Sambaza....

Aliekua msemaji wa zamani wa vilabu vikongwe nchini Simba na Yanga Haji Manara ameonyesha masikitiko yake kwa watu wanaomsema vibaya nahodha wa Simba John Bocco kutokana na fomu yake mbaya aliyokua nayo kipindi hiki.

Kupitia ukurasa wake wa instagram Manara ameandika ujumbe mzito kwenda kwa mashabiki wa soka huku akionyesha wazi kusimama na John Bocco.

“Naandika kama Mwanahabari mbobezi wa football nchini. Kuna vitu vinaumiza sana kuona mchezaji kama huyu (Bocco) hapewi heshima yake na washabiki wasiojua kitu wa Simba, timu yao ikifanya vibaya Bangusilo wao ni capteni wao John Bocco. Ni upuuzi ni kutowapa “respect” wachezaji waliofanya makubwa katika soka nchini, ni zaid ya undumilakuwili na kukosa heshima kunakofaa kukemewe.

Katika kizazi hiki cha sasa, nani kafunga kumzidi yeye nchi hii katika Premie league? Mpeni heshma anayostahili huyu mtu, tukiwa wote pale (Simba) kashinda vikombe vingapi kama captain?,” alisema Haji

Pia Manara aliongeza “Kwangu mimi hata kocha wenu kumtoa juzi na Waarabu ni uchale wake tu, uwepo wake uwanjani siku ile ndio ulikuwa unafanya hata mpira ukae kule mbele na aliwapa tabu sana mabeki, ni kama kakariri zile substitutions zake za michongo.

Hakuna kitu sikipendi na siwezi kukikalia kimya kama kuona heshima ya wachezaji inanajisiwa , tena wanajisi wenyewe ni watu wasiojua lolote kuhusu football, watu ambao hata danadana mbili kupiga hawawezi.”

Msemaji huyo wa zamani wa Simba pia alionyesha anatamani mafanikio ya Bocco lakini si kwa kumuombea mema yeye na timu yake ya Simba.

Haji Manara

“Ipo hivi captain, wewe ni star na endelea kupuuza maneno yao, baki hivyo ulivyo na beba hizo lawama kama changamoto tu, potezea mwamba.

Siwezi kukuombea mazuri wewe na wenzio mkiwa uwanjani na timu yenu , lakini kama rafiki yako nitaendelea kukuheshimu daily , Kwa unachoendelea kutoa Kwa ajili ya football ya nchi hii.” Haji Manara

Kwasasa John Bocco yupo nchini Uganda na klabu yake ya Simba kuelekea mchezo dhidi ya Vipers ya Uganda baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya awali huku wakiwa hawajafunga bao lolote mpaka sasa.

 

Sambaza....