Sambaza....

Hapana shaka Manchester United ilikuwa alama halisi ya mafanikio katika mpira wa England. Hawa ndiyo walikuja kutoa utawala wa Liverpool na kuja kuweka utawala wao.

Utawala ambao uliwafanya wajimilikishe kila kitu ambacho walikuwa wanakitaka. Na hapa walikuwa chini ya Sir. Alex Ferguson. Mtu mwenye mbinu nyingi za kushinda.

Utawala wao ulianza kuingiwa na walakini baada ya Sir. Alex Ferguson kuamua kukaa pembeni, hapa ndipo ukawa mwanzo wa Manchester United kupoteza urembo wao, kama ilivyo katika maisha ya kawaida kila zama huwa na kitu chake. Mrembo Manchester United ameanza kuchakaa na Manchester City amekuwa ndiye mrembo anayevutia.

Leo hii wanakutana, mrembo wa zamani na mrembo wa sasa.

UPI UIMARA WA MANCHESTER CITY?

Mara nyingi Manchester City hutumia mfumo wa 4-3-3. Ambapo wachezaji wapembeni (Sane na Sterling) huwa wanakaa pembeni muda mrefu, hii huwa inasababisha mabeki wa pembeni wa timu pinzani kuvutika kuja kuwakaba pembeni.

Wanapovutika pembeni kwenda kuwakaba wachezaji hawa wawili wa pembeni, huacha uwazi eneo la nyuma. Uwazi ambao huwasaidia viungo wawili wa kati kuutumia ( Bernardo Silva na David Silva).

Na hii huongeza idadi ya wachezaji wa Manchester City kule mbele. Idadi hufikia watu watano kule mbele. Pia mabeki wa pembeni wa Manchester City Mara nyingi huja katikati ya uwanja kuziba nafasi ya kina Bernardo Silva na David Silva ambao hupanda mbele kushambulia. Kwa hiyo Manchester City inapokuwa inashambulia inakuwa na umbo la 2-3-5

Mendy

SILAHA YA KUJILINDA YA MANCHESTER CITY NI IPI ?

Manchester City inapojilinda hurudi katika umbo lake halisi la mfumo wa 4-3-3. Lakini kipindi cha kujilinda huwa inakuwa na udhaifu sana katika upande wa kushoto, kwa Benjamin Mendy ambaye huchelewa kushuka , hivo kuna wakati eneo la kushoto la Manchester City huwa na uwazi sana eneo hilo la kushoto. Manchester United wanatakiwa kutumia udhaifu wa Manchester City upande wa kushoto.

UPI UDHAIFU WA MANCHESTER UNITED.

Manchester United na wao hutumia mfumo wa 4-3-3. Kwa msimu jana Manchester United ilikuwa timu ambayo ilikuwa imeruhusu magoli machache nyuma ya Manchester City ambaye alikuwa bingwa.

Msimu huu wamekuwa wakiruhusu sana magoli. Na hii inasababishwa na kitu kimoja, nacho ni uwazi mkubwa ambao unatengenezwa kati ya eneo la kiungo na eneo la ulinzi.

Martial

Viungo wa kati wa Manchester City hujikuta sehemu moja kwa pamoja. Na hii huleta uwazi mkubwa kati ya eneo la kiungo na ulinzi.

Kitu ambacho husababisha mzigo mkubwa sana katika eneo la ulinzi kwa kuruhusu idadi kubwa ya mashambulizi. Ndiyo maana msimu huu wameruhusu magoli mengi, wana wastani wa kuruhusu goli 2 kwenye kila mechi ambayo wanacheza msimu huu.

KIPI WAKIFANYE MANCHESTER UNITED ILI WASHINDE MECHI HII?

Katika mechi dhidi ya Chelsea na Juventus, Manchester United katika kipindi cha kwanza walikaa nyuma ya Mpira na kuwaruhusu (Juventus na Chelsea) kuwa na Mpira, lakini kipindi cha pili walifanya kushambulia kwa kushtukiza. Na mwisho wa siku Manchester United wakapata ushindi.

Hiki ndicho kitu ambacho Manchester United wanatakiwa kufanya. Silaha kubwa kwao wao ni kujilinda muda mwingi mwa uwanja na kushambulia kwa kushtukiza.

UBORA WA MANCHESTER UNITED NI UPI?

Kama nilivyosema hapo juu, Manchester United wamekuwa wazuri sana wanapofanya mashambulizi ya kushtukiza kutokana na aina ya wachezaji ambao wako nao.

Sambaza....