio tumeona kiwe shilingi 2000 ili wanasimba wote waje kwa nguvu timu yao”

Maneno yote ya MO yanamaanisha mashabiki wajitokeze uwanjani kuishangilia Simba ili ipate matokea mbele ya Al Ahly ili kufufua ndoto za kusonga mbele katika kundi D. Kiingilio kidogo kabisa ni 2000, lengo ni kumuongeza mchezaji wa 12 uwanjani. Bila shaka mashabiki na wadau wa soka nchini watakuwa wamemuelewa vizuri MO.

Sambaza....